Rais Samia amteua Badru bosi mpya Ngorongoro, Dk Doriye aliwa kichwa

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wawili akiwemo Abdul-Razak Badru aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Uhifadhi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), akichukua nafasi ya Dk Elirehema Doriye ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Badru anachukua nafasi hiyo baada ya kuhudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) tangu alipoteuliwa Februari 6 mwaka jana. Kabla ya kuteuliwa kuongoza mfuko huo, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Kuteuliwa kwa Badru kuiongoza NCAA, kunaendelea kutengeneza panda shuka za Dk Doriye ambazo amekuwa akikutana nazo tangu aanze kuhudumu kama mteuliwa ndani ya Serikali.

Kwa mara ya kwanza Julai 29, 2019 Dk Doriye aliukwaa uteuzi baada ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli kumpa nafasi ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Aliteuliwa kushika nafasi hiyo akitokea Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) alipokuwa akifanya kazi kama mhadhiri.

Baada ya kudumu katika nafasi hiyo kwa siku 1,562 hadi Novemba 7, 2023, Rais Samia alimteua Kaimu Abdi Mkeyenge kuchukua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa NIC ambaye awali alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)

Baada ya Dk Doriye kuahidiwa kuwa atapangiwa kazi nyingine, hatimaye Mei 7 , 2024 alirudishwa katika mfumo kwa kuteuliwa kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ambapo amehudumu kwa siku 384 pekee.

Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo Mei 26, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu pia imeeleza kuwa Rais amteua Dk Rhimo Nyansaho kuchukua nafasi ya Badru PSSSF. 

Kabla ya uteuzi huo, Dk Nyansaho alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania.

Related Posts