Mikakati Chadema kusuka safu Mbeya, Mwabukusi atoa msimamo

Mbeya. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisisitiza msimamo wao wa kutoshiriki uchaguzi kwa madai ya kutaka mabadiliko, huko mkoani Mbeya maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wa ndani katika majimbo mawili ya Mbeya Mjini na Uyole yameanza.

Hivi karibuni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza Jimbo la Mbeya Mjini kugawanywa kupata jipya la Uyole, ambapo tayari mbunge wa jimbo hilo na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameshatangaza nia ya kugombea Uyole.

Pia tume hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Ramadhan Kailima ilitangaza kuwa chama ambacho hakijasaini kanuni za maadili ya uchaguzi hakitaruhusiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu au uchaguzi wowote kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2030.

Hata hivyo katika vyama ambavyo vilisaini kanuni hizo ni 18 kati ya 19, huku Chadema kikiwa ndicho hakijasaini kanuni hizo kikishinikiza mabadiliko ya mfumo katika uchaguzi kikieleza kutoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wakati Dk Tulia akitangaza kuhamia jimbo hilo jipya, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi anatajwa kugombea jimbo hilo katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu kupitia Chadema.

Picha za Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli

Pamoja na kutajwa mwanaharakati huyo, mwenyewe amefunguka msimamo wake, huku akiwashukuru wananchi wanaomtaja kwa kuona namna anavyofaa na kumuamini katika safari hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli ameliambia Mwananchi leo Jumatano, Mei 28 kuwa hadi sasa maandalizi ya uchaguzi katika majimbo hayo yanaendelea vizuri.

Amesema msimamo wa chama hicho ni kutoshiriki uchaguzi iwapo hakutakuwapo mabadiliko ‘na kwamba baada ya vikao vya baraza la uongozi mkoani humo, watatangaza tarehe rasmi ya uchaguzi.

“Hakuna uchaguzi bila mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, uongozi ni endelevu bila kujali tunaingia au hatuingii kwenye uchaguzi, hii ni taasisi lazima tutekeleze wajibu wetu wa kusimamisha viongozi ili kusaidia huduma kwa wananchi,” amesema.

“Wananchi wawe tayari muda wowote, lakini wanapaswa kujua kwamba bila uchaguzi nchi hii bila Chadema kuwepo hii ni kujidanganya, tumaini pekee kwao ni Chama hiki,” amesema na kuongeza.

“Kama Chadema haitashiriki uchaguzi basi siyo uchaguzi badala yake waendelee kukiunga mkono haswa kipindi hiki kigumu tukipambana na dora kupata Reform mwaka huu,” amesema mwenyekiti huyo.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa baada ya uchaguzi wa ndani, wanatarajia kutoa ratiba ya uzinduzi wa kampeni ya ‘No Reforms No Elections’ mkoani humo inayotarajia kufanyika katikati ya mwezi Juni.

 

Mwabukusi atoa msimamo

Akizungumza na gazeti hili, Mwabukusi amesema msimamo wake katika uchaguzi wa mwaka huu ni kutoshiriki kugombea sehemu yoyote, huku akiwashukuru wananchi wanaomtaja kugombea.

Amesema pamoja na kutajwa katika Jimbo la Uyole mkoani Mbeya, yeye hajui, lakini ameshatoa msimamo katika mtandao wake wa X (zamani Twiter) akifafanua kuwa anayo mambo mengi ya kufanya kwa sasa.

“Mimi sijui kama wananitaja ila nimeshaeleza msimamo wangu kuwa safari hii sitagombea na msimamo wangu uko vizuri pale akaunti yangu ya X, Ninawashukuru wanaoniona nafaa na wanaoniamini ila safari hii sitagombea nina mambo ya kufanya kwa sasa” amesema Mwabukusi.

Related Posts