Katavi.Wakati mwelekeo wa Taifa sasa ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu ujuzi ili kumuwezesha kikamilifu kwenye shughuli za kujenga uchumi, hali iko tofauti katika Halmashauri ya Mpimbwe iliyopo mkoani Katavi.
Katika eneo hilo linalokaliwa na jamii za Wasukumu bado kuna kilio cha mila potofu ya chagulaga inayosababisha wasichana wakatishe masomo na kuangukia kwenye ndoa za utotoni.
Mila hii si ngeni masikioni mwa wenyeji wa mikoa ya kanda ya ziwa na ile inayokaliwa na idadi kubwa ya Wasukuma, ambapo binti hulazimishwa kumchagua mwanaume bila kujali umri wake hata kama ni mwanafunzi.
Ajabu ni kwamba imekuwa ikipigiwa kelele kwa miaka mingi kuwa haifai lakini hadi sasa bado kuna jamii zinaitekeleza na kuipa heshima kubwa licha ya kuathiri ustawi wa mtoto wa kike.
Kutokana na mila hiyo hali ya elimu kwa watoto wa kike katika halmashauri ya Mpimbwe imekuwa ya kusuasua changamoto inayogonga vichwa vya wanaoamini katika elimu.
Kwa mujibu wa Spitali Kijika ambaye kwa asili ni Msukuma, mila hiyo hutekelezwa na jamii ya Wasukuma wa makoja na si Wasukuma wote kama inavyofikiriwa na wengi.
Anasema kinachofanyika vijana hujipanga na kumtaka msichana achague mmoja wao na hilo wakati mwingine hufanyika kwa lazima kulingana na rika la vijana husika hasa kama wako kwenye shauku ya kupata wenza.
“Vijana wanakuwa wengi wanamvizia msichana mmoja na kumtaka achague mmoja wao, wananyoosha mkono na ikitokea binti amekamata mkono wa kijana mmoja huyo, ndiyo anakuwa amemchagua sasa mazungumzo yanaanzia hapo hadi kurasimisha kuwa ndoa.
“Kwa wengine inaonekana jambo la ovyo ila wenyewe wanaiheshimu sana na ikitokea binti hajawekwa kwenye mazingira ya kuchagua mwanaume, mzazi wake anaweza kwenda hata kwa mganga kusafisha nyota. Ikitokea binti anatakiwa sana kuchagua mwanaume kwa mzazi hiyo ni sifa,” anasema na kuongeza:
“Wapo wazazi ambao ikitokea binti yao mwanafunzi amechaguliwa, wanamshawishi afanye vibaya kwenye masomo ili akaolewe hawataki kupoteza hiyo nafasi ya binti yao kupendwa”
Hata hivyo, Kijika ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mirumba kilichopo kata ya Kibaoni halmashauri ya Mpimbwe anakiri kuwa imani hiyo imekuwa ikitendwa ndivyo sivyo, kwani vijana wa sasa huishia kujihusisha kimapenzi na wasichana wanaowachagua au kuwatorosha bila kufuata taratibu ikiwemo kupata ridhaa ya wazazi.

Mwanafunzi wa kidato cha nne sekondari ya Chamalendi Felista Mabula (19) ni miongoni mwa wasichana walionusurika kuangamizwa na mila hiyo akieleza kuwa ni kikwazo kwa wasichana wengi hasa wanafunzi.
“Niliwahi kukutana na kundi la vijana wa kiume nikiwa natoka mashine kusaga, nilipatwa na hofu nikajua kwamba ndiyo itakuwa hatima yangu kama ambavyo imewahi kuwatokea wasichana wenzangu.
“Wale vijana walinizonga wakaanza kunilazimisha nichague mmoja wao, nikawajibu kwamba mimi sina mpango wa kuanzisha uhusiano wala kuingia kwenye ndoa kwa sasa kwa kuwa bado ni mwanafunzi.Hawakunielewa waliendelea kunilazimisha nichague bahati nzuri mmoja wao akanitambua na kuwaambia wenzake waniache,” anasema Felista.
Kueleweka kwa utetezi wake kwamba yeye ni mwanafunzi ilikuwa kama bahati ya mtende kwani wapo wasichana wenzie ambao walilazimika kukatisha masomo baada ya kukumbana na vijana wa chagulaga.
“Ni mila ambayo inatutesa sana wasichana kwenye jamii za kisukuma, nasi tunatamani kusoma ili tutimize ndoto zetu lakini huu utamaduni unatulazimisha kuacha masomo na kuingia kwenye ndoa.
“Bahati mbaya ni mila inayobarikiwa na wazazi, wao wanafurahi binti akichaguliwa wanachowaza wao ni ng’ombe ndiyo maana wenzetu wengi tulianza nao shule lakini walikatisha masomo na sasa wameshaolewa na kuzaa katika mfumo huu huu,” anasema Felista.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Chamalendi Dedan Msabi anathibitisha kuwa mila ya chagulaga ni chanzo kikubwa cha mdondoko wa wanafunzi hasa wasichana.
Akitolea mfano wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2024 walianza kidato cha kwanza mwaka 2021 wakiwa 123 ila ni 48 pekee ndiyo waliohitimu elimu ya sekondari.
Kwa upande wa wanafunzi kidato cha nne ambao wanatarajiwa kuhitimu elimu ya sekondari mwaka huu anasema walianza wakiwa 158 lakini hadi kufikia Januari mwaka huu walioendelea na masomo walikuwa 67.
“Hili ni suala linalotusumbua sana, wasichana wengi wanakatisha masomo kwa sababu ya mila hii, wengine wanahofia kuja shuleni kwa sababu njiani ndiko vijana hawa wanakojipanga wakisubiri wasichana na kulazimisha kuchaguliwa.
“Tena wakati mwingine ni afadhali wakiwaona na sare za shule wanahofia kuwasumbua, lakini kama msichana amevaa tu nguo za nyumbani anaendelea na shughuli zake kijijini ni rahisi kusombwa na akapotelea huko,”
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwaroko, anakiri kuwa halmashauri yake ina mdondoko mkubwa wa wanafunzi unaosababishwa na mila na desturi, akitolea mfano wa mila hiyo ya chagulaga ambapo wasichana huingizwa kwenye ndoa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.
“Tunakiri kwamba hii ni changamoto kubwa na ina athari sana inawezekana darasani wakaanza watoto 100 lakini wakamaliza 80. Jitihada zinafanyika ikiwemo kuelimisha wananchi.
Pia tunafanya kazi kubwa kuelimisha hata hao watoto wenyewe waelewe umuhimu wa elimu kwa sababu tumebaini hata wao wenyewe ni rahisi kushawishika wakatishe masomo wakaolewe,”anasema Shamimu.
Naye Mkurugenzi wa miradi na ushirikiano wa shirika linaloshughulika na wasichana na Camfed, Anna Sawaki anasema ndoa za utotoni ni kikwazo kikubwa katika jitihada za kuwakomboa watoto wa kike.
“Ili kutatua changamoto hii inapaswa kufahamika kuwa hili ni suala mtambuka, inamhitaji mtoto mwenyewe kujitambua. Ni wakati sasa wazazi, shule na jamii kwa ujumla tufikirie kuwawezesha hawa watoto kupata stadi za maisha. Anaweza kufaulu masomo darasani lakini kama hana elimu ya stadi za maisha, inaweza kuwa changamoto kwake kupita kwenye vipindi mbalimbali vya mpito.