Unguja. Mapato yanayotokana na viwanja vya ndege Zanzibar, kwa kipindi cha miaka mitatu yameongezeka kutoka Sh18 bilioni hadi kufikia Sh50 bilioni, huku mikakati ikizidi kuwekwa kuimarisha viwanja na kujenga vingine vipya.
Ongezeko hilo linakwenda sambamba na abiria wanaopitia kwenye viwanja hivyo ambao wamefikia milioni 2.4 mwaka 2024 kutoka abiria 1.9 mwaka 2023 sawa na asilimia 23.
Akizungumza leo Mei 27, 2025 baada ya kupokea ndege ya kampuni ya Ufaransa ambayo ilikuwa imesitisha safari zake tangu Machi mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa viwanja vya ndege Zanzibar, Seif Abdallah Juma amesema wanatarajia kupokea abiria 2.7 mwaka huu.
“Tumejipanga kuratibu uingiaji wa wageni, mwaka 2023 uwanja uliingiza abiria milioni 1.9 lakini imeongezeka kwa asilimia 23 na kufikia abiria milioni 2.4 kwa hiyo mwaka huu tutapokea zaidi ya abiria milioni 2.7 hivyo tumejipanga kimiundombinu na kutoa huduma bora zaidi katika ushindani mkubwa wa sekta ya anga,” amesema Seif.
Amesema mapato kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yameongezeka kwa asilimia 200, mwaka 2023 walikusanya Sh18 bilioni lakini kwa sasa wamefikisha Sh50 bilioni, “kwa hiyo utaona mabadiliko makubwa ya mapato yanakusanywa kupitia viwanja vya ndege Zanzibar.”
Akizungumzia ujio wa ndege hiyo ya Air France yenye uwezo wa kubeba abiria 275, Seif amesema ilisitisha safari zake Machi mwaka huu kwa sababu ya kupungua kwa wageni (Low season).
“Kwa kipindi cha miezi miwili wamesitisha safari zao Zanzibar lakini leo wamerudi na ndege ileile itakuwa inakuja mara tatu kwa wiki ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 275, kwa hiyo tutegemee huduma za moja kwa moja kutoka Ufaransa hadi Zanzibar,” amesema.
Kwa mujibu wa Seif kuna kampuni zaidi ya 78 ambazo zinaleta ndege kisiwani humo na msimu wa wageni wengi umeanza vizuri na wanatarajia kuwa na mashirika mengi zaidi ya hayo kuanzia Juni na Julai, hivyo sekta hiyo ya anga na utalii kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar.
Katika kufikia azima hiyo, mkurugenzi huyo amesema Zanzibar itaendesha mkutano mkubwa wa maendeleo ya sekta ya anga Afrika (Aviadev), unaotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.
Mkutano huo utayakutanisha mashirika 50 kutoka duniani kote ukiwa na washiriki zaidi ya 500.
“Mkutano huu utahusisha wadau wa sekta ya anga duniani kwa maana ya kwamba mashirika ya ndege, wajenzi wa ndege na watoaji wa huduma za ndege na wadau wa sekta ya watalii, kwa hiyo watakuja kuungana katika kukuza sekta ya anga na sekta ya utalii,” amesema.
Mdau wa utalii kisiwani humo, Haji Ali Haji amesema miundombinu inazidi kuimarika na ndio maana kunakuwapo na mabadiliko makubwa katika sekta hiyo, huku akishauri kuendelea kuboresha zaidi ili kupata wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali.