Dk Tulia: Tuombee uchaguzi, viongozi wapatikane kwa haki

Hai. Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson ametumia mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Askofu Immanuel Lazaro kuwataka Watanzania kuliombea Taifa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili viongozi wapatikane kwa haki.

Kauli hiyo ameitoa leo Mei 27, 2025 wakati akitoa salamu za Serikali katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa la  TAG-Jerusalemu Mudio, lilipo katika kata ya Masama, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Askofu Lazaro ambaye alizaliwa Oktoba 4, 1937, alifariki Mei 17, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC, siku na mwezi sawa na aliyofariki mke wake, Evagrace mwaka 2017.

Askofu Lazaro ambaye amezikwa leo Mei 27,2025 katika eneo la Kanisa la TAG -Jerusalemu Modio Masama, alianza huduma za kiroho mwaka 1959, na mpaka anastaafu huduma hiyo mwaka 2019 alikuwa amefikisha miaka 60 ya utumishi wake.

Alifanya huduma katika mazingira magumu akitembea kwa miguu, baiskeli na pikipiki mara nyingi kutoka Mkoa wa Mbeya hadi Kilimanjaro katika kutekeleza majukumu yake ya kiaskofu

Ibada hiyo ya maziko imehudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa dini na Serikali, baadhi ya maaskofu na wachungaji wameelezea namna walivyomfahamu Lazaro enzi za uhai wake na alivyosimama kueneza injili ndani na nje ya nchi.

Akiendelea na salamu za Serikali  Dk Tulia, amewataka pia Watanzania kuwaombea viongozi watakaopatikana kwa haki  katika uchunguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani.

“Kwa sababu huko mbele tunao uchaguzi niwaombe sana, pamoja na kwamba huwa mnatuombea sana sisi viongozi lakini pia mnaliombea Taifa letu,  niwaombe mwaka huu tuliombee zaidi Taifa letu, mwaka huu tuwaombee viongozi watakaopatikana kupitia uchaguzi wa haki,”

Amesema, “lakini hao watakaopatikana kwa haki Biblia imetuagiza kuheshimu wenye mamlaka, ni vizuri sana sisi tumjuao Kristo kupanga nini cha kusema, cha kufanya, kujua namna ya kuenenda mbele ya viongozi wetu, wewe umjuaye Kristo usiwe sehemu ya kulikosea neno.”

“Wakati mwingine Mungu atatupa neema, hata  wale wafalme wa zamani, sasa hivi ni viongozi wa nchi zetu kwa hiyo unavyowasoma wale na yale mamlaka yao na nguvu yao amini kwamba neno linaposema umuheshimu mwenye mamlaka ni kwa sababu hakuna mamlaka isipokuwa itokayo kwa Mungu,”amesema Dk Tulia.

Pamoja na mambo mengine, amesema Askofu Lazaro alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa dini waliotumia nguvu kubwa kuliombea Taifa ili  liendelee kuwa salama.

“Tujifunze kwa baba huyu aliyelala, alikuwa ni mtu wa kujishusha, sio mtu wa kujikweza, wala wa maneno mengi, wala hutasikia kauli yake mpaka uwe umemtafuta, sisi tujifunze huko, lakini pia yeye ametupa masomo mengine, “amesema Dk Tulia.

Akihubiri katika ibada hiyo ya mazishi, Makamu wa Askofu Mkuu wa TAG, Dk Magnus Mhiche amesema Askofu Lazaro licha ya kwamba aliugua kwa muda mrefu alikuwa bado akilipambania kanisa hilo, na kuwataka viongozi wengine kuiga maisha yake.

“Baba huyu aliyelala hapa licha ya kwamba alikuwa ni mgonjwa kitandani  kwa muda mrefu aliendelea kulipambania kanisa lake, na alikuwa akihimiza upendo na mshikamano siku zote, sisi kama viongozi na wananchi tuendelee kujifunza kwake,”amesema Dk Mhiche

Amesema kama kanisa wataendelea kumuenzi Askofu Lazaro na kuendeleza yale yote aliyo yaasisi katika kanisa hilo.

Akizungumza Diwani wa Kata ya Machame Magharibi, Martine Munis amesema wamempoteza baba wa kiroho, ambaye alisimama kuliombea Taifa na kuhakikisha linakuwa salama.

“Aliyelala hapa ni miongoni mwa wazee walioliombea Taifa hili na usalama uliopo Tanzania, tutajivunia kwa sababu ya wachungaji, amani, mshikamano wa Taifa hili umetokana na wazee kama huyu ambao hawakuwa na matamko ya kisiasa bali walipoona mambo hayaendi vizuri walikimbilia magotini kwa Mungu, maana ndipo ulipo usalama wa nchi hii” amesema Munis.

Ameongeza kuwa, “waombaji ndiyo wenye usalama wa nchi hii, na hapa amelala baba ambaye alikuwa na mchango mkubwa wa kiroho, tutamkumbuka daima na mchango wake mkubwa wa kuwalea watu kiroho.”

Related Posts