Bwawa la Nyerere, SGR na daraja la Busisi vyaipaisha NIC, yajitosa MV Mwanza

Mwanza. Miradi mikubwa ya kimkakati likiwemo Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR) na daraja la Kigongo –Busisi vimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu za kulifufua Shirika la Bima la Taifa (NIC), lililokuwa limekimbiwa na wateja na kuliimarisha kiuchumi.

Katika kipindi cha ujenzi na baada ya kukamilika kwa miradi hiyo mikubwa, shirika hilo lilipewa dhamana ya kukinga bima za miradi hiyo, jambo ambalo limeimarisha mtaji wa NIC na kufikia Sh15 bilioni na kulifanya kuwa miongoni mwa mashirika yenye mtaji mkubwa nchini, huku likiwa na dhamana na mali zinazofikia zaidi ya Sh292 bilioni.

Hayo yameelezwa leo Mei 27, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Bima la Taifa (NIC), Justine Mwandu wakati akizungumza na wateja wa shirika hilo na baadhi ya taasisi za umma na binafsi jijini Mwanza, wakati wa ziara ya kutembelea na kuwashukuru wateja waliolivumilia na kuimarisha uhusiano.

Mwandu amesema baada ya soko la bima nchini kuwa huria shirika hilo liliyumba na kukimbiwa na wateja, lakini baada ya Serikali kulipa kipaumbele kwenye miradi mikubwa ya kimkakati kwenye kutoa kinga ya bima limeimarika na sasa kipaumbele ni kuendelea kuaminika kwenye miradi mingine, inayoendelea kukamilika ukiwemo mradi wa ujenzi wa meli ya MV Mwanza.

“Kwa kweli hii imeweza kunyanyua sana NIC kimapato na kuileta katika hali ya kifedha ambayo sasa hivi tunaweza kusema tunaringa kwamba iko katika hali nzuri. NIC ina mtaji wa kutosha, Serikali ilikubali kutuongezea mtaji kupitia faida zetu na tuna mali na uwekezaji kwenye dhamana za benki na Serikali,” amesema Mwandu.

Mwenyekiti huyo amesema kutokana na uimara huo wa kiuchumi kwa sasa shirika hilo halidaiwi na wateja ama kuchelewesha malipo ambayo nyaraka husika zimekamilika, kwani limekuwa likihakikisha linalipa madai yote ndani ya siku saba.

“Hivi karibuni mtazindua meli kubwa ya MV Mwanza tutaomba mtuletee kwa ajili ya huduma ya bima, sisi nia yetu ni kwamba kama bodi tunawahakikishia tuko tayari kuwapa huduma ya bima kama inavyostahiki na kuongeza mashirikiano,” amesema Mwandu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Erick Hamis akizungumzia huduma ya bima katika mradi wa meli ya MV Mwanza, amesema sehemu kubwa ya meli za kampuni hiyo zinalindwa na bima za Shirika la Bima la Taifa (NIC) na wako tayari kushirikiana kwenye mradi huo mpya ambao umefikia asilimia 98 za ujenzi, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo.

“Moja kati ya jambo ambalo tunalihitaji sasa hivi ili kupata leseni ya usafirishaji kutoka Mamlaka ya Usafiri Majini (Tasac) ni bima, kwa hiyo wamekuja wakati muafaka ambapo tunahitaji bima kama moja ya masharti ya kukamilisha meli iweze kubeba abiria. Watafanya hesabu aina ya gharama tutakazolipa ili tupate hiyo bima na kuifanya meli itembee tukiwa tumepata vibali vyote,” amesema Hamis

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amelishauri shirika hilo kutokuwa tegemezi kwenye miradi ya Serikali ambayo wana uhakika wa kuipata na badala yake watoke nje, washindane na kuchangamkia fursa kwa wateja, taasisi na miradi ya watu binafsi likiwemo soko kuu la Mwanza lenye zaidi ya thamani ya Sh20 bilioni.

“Mko sokoni msilale mna ushindani, miradi ya Serikali  mnaweza kuwa na uhakika wa kuipata lakini miradi binafsi lazima muichangamkie. Kwa kuwa ni taasisi ya Serikali tumieni utaalamu wenu na uhakika wa mtaji mkubwa mlionao kushawishi wadau,” amesema Mtanda.

Related Posts