Majaliwa aendelea kuwashawishi Wajapan kuwekeza nchini

Tokyo. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameendelea kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Japan kuja kuwekeza nchini kwenye sekta za kilimo, afya, uchumi wa buluu, nishati, miundombinu, ufugaji na Tehama.

Ametoa rai hiyo kutokana na kile alichoeleza kuwa Serikali imeshaboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji.

Ameyasema hayo leo Jumatano, Mei 28, 2025 alipokutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu, Shirikisho la Wawekezaji na Wafanyabiashara nchini Japan (KEIDANREN) na Jumuiya ya Wamiliki, Marais na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Kampuni wa Japan (KEIZA DOYUKAI). Waziri Mkuu yupo Tokyo nchini Japan kwa ziara ya kikazi.

 “Tunakaribisha kampuni za Japan kuchangamkia fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania, zikiungwa mkono na mazingira tulivu ya biashara, mageuzi ya sera, na juhudi zinazoendelea za kupunguza urasimu.”

Jana, Mei 27, 2025, Majaliwa alikutana na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan (MLIT), Kenichi Ogasawara pamoja na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu Japan na Afrika (JAIDA), Miyamoto Yaichi

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za MLIT na kuhudhuriwa na marais wa makampuni makubwa ya uwekezaji ya Japan, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za nishati, miundombinu, utalii, kilimo na biashara.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Tanzania imejiimarisha katika kujenga uwezo wa rasilimali watu, hivyo aliwakaribisha katika kutoa mafunzo na programu za kubadilishana maarifa zitakazowezesha wahandisi wa Kitanzania, wapanga miji, na wataalamu wa miundombinu kunufaika na utaalamu na ubunifu mkubwa wa Japan.

Amesema Japan imeendelea kuwa mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na kwa kipindi cha miaka mingi, nchi hizo mbili zimejenga uhusiano thabiti, hasa katika eneo la miundombinu. “Tunathamini sana uhusiano huu na mchango mkubwa wa kampuni za Kijapani katika maendeleo ya Taifa letu.”

Majaliwa amesema Serikali inaamini kuwa miundombinu bora ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuboresha maisha ya watu, kuwezesha biashara, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda. “Lengo la Tanzania kuendelea kuboresha mtandao wa barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege”.

“Haya ni maeneo muhimu ya kuimarisha muunganiko wa ndani ya nchi na maeneo ya kikanda. Miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na upanuzi wa bandari za Dar es Salaam na Mtwara ni mifano thabiti ya dhamira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji wa kikanda.”

Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema kuwa ametumia vikao hivyo kuwaeleza wawekezaji na wafanyabiashara hao kuhusu mipango na mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inavutia zaidi uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Amesema kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambayo itaeleza kwa kiasi kikubwa itasaidia kubainisha maeneo muhimu ya uwekezaji ili yanayolenga kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNDP), Shigeki Komatsubara amesema kuwa Tanzania itaendelea kunufaika na utaalamu na teknolojia kutoka Japan katika sekta mbalimbali zikiwemo za miundombinu na rasilimali watu.

Related Posts