Ruangwa. Serikali ya Wilaya ya Ruangwa kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo wametoa majiko ya gesi 626, pamoja na majiko banifu katika kuendeleza nishati safi ya kupikia.
Akizungumza leo Jumatano Mei 28, 2025 baada ya kukabidhiwa jiko mkazi wa Ruangwa na mjasiriamali, Salome Akida amesema kuwa majiko hayo yanasaidia kuokoa muda pamoja na kupika kwa urahisi.
“Majiko ya gesi pamoja na banifu yanasaidia kupunguza muda wa kupika kuliko ya mkaa,” amesema Akida.
Juma Bakari ambaye amepata jiko banifu amesema kuwa jiko hilo linasaidia kupunguza muda wa kupika na hayaharibu mazingira.
“Rais anapambana na nishati safi, sisi wananchi wake lazima tumuunge mkono katika mapambano haya, na ndio maana Wilaya ya Ruangwa wametoa majiko ya gesi pamoja na majiko banifu ili kuweza kulinda misitu yetu pamoja na kutunza mazingira,” amesema Bakari.

Amesema nishati safi inasaidia kulinda afya ya mtumiaji, kwani utumiaji wa mkaa unaathiri afya na kuharibu mazingira.
Naye mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa, Ismail Ally Ussi amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Samia katika kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Tuendelee kushirikiana na Rais Samia katika kutumia nishati safi ili kutunza mazingira yetu kwa kuacha kukata miti hovyo, kwani ukataji huo unaharibu mazingira,” amesema Ussi.
Jumla ya miradi 17 yenye thamani ya Sh2 bilioni imekaguliwa, kuonwa na kuwekewa mawe ya msingi na mwenge wa uhuru katika Wilaya ya Ruangwa.