Dar es Salaam. Zaidi ya wagonjwa 200 wanaohitaji huduma ya kuchuja damu ‘dialysis’ na watoto wanaopokea huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana walipitia wakati mgumu baada ya jengo wanalolitumia kupata huduma hizo kukosa umeme kwa saa 18.
Wagonjwa hao wanaopokea huduma katika jengo la watoto kwa zamu ndani ya hospitali hiyo, walijikuta wakirundikana baada ya huduma hiyo kusimama kwa tangu saa 3 usiku wa kuamkia jana.
Matibabu ya dialysis yanajumuisha mashine zinazotumia umeme kuchuja damu kutoka kwenye figo kwa lengo la kutoa sumu, taka na maji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana asubuhi, wagonjwa hao walisema umeme huo ulikatika saa tatu usiku juzi, kabla ya kuwashwa jenereta ambalo nalo liliharibika baada ya muda mfupi.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MNH, Aminiel Aligaesha alikiri kutokea kwa hitilafu hiyo na kueleza hatua zilizochukuliwa.
Wagonjwa hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao kwa sababu za kiusalama, walisema hali hiyo ilisababisha baadhi yao kuanza kupata athari hasi kwa kuvimba miguu, matumbo na kutapika.
“Jengo lote umeme ulikatika jana usiku saa tatu, jenereta likawashwa nalo linakazima, wanasema ni bovu, wameleta mafundi wanatengeneza lakini watu wa Tanesco hawajafika mpaka sasa hatuna matibabu, hata wagonjwa waliokuwa ICU wamehamishiwa kwenye majengo mengine,” alisema mmoja wa wagonjwa hao.
Alisema hakuna matibabu yanayoendelea kwa wakati anazungumza na Mwananchi.
“Wagonjwa wa figo tuko nje tumekaa tu, viongozi wanapita wanatuambia kama unajisikia hauko vibaya sana unaweza kwenda kupumzika nyumbani.”
Saa 5:10 asubuhi mgonjwa mwingine alisema eneo lote la jengo la watoto lilikuwa halina huduma zilizokuwa zinaendelea akifafanua kuwa alifika hospitalini hapo tangu juzi lakini alikuwa bado hajapata huduma.
“Watu wamezidiwa, wengine wapo hoi kabisa na hatujui chochote kinachoendelea, ratiba yangu ilibidi niwe nimepata matibabu shift ya saa 4 usiku, lakini mpaka sasa nimenasa hapa sijapata matibabu.
“Kiukweli kadri masaa yanavyosogea wagonjwa wanaanza kuchoka, sisi figo zote zimekufa tunategemea hizi mashine, wengine wameshazidiwa matumbo yamejaa, miguu imevimba, wengine wanatapika, watoto huko juu wako hoi baadhi wamehamishiwa wodi zingine,” alisema mgonjwa huyo.
Mkazi wa Tegeta ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema mtoto wake amelazwa katika moja ya wodi na wamepambana na giza usiku kutokana na kukosekana kwa umeme.
“Wenzetu wenye hali mbaya watoto wao wamehamishwa, wamepelekwa wodi zingine hasa wale ambao walikuwa wanatumia oksijeni na waliokuwa ICU, sasa tunapambana na joto maana hakuna umeme, usiporudi tutalala tena gizani,” alisema mama huyo.
Aligaesha alisema; “usiku wa kuamkia Mei 26 (jana), 2025 majira ya saa tano usiku, kulijitokeza changamoto ya umeme katika jengo la watoto baada ya njia mbili za umeme kutoka na kusababisha kuwepo na hitilafu kwenye transfoma na kuathiri pia jenereta ya dharura ya jengo hili.”
Alisema kilichotokea ni kuwa jengo hilo lina ‘phase’ tatu za umeme, mbili zilitoka, ikabaki moja ambayo baadaye nayo ilitoka.
Alisema walitoa taarifa Tanesco nao wakafika kwa wakati wakajaribu kutafuta chanzo cha hitilaf, wakafanikiwa kurudisha umeme usiku huo.
Hata hivyo, alisema umeme ulikatika tena baada ya muda mfupi na jenereta linalolisha jengo hilo nalo lilipata hitilafu, halikuweza kuwaka.
“Kwa hiyo tunachokifanya sasa toka jana saa sita usiku wa kuamkia leo, Tanesco wako Muhimbili hawajalala, na mafundi pia wapo. Tumemwita mmiliki wa jenereta hili naye hajalala, wote wako hapa, wanajaribu kuangalia tatizo ni nini kwa pamoja,” alisema.
Alisema kwa wananchi wanaopata huduma katika jengo hilo, wale ambao huduma zao zinategemea umeme kwa kiasi kikubwa, walihamishiwa kwenye wodi zingine.
“Tuna wagonjwa wanaohitaji huduma za ICU, tunayo ya watoto kwenye jengo hilo, ambao tumewasambaza katika ICU zingine ili waendelee kupata huduma. Kulikuwa na watoto wa maeneo mengine, wengine wako kitengo cha dharura sehemu ya watoto na wengine tumewapeleka jengo la wazazi,” alisema.
Kuhusu hatima ya wagonjwa wa dialysis, Aligaesha alisema tayari hospitali imechukua hatua za haraka kuwasiliana na hospitali zingine za karibu.
“Tunawasiliana na hospitali jirani ili waendelee kusafishwa figo, sisi tuna wagonjwa wengi kwa siku. Jitihada ziko palepale kuhakikisha tunarejesha umeme na huduma kwa wagonjwa wetu,” alisema.
Alipotafutwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ilala, Regina Mvungi alisema mafundi walikuwa wanaendelea na matengenezo tangu juzi usiku.
“Tulipeleka mafundi tangu jana (juzi) usiku, mpaka sasa bado wanaendelea na matengenezo, kama kungekuwa na changamoto kubwa zaidi ningetaarifiwa, nadhani muda si mrefu watamalizia,” alisema.
Hata hivyo, ilipofika saa 7:00 mchana jana, wagonjwa wa dialysis kutoka hospitalini hapo walianza kuhamishiwa katika hospitali zingine za karibu ili kupata huduma.
Miongoni mwa wagonjwa tuliowasiliana nao, walisema wamepelekwa Hospitali ya Hindu Mandal, Regency, Alsifa na wengine Mloganzila.
Ilipofika saa 10:10 jioni jana, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilifanikiwa kurejesha umeme katika jengo hilo, baada ya matengenezo yaliyochukua takribani saa 18.
Kwa mujibu wa Aligaesha; “Umeme umerudi katika Jengo la Watoto dakika 10 zilizopita na tayari huduma zimerejea. Wagonjwa ambao walikuwa na uhitaji zaidi wa huduma tuliwahamishia katika majengo mengine na wa dialysis tuliwapeleka hospitali za karibu kupata huduma.”
Hali hiyo pia ilithibitishwa na Mvungi kuwa matengenezo yamefanyika na tayari umeme umerejea Muhimbili, akiongeza kuwa changamoto iliyosababisha hitilafu hiyo imekabidhiwa kwa Hospitali ya Muhimbili.