Mtoto mbaroni akidaiwa kuiba gari la mwalimu

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linafanya uchunguzi kuhusu tukio linalomhusisha mtoto wa miaka 10, mwanafunzi wa darasa la tano, anayedaiwa kuiba gari la mwalimu akiwa na wenzake.

Inadaiwa kuwa mtoto huyo alikuwa na wenzake wanne, ambapo kwa pamoja walipanga kuiba gari aina ya Toyota Spacio, mali ya Zuhura Khatibu (47), mkazi wa Kilakala, Manispaa ya Morogoro.

Tukio hilo limetokea jana, Mei 26, 2025, katika eneo la Shule ya Msingi Kigurunyembe iliyopo ndani ya Manispaa ya Morogoro, wakati mmiliki wa gari hilo akiwa darasani.

Alipotafutwa na Mwananchi leo, Mei 27, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Alex Mkama, amesema jeshi hilo linafanya uchunguzi na taarifa itatolewa.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo, akiwa na wenzake ambao bado wanatafutwa, walitumia funguo bandia kuendesha gari hilo. Taarifa kamili itatolewa baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika,” amesema Mkama.

Baadhi ya mashuhuda, akiwepo Paul Boniface, wamesema mtoto huyo alikamatwa baada ya kugongana na bodaboda eneo la Kigurunyembe akiwa anaendesha gari hilo. Baada ya kugongana alikimbia.

“Huyu mtoto baada ya kugongana alikimbia, ndipo wananchi walimkimbiza na kufanikiwa kumkamata akiwa amejificha kwenye shimo.

“Baada ya kugundua kuwa ameshtukiwa, ikabidi ashuke kwenye gari na kukimbia kuelekea kwenye shule ya chekechea, ndipo watu wakaanza kumkimbiza na kumkuta kwenye shimo amejificha,” amesema.

Amesema baada ya kumkamata, mtoto huyo alipelekwa barabarani na kuanza kuhojiwa huku akipigwa na wananchi wenye hasira, ndipo alipojitetea kuwa alitumwa kulichukua gari hilo na kulipeleka Msamvu.

Shuhuda mwingine, Godfrey Paskali, amesema inavyosemekana mtoto huyo alifika eneo la tukio akiwa na watu wanne na walifanikiwa kuchukua pesa ambazo zilikuwepo kwenye gari zaidi ya Sh 200,000 pamoja na vitenge.

“Baada ya wenzake kuondoka na vitu hivyo, ikabidi mtoto huyo atoke na gari hilo,” amesema.

Hata hivyo, mtoto huyo alisikika akisema kuwa aliambiwa na kijana mmoja achukue gari hilo, kwani anaweza kuliendesha.

“Aliniambia, ‘Jipe imani, unaweza kuliendesha gari hilo, mdogo wangu’,” amesema.

Related Posts