Madakari bingwa 49 watua Mbeya

Mbeya. Serikali mkoani Mbeya imepokea kambi ya madaktari bingwa bobezi 49 kwa ajili ya   kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa wananchi katika halmashauri saba.

Ujio wa madaktari hao umetajwa kuleta suluhisho kwa wananchi wenye changamoto za magonjwa ukiwepo mfumo wa njia ya mkojo.

Kambi hiyo imepokewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera leo Jumatano Mei 28, 2025 na kwamba itadumu kwa muda wa siku sita

Awali   Dk, Homera amewataka wataalamu wa afya na madaktari bingwa bobezi kuangalia namna bora ya kutatua changamoto ya tatibabu ya mfumo wa njia ya mkojo kwa wanaume.

“Kuna changamoto kubwa ya tatizo la mfumo wa njia ya mkojo kwa wanaume walio wengi,niwaombe licha ya kutafuta suluhisho mtoe elimu ya kukabiliana na tatizo hilo,” amesema.

Amesema elimu ya kutosha ikitolewa kuhusiana na visababishi vya tatizo la hilo jamii hitajua njia mbadala ya kukabiliana nayo.

Dk Homera amesema kambi  hiyo ya madaktari bobezi itatoa huduma kwa magonjwa ya watoto na watoto wachanga, upasuaji wa mfumo wa njia ya  mkojo, magonjwa ya ndani, ganzi, kinywa na meno, pua sambamba na mifumo ya koo na masikio.

“Nitoe rai kwa wananchi katika halmashauri saba za Mkoa wa Mbeya kutumia fursa ya kambi ya siku sita kufika katika hospitali  za wilaya ambazo zinatoa huduma,”amesema.

 Amesema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kuja na kampeni hiyo ni kuboresha afya za Watanzania ambapo kila halmashauri itapokea madaktari bingwa sita na muuguzi mmoja,”amesema.

Mratibu wa kambi ya madaktari bingwa bobezi, Dk Destelia Nanyanga amesema pamoja na kutoa huduma kwa wananchi wamelenga kuwajengea uwezo madaktari wa hospitali za wilaya katika halmashauri saba.

“Lengo la kuwajengea uwezo ni kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi pia watumie fursa ya uwepo wetu kufika kupata huduma za kiuchunguzi kwa magonjwa mbalimbali,”amesema.

Dk Nanyanga amesema wamepokea ombi la Mkuu wa Mkoa kutoa elimu ya changamoto ya mfumo wa njia ya mkojo kwa wanaume jambo ambalo tutalipa kipaumbele.

“Hilo tutalifanya pia  tutafanya  utafiti wa hali ya changamoto ya mfumo wa  njia ya mkojo kwa wanaume Mkoa wa Mbeya na kutoa elimu ya viashiria vya  vinavyo changia tatizo hilo,” amesema.

Mkazi wa Kata ya Jakalanda, James Mwakyusa amesema ujio wa kambi hiyo utatatua changamoto ya magonjwa ya watoto ambayo hupelekea familia kukata tamaa kutokana na ukata.

“Unajua Serikali imeona mbali kuleta huduma za matibabu ya kibingwa kupitia kampeni hiyo, ukata ni kikwazo kikubwa cha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa jamii,” amesema.

Mwakyusa ameomba Serikali kuona namna ya  huduma hizo kufikishwa maeneo ya vijijini ili kuokoa vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika.

Related Posts