Mabalozi wakubali kuwekeza Dodoma wakieleza ardhi inafaa

Dodoma. Serikali imewaita mabalozi kutambua umuhimu wa kuwekeza katika Jiji la Dodoma, kwani ndiyo eneo pekee linalowafaa kwa sasa.

Wito huo umetolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo alipokuwa akizungumza na mabalozi kwenye hafla na ziara iliyopewa jina la ‘Diplomatic Capital City Tour’.

Balozi Kombo amesema jambo jema la uwekezaji kwa sasa ni kuelekeza nguvu katika Mkoa wa Dodoma ambao umekuwa na vigezo vyote muhimu na vinavyojitosheleza kuvutia wageni ikiwemo ardhi ya kutosha kwa ajili ya biashara na uwekezaji.

Mabalozi hao wapo Dodoma kwa mwaliko wa wizara hiyo ambayo leo Jumatano Mei 28, 2028 ndiyo wamewasilisha Bajeti yao kwa mwaka wa fedha 2025.

“Dodoma kuna fursa za biashara na uwekezaji, ipo ardhi ya kutosha yenye maji au uwezo wa kuchimba visima, utalii, mahoteli na uhitaji wake ni mkubwa,” amesema Waziri Kombo.

Kwa mujibu wa Balozi Kombo, maeneo yanayoonekana kuwa mbali na mji muda si mrefu hayataonekana hivyo kwani ujenzi wa makazi umekuwa ukienda kwa kasi ikiwemo ujenzi wa mahoteli makubwa akaomba mabalozi kuanza kuchangamkia kwa haraka.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema maeneo ya uwekezaji kwa Mkoa wa Dodoma yametengwa kimkakati ikiwemo maeneo maalumu ya ujenzi wa ofisi ya mabalozi.

Senyamule amesema ipo miradi mikubwa inayotekelezwa kimkakati ambayo inaufanya kuwa na hadhi ya makao makuu ya nchi na kuwa chachu ya kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Mkuu huyo ameeleza namna mkoa ulivyofunguka kwenye masuala ya usafiri wa ardhini na anga, hivyo hakuna sababu ya kuchelewa kuwa na makazi Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wengine, Balozi wa China nchini Dk Lu Youqing, amesema nchi yake inaunga mkono maendeleo ya Tanzania na kwamba atashawishi makampuni ya nchini mwake kutembelea Dodoma na kuleta shughuli zao za kibiashara kwa kuwa amebaini panafaa kwa shughuli za kibiashara.

Dk Youging amewataka mabalozi wengine kupeleka ujumbe katika nchi zao kuhusu Ardhi ya Dodoma ili uwekezaji wa hapo uwe mkubwa na kufanya mkoa uchangamke kwa haraka.

Sanjari na hafla hiyo fupi mabalozi hao walipata fursa ya kutembelea miradi ya kimkakati kwa kuanzia huduma za afya ambapo walitembelea Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Mji wa Serikali Mtumba na mwisho walitembelea mradi wa Uwanja wa Ndege Msalato katika safari waliyoita Diplomatic Capital City Tour.

Related Posts