Simanjiro. Mashahidi wawili kwenye kesi ya rushwa inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Samwel Warioba Gunza wameanza kutoa ushahidi wao mahakamani.
Warioba anashtakiwa kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kutotimiza wajibu wa kisheria ambao ni kinyume cha sheria.
Akitoa ushahidi wake, Mei 28 mwaka 2025, mbele ya hakimu mkuu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uiso, ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brown Mwasomola amewasilisha vielelezo viwili vya kesi hiyo.
Mwasomola ameeleza kwamba kielelezo cha kwanza cha kesi hiyo ni barua ya maombi ya Elias Tipiliti ya kukusanya ushuru katika Soko la Mnada wa Orkesumet.
Kielelezo cha pili alichowasilisha ni barua ya Tipiliti kuteuliwa kukusanya ushuru kwenye Soko la Mnada wa Orkesumet.
Amesema vielelezo hivyo viwili vinaonyesha kuwa Tipiliti hakukidhi vigezo vya kupatiwa zabuni ya kukusanya ushuru huo kwani zabuni haikutangazwa hivyo kuwepo mazingira ya rushwa.
Shahidi wa pili, mhasibu wa halmashauri hiyo Edward Casmiry ameieleza mahakama hiyo kuwa alimshauri aliyekuwa mkurugenzi huyo Warioba kuwa asimpe zabuni ya kukusanya ushuru Tipiliti, kwenye Soko la Mnada wa Orkesumet.
Casmiry ameeleza kwamba alimshauri Warioba kuwa mzabuni huyo alipewa nafasi hiyo bila tenda kushindanishwa kama sheria, kanuni na taratibu zinapaswa kufuatwa za ombi la kukusanya ushuru.
Amesema alimshauri aliyekuwa mkurugenzi kuwa kitendo hicho kitasababisha wajibu hoja kwa wakaguzi kutokana na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za kuomba zabuni.

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Uiso ameahirisha hadi Juni 6 mwaka 2025 ambapo mashahidi wengine wa upande wa Jamhuri wataendelea kutoa ushahidi wao.
Hata hivyo, Warioba hakuwepo mahakamani hapo kwa sababu ni mgonjwa ila alifuatilia kesi hiyo kwenye kituo jumuishi mkoani Dodoma.
Warioba ana kesi mbili za rushwa kwenye mahakama hiyo ikiwemo ya matumizi binafsi ya Sh5 milioni, mali ya halmashauri ya Simanjiro iliyopo kwa Hakimu Onesmo Nicodemo