Wanafunzi wanaojifungua na kurudi shuleni hawasababishi ongezeko la mimba – Utafiti

Dodoma. Serikali imesema kuwa utafiti uliofanywa kuhusu kuwarudisha wanafunzi waliopata mimba shuleni kuendelea na masomo haujaonyesha ongezeko la wanafunzi kupata mimba katika shule husika, badala yake umepunguza.

Mpaka sasa jumla ya wanafunzi 10,300 waliopata mimba shuleni wamerudi kuendelea na masomo yao katika shule walizokuwa wanasoma awali na wengine kuhama shule, baada ya kujifungua.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.

Profesa Mkenda amesema Serikali iliruhusu wanafunzi wanaopata mimba shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua ili waweze kutimiza ndoto zao kwa kuwa elimu ni maisha, hivyo kuwanyima fursa hiyo ni sawa na kuwanyima maisha.

Amesema  kuwa watoto wa kike waliopata ujauzito hawapaswi kunyimwa haki ya kuendelea na masomo kwa kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto.

Profesa Mkenda amesema  kupata ujauzito si mwisho wa ndoto za mtoto wa kike wanapaswa kuwawezesha kurejea shuleni na kuendelea na masomo yao.

Amesema jambo hili linafanyika kwa kufuata waraka maalumu wa kamishna wa elimu, ambao unatoa namna ya mwanafunzi kurudi kuendelea na masomo kwa kujali masilahi ya mtoto aliyezaliwa.

Profesa Mkenda pia amesema zipo changamoto mbalimbali katika kutekeleza suala hilo ikiwemo, baadhi ya wazazi pamoja na walimu kupinga wakiamini kuwa litachangia wanafunzi wengine pia kupata ujauzito.

Amesema  Serikali imefanya uchunguzi wa kutosha na kubaini kuwa jambo hili halichangii wanafunzi wengine kupata ujauzito kama inavyoaminiwa na baadhi ya wazazi na walimu hao.

“Tumefanya utafiti katika jambo hilo na tumebaini kuwa halichangii wanafunzi wengine kupata ujauzito katika shule hizo na ndiyo maana mpaka sasa tuna wanafunzi 10,300 ambao walipata mimba mashuleni, lakini baada ya kujifungua wamerudi kuendelea na masomo yao.

Akizungumzia suala la utoro, Profesa Mkenda amesema bado ni changamoto kubwa nchini, hivyo Serikali imejipanga kumpa kila mwanafunzi namba yake ya utambulisho ya kipekee ili kila anapokwenda atambuliwe kutokana na namba hiyo.

Amesema namba hiyo itawawezesha kujua idadi ya wanafunzi walioko shuleni na wale ambao wameacha shule na namna ya kuwafuatilia hata kama watakuwa wamehamia kusoma nje ya nchi.

Aidha amesema mpaka sasa mkoa unaoongoza kwa utoro ni Geita ambapo idadi kubwa ya wanafunzi watoro ni wa kiume na siyo wa kike.

Kuhusu changamoto za mikopo ya elimu ya juu, Profesa Mkenda  amesema pamoja na Serikali kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh464 bilioni mwaka 2021 hadi Sh787 bilioni kwa sasa,  wanafunzi wengi wenye sifa wanaokosa mikopo hawajui namna ya kuiomba.

 “Kama wewe umefiwa na mzazi unatakiwa kuambatanisha cheti cha kifo kwa sababu bila ya kufanya hivyo hawatajua ukweli kuwa wewe huna wazazi, sasa wengi hawafanyi hivyo… lakini kwa sasa kuna namba ya kupiga kama mwanafunzi atakosa mkopo ambapo atajulishwa mahali alipokosea na kuna baadhi ya watu wamepata mkopo baada ya kurekebisha makosa yao,” amesema Profesa Mkenda.

Aidha amesema watoto wa watu wenye uwezo kuomba mikopo ya elimu ya juu ni kitendo cha wizi kwa sababu kuna ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia ada ndiyo wanaotakiwa kupata mikopo na si kwa watu wenye uwezo.

Mmoja wa wadau wa kutetea wasichana dhidi ya mimba za utotoni, Veronica Chaki amesema pamoja na Serikali kutoa fursa ya wanafunzi waliopata mimba shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua, lakini wazazi wamekuwa kikwazo katika kufanikisha hilo.

Amesema wazazi wanapoona watoto wao wamepata mimba huwakimbiza na kwenda kuwaficha mbali ili kuficha aibu ya familia, bila kujua kwa kufanya hivyo kunamkosesha msichana huyo haki yake ya kupata elimu.

Related Posts