Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imetoa taarifa kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2024, fedha zinazotumwa na diaspora kuja Tanzania zimefikia Sh2.11 trilioni.
Takwimu hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, leo Machi 28, 2025 wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka 2025/26 ambayo wizara imeomba Sh340.5 bilioni zitakazotumika katika maeneo makuu manne.
Kati ya fedha hizo, Sh294.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, zinazojumuisha Sh273.66 bilioni za matumizi mengineyo na Sh21.3 bilioni kwa ajili ya mishahara ya watumishi waliopo makao makuu ya wizara na Balozi za Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati akiwapokea mabalozi bungeni leo Machi 28, 2025.
Hata hivyo, asilimia 70 ya bajeti hiyo imetajwa kuwa itatumika kwa ajili ya shughuli za mabalozi ambazo zinakadiriwa kufikia Sh23.8 bilioni.
Maeneo ambayo yamepangwa kutumia fedha hizo ni pamoja na kuendelea kuvutia na kutoa huduma za mikutano zinazokidhi viwango vya kimataifa, ili kukuza jina la Tanzania katika sekta ya utalii wa mikutano duniani.
Nyingine ni kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia diplomasia ya uchumi, kuboresha mbinu za masoko, kuongeza idadi ya mikutano na shughuli zinazoingizia kituo mapato na kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya kimataifa katika kufikia malengo yake.
Akizungumzia suala la diaspora, Waziri Kombo amesema wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika sekta mbalimbali, ikiwamo kwenye miradi ya maendeleo na mwaka 2024 diaspora waliwekeza Sh7.5 bilioni ikilinganishwa na Sh6.4 bilioni walizowekeza mwaka 2023 katika Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja wa UTT-AMIS.
“Hatua hii inachangia ukuaji wa sekta ya fedha na uwekezaji wa ndani, lakini vilevile Watanzania waishio nje ya nchi wamekuwa wakinunua nyumba na viwanja kupitia Shirika la Nyumba la Taifa na sekta binafsi, hivyo kuchangia maendeleo ya sekta ya milki na kuchangia upatikanaji wa makazi bora,” amesema Waziri Kombo.
Kwa mujibu wa waziri huyo, uwekezaji huo umeongezeka kutoka Sh7.5 bilioni 2023 hadi kufikia Sh9.2 bilioni katika mwaka mwaka 2024.
Kuhusu mafanikio, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetaja ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano wa uwili hususan kutokana na kusainiwa na utekelezaji wa mikataba na hati za makubaliano na upatikanaji wa rasilimali fedha, ujuzi na teknolojia kutoka nchi rafiki.
Mengine ni kunufaika na ushirikiano wa kikanda hususan kupitia utekelezaji wa mikataba na itifaki zake na programu za mtangamano wa kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa kutokana na ushiriki wa Tanzania katika masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na nishati safi ya kupikia kwa kinamama.
Kuhusu changamoto, amezitaja kuwa ni kwa baadhi ya nchi wanachama katika Jumuiya za Kikanda kutoheshimu baadhi ya mikataba na makubaliano, ikiwamo kutolipa michango yao ya kibajeti kwa wakati.
“Hatua hii inaathiri uratibu na ushiriki wetu katika utekelezaji wa programu za mtangamano wa kikanda ambapo hivi sasa, majadiliano yanaendelea kwa upande wa EAC na SADC, huku baadhi ya wadau ikiwemo sekta binafsi kutochangamkia ipasavyo fursa zitokanazo na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kupitia ushirikiano wa uwili,” amesema.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dk Issac Njenga akiwashukuru wabunge waliokuwa wakimshangilia baada ya kutambulishwa kuwa ni miongoni mwa mabalozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa waliokuwemo ukumbini wa Bunge jijini Dodoma leo Mei 28, 2025.
Akizungumzia ukarabati wa majengo hoja ambayo iliibuliwa na wabunge, waziri huyo amesema kuna mpango wa kufanya ushirikiano na sekta binafsi.
Katika michango ya wabunge, wamesema diplomasia ya uchumi kwa Tanzania imezidi kushuka, huku wakiomba juhudi ziongezwe.
Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi ameelezea upungufu huo huku akiwatupia lawama mabalozi wa Tanzania kuwa wameshindwa kutimiza wajibu wao na kutaka waanze kupewa vipimo vya kiutendaji kazi, huenda wanajisahau.
Mkundi pia amezungumzia uchakavu wa majengo ya Balozi nyingi za Tanzania kwamba yanahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa. “Majengo mengi yamechakaa kiasi ambacho hayavutii tena,” amesema.
Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega amesema hadhi ya Tanzania inaporomoka kwa sababu ya kuacha majengo 105 bila kufanyiwa ukarabati.
Wabunge pia wametaka majengo ya Balozi za Tanzania yawekwe mabango ya matangazo kuhusiana na mashindano ya Afcon 2027.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Cosato Chumi amekiri kuwa mpango wa kuwapa vipimo vya kiutendaji mabalozi unaweza kusaidia kwa kuwa utawakumbusha wajibu wao.
Chumi pia amekubali uwekaji wa mabango ya matangazo ya nchi kwa nchi kuwa utasaidia pia kuikuza na kuitangaza Tanzania kabla na hata baada ya mashindano ya Afcon kumalizika.
Akisoma maoni ya kamati, Balozi Liberata Mulamula amesema mipango mingi inakwama kutokana fedha kutolewa kwa kiwango kidogo.
Mulamula ambaye ni waziri wa zamani wa wizara hiyo, amesema hali hiyo ndio imesababisha kushindwa kukamilisha ujenzi wa kumbi za mikutano katika kituo cha Dk Salim Ahmed Salim.