Dar es Salaam. Benki ya TCB imeandika historia mpya baada ya kutangaza kupata faida ya Sh48 bilioni kabla ya kodi kwa mwaka 2024, mafanikio makubwa zaidi kuwahi kufikiwa na benki hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza Mei 26, 2025, katika mkutano mkuu wa 33 wa wanahisa uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo amesema mafanikio hayo yanatokana na ukuaji mkubwa wa mali za benki hiyo kwa asilimia 25, uwiano mzuri wa mikopo, pamoja na usimamizi makini wa matumizi ya fedha.
“Kwa kweli mali za benki yetu zimekua kwa asilimia 25, ukuaji ambao ni wa juu ukilinganisha na wastani wa ukuaji wa sekta ya benki nchini,” amesema Mihayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi, mikopo iliyotolewa na benki hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 huku mapato ya riba na yasiyo ya riba yakiongezeka maradufu, hatua inayothibitisha kuimarika kwa uaminifu wa wateja kwa taasisi hiyo ya kifedha.
“Ukwasi wetu umefikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka 16 iliyopita, ikimaanisha kuwa wateja wetu wanaendelea kutuamini kama sehemu sahihi ya kutimiza ndoto zao,” ameongeza.
Katika kikao hicho, TCB ilitangaza rasmi kutoa gawio kwa wanahisa wake, jambo lililopokelewa kwa shangwe na furaha, hasa ikizingatiwa kuwa mwaka uliopita benki hiyo ilikumbwa na hasara ya Sh48 bilioni.
“Kikao kimeiridhia kutoa gawio kutokana na faida tuliyopata mwaka jana. Hili ni jambo la kihistoria kwani miaka ya nyuma tulipata hasara, lakini sasa tumefanya mabadiliko makubwa,” ameeleza mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa uongozi, hasara ya mwaka 2023 ilitokana na mabadiliko ya kiutendaji na changamoto za mfumo wa kifedha kufuatia muunganiko wa baadhi ya benki. Hata hivyo, hatua zilizochukuliwa zimeiwezesha benki hiyo kusimama tena kwa nguvu mpya.
“Kwa niaba ya bodi ya wakurugenzi na menejimenti, nawahakikishia kuwa TCB itaendelea kuwa chombo cha kuaminika katika kukuza ujumuishi wa kifedha na kuchochea maendeleo ya taifa letu,” amesema Mihayo.
TCB imeeleza kuwa inaendelea kujiimarisha kama benki kinara kwa siku zijazo, huku ikieleza dhamira yake ya kutumia fursa zilizopo sokoni, kukabiliana na changamoto, na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Martin Kilimba ameahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuwekeza katika ubunifu na teknolojia ya kisasa ili kuboresha ufanisi wa kazi na kuongeza thamani kwa wanahisa wake, ikiwa ni sehemu ya malengo yake ya kimkakati kwa mwaka huu wa fedha.
Ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana mwaka uliopita ni ushahidi wa jitihada za pamoja na dhamira ya dhati ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taasisi hiyo.
“Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, tumeweza kufanikisha mengi mwaka uliopita. Mkutano huu ni fursa ya kutafakari utendaji wetu, mafanikio yaliyopatikana na kupanga mikakati ya siku zijazo,” amesema.
Amesema uwasilishaji wa takwimu za kifedha kwa mwaka uliopita zimeonesha mwenendo mzuri wa benki hiyo ipo katika njia sahihi kuelekea mafanikio makubwa zaidi.
“Utendaji wetu wa mwaka jana unaakisi dhamira yetu ya wazi katika kupanga mikakati inayolenga ukuaji, ubunifu na kukidhi mahitaji ya mteja,” taarifa hiyo imeeleza.
Kwa mujibu wa Kilimba, uwekezaji katika teknolojia ya kidijitali umeimarisha utendaji, kuendana na kasi ya mabadiliko ya sekta ya fedha duniani na kuweka TCB katika nafasi nzuri ya ushindani.
Aidha, benki imesisitiza kuwa itaendelea kuweka kipaumbele katika kusikiliza mahitaji ya wateja, kuhakikisha huduma bora na suluhisho za kifedha zinazolenga kuinua maisha ya Watanzania.
Katika mikakati ya mwaka huu, TCB imepanga kuongeza ufanisi, kufanya uhakiki wa hasara, kusimamia kwa makini rasilimali watu, na kuimarisha mizania ya taasisi ili kuhakikisha ukuaji endelevu na mafanikio kwa wanahisa wake.