Mtama. Wananchi wa kata ya Nachunyu wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya baada ya Serikali kuwajengea kituo cha afya Pangaboi.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Kituo cha afya Pangaboi leo Jumanne Mei 27, 2025 Kaimu Mganga Mkuu wa kituo hicho, Dk Tasilo Lupapa amesema kitakapokamilika kitahudumia wakazi zaidi ya 6,000 ambapo wananchi hao walikuwa wanapata adha kubwa ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.
Dk Lupapa ameendelea kusema kuwa kituo hicho cha afya hadi kumalizika kwake kitagharimu zaidi ya Sh600 milioni ambapo mpaka sasa wameshatumia Sh500 milioni na kuiomba Serikali kuwaongezea fedha ili kukimalizia.
“Naiomba Serikali itusaidie kutuongezea fedha ili kuukamilisha mradi kwa wakati, pia itutengenezee barabara kwani iliyopo imechangia kwa kiasi kikubwa kutomalizika mradi kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amesema kuwa changamoto kubwa katika kata ya Nachunyu ilikuwa kukosekana kwa huduma ya afya na ubovu wa barabara.
“Kata ya Nachunyu inazalisha korosho kwa wingi ,changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa kituo cha afya na barabara, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kutomalizika kwa kituo cha afya kwa wakati lakini ninamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea kituo hiki cha Pangaboi,”amesema Nnauye.
Aidha mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa, Ismail Ally Ussi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kituo hicho cha afya, ameishukuru Serikali kwa hatua waliyoifanya ya kupunguza changamoto ya upatikanaji huduma za afya huku akiwataka wananchi kulinda miundombinu iliyowekwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
“Nawapongeza sana viongozi kwa usimamizi mzuri wa mradi huu lakini niwaombe wananchi kutunza miundombinu hii”amesema Ismail Ally Ussi.

Sada Shabani mkazi wa Nachunyu ameishukuru Serikali kwa kuwaletea huduma ya afya, kwani mwanzoni walikuwa wanapata shida kwenda mbali.
“Tulikuwa tunatembea zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma ya afya lakini sasa hivi tuna furaha kubwa kwani tumesogezewa karibu, pia tunamshukuru mbunge wetu kwa jitihada alizofanya,” amedai Sada.
Kituo hicho cha afya Pangaboi kitahudumia na vijiji jirani.