Wabunge wataka mkono wa sheria kwa wasanii wenye mavazi ya aibu

Dodoma. Wabunge wameishinikiza Serikali kuweka msimamo thabiti katika kuwalinda watoto na kizazi cha sasa, wakieleza kuwa maadili yameendelea kuporomoka kwa kiwango cha kutisha.

Baadhi yao wamependekeza kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya wale wanaobainika kufanya vitendo viovu vinavyoharibu maadili ya jamii.

Kauli za wabunge zilitolewa wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka 2025/26.

Waziri wa Wizara hiyo Dk Doroth Gwajima aliwasilisha hotuba hiyo leo Jumanne Mei 27,2025 akiliomba Bunge kupitisha Sh76.05 bilioni na ambazo zimepewa vipaumbele vitano.

Mbunge wa kuteuliwa Profesa Shkrani Manya amesema maadili kwa Watanzania yameporomoka kwa kiasi kikubwa ndiyo maana wanaume wanawatelekeza watoto wao.

Profesa Manya amesema katika maeneo mengi nchini kumeshuhudiwa watu wakizitelekeza familia zao hasa watoto waliowazaa na ndipo inaibukia wimbi la watoto wa mitaani,  lakini akaitaka Serikali kutafuta namna bora ya kupeleka elimu kwa watu.

“Kimsingi hakuna mimba za mitaani na hivyo hakuna watoto wa mitaani lakini tukubaliane kwamba kuna mahali maadili yamesahaulika au uwajibikaji umekuwa mdogo, kuzaa mtoto na kumtelekeza ni dhambi kubwa sana,” amesema Profesa Manya.

Hata hivyo Manya amezungumzia suala la kujiimarisha kimwili akiitaka Serikali iendelee kutoa elimu ili watu waache kutumia vyakula ambavyo havifai na badala yake warudi kwenye vya asili,  ikiwemo mbegu za maboga.

Mbunge wa Viti Maalumu,  Munde Tambwe amelalamikia taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kwamba yamekuwa kichaka cha kujificha na kuwatapeli watu kwa mgongo wa imani za kidini, jambo alilosema halikubaliki.

Munde amedai ndani ya Taifa kuna Asasi ambazo zinajulikana zinaendelea kufundisha mmomonyoko wa maadili na mambo yasiyofaa kwa watoto, lakini ni kama Serikali imefumba macho haiwachukulii hatua zinazostahili wahusika wote.

Munde amesema kuna asasi hazijihusishi kabisa na mambo ya kijamii licha ya kuwa zimesajiliwa kwa ajili ya huduma za watu.

Pia alizungumzia ukatili wa kimtandao kwamba unaendelea kuitesa Tanzania lakini Serikali licha ya kuwa na uwezo bado imekuwa kimya .

Naye Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas (CCM) ameitaka Serikali kuondoa usiri na badala yake iwe inawatangaza hadharani watu wenye kesi za ubakaji na hata inapofika wamehukumiwa majina yao yaanikwe hadharani, ili wawe kwa alichokiita ‘blacklist’.

“Mashauri ya ukatili yanamalizwa nyumbani, hii siyo sawa kabisa, haya mambo yasiwe na mapatano bali wanaoyafanya waanze kutangazwa mapema wakati kesi zikiendelea na utakapofika mwisho basi wawe kwenye orodha, lakini kwenye vyombo vya maamuzi hebu watusaidie kasi zisichukue muda mrefu,” amesema Tarimba.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Teya Ntala amegusia suala la misuko kwa wanaume, uvaaji mavazi yasiyo na staha ikiwemo kwa wasanii lakini akasema inashangaza kuona Serikali ikiendelea kuwashangilia.

Dk Ntala ametaka sheria ya ndoa ya mwaka 1992 kwamba imekuwa tatizo badala ya suluhisho hasa watu wanapojificha kwenye kivuli cha balehe.

“Lakini yote kwa yote, naona hawa Polisi wapo hapa, nataka kuhoji ni kwa nini isije sheria tuipitishe humu ili mtu akibainika kwa kosa la ubakaji adhabu yake ahasiwe kabisa.

“Nawaomba Polisi mshughulike na wanaume wa aina hiyo, hakikisheni mnamwachia sehemu ndogo kwa ajili ya kupatia haja ndogo tu,” amesema Dk Ntala.

Kuhusu ukatili wa ubakaji amesema ni tishio huku akitaja Sheria ya ndoa ya mwaka 1972 kwamba inatumika kuwakandamiza watoto wa kike.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kukua kwa mtoto siyo hedhi tunaangalia masuala ya kimaumbile, kupanuka kwa mwili ikiwemo nyonga zake, sauti kuwa nyororo, nywele kuota sehemu mbalimbali za mwili wake, hapo ndipo unaweza kusema huyu kakua lakini siyo hedhi,” amesema Dk Ntala.

Mbali na hizo amezungumzia mavazi akisema watu wanatia aibu kwa kuvaa mavazi yasiyo na staha akitolea mfano kwa wasanii, ambao wanavaa mavazi ya ajabu na wengine kusuka nywele kama watoto wa kike.

Katika mchango wake Mbunge wa Viti Maalumu, Tauhida Gallos amezungumzia suala la michango hasa inapotokea mambo ya misiba ambayo watu huchangisha kupitia mitandao ya simu, akisema ni utapeli mwingine unaopaswa kushughulikiwa.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko amesema wengi wanaochukua  mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu hawalipi, akaomba itungwe sheria ili watakaofanya hivyo washtakiwe kwa makosa ya jinai.

Matiko pia aliunga mkono hoja ya wabunge wengine kwamba suala la ubakaji bado ni janga na lisipofanyiwa kazi litaleta madhara makubwa kwenye mmomonyoko wa maadili.

Ametolea mfano wa matukio ya hivi karibuni kwamba kuna wanawake wawili walibakwa katika Wilaya ya Tarime hata wakasababisha kifo cha mmoja wao, lakini wakati yanafanyika haya jamii na Serikali wapo wakiyashuhudia.

Matiko pia aligusia suala la kutoa mimba ambapo amesema Tanzania hakuna ruksa ya kufanya hivyo,  labda iwe kwa ushauri wa madaktari.

Related Posts