Rais Ruto awaomba msamaha Watanzania

Dar es Salaam. Rais wa Kenya, William Ruto amewaomba msamaha Watanzania na Waganda kama kuna jambo lolote ambalo nchi hiyo imekosea.

Rais Ruto ameyaomba radhi mataifa hayo leo Jumatano Mei 28, 2025, wakati wa Ibada Maalumu ya kuliombea taifa hilo iliyofanyika eneo la Safari Park nchini humo.

Akinukuu Biblia, Ruto amesema nchi yoyote isiyo na shukurani kwa kidogo inachopata basi haitoshukuru hata ikipata mafanikio makubwa, huku akiwataka raia wa nchi hiyo kuungana na kuwa kitu kimoja.

“Ninaposimama mbele yenu kuwaambia kuwa nina uhakika kesho ya Kenya ni njema na imebarikiwa. Kesho yetu itakuwa njema kuliko leo,” amesema Ruto.

Kutokana na kauli hiyo, Rais Ruto amewaomba radhi Watanzania na Waganda kwa mambo mabaya ambayo Wakenya wamewahi kuwafanyia.

“Majirani zetu Watanzania kama tumewakosea kwa namna yoyote tunaomba mtusamehe….na majirani zetu Waganda mtusamehe, vijana wetu kama kuna kitu tumekosea mtusamehe,” amesema Ruto.

“Tunataka kujenga uhusiano ambao utafanya taifa letu kuwa bora na linalosonga mbele kwa kasi. Najua leo Mungu kwa namna yake amefanya kuwe na tofauti za kisiasa na ndicho kinachoifanya nchi yetu kuwa ya kidemokrasia,” amesema Ruto.

Related Posts