Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson ameonya wabunge wanapochangia bungeni wasivunje kanuni, Katiba na sheria licha ya kuwepo kwa uhuru wa kujieleza.
Spika ametoa kauli hiyo kutokana na michango ya wabunge katika hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Maendeleo ya ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu iliyolenga kuwashambulia waliotajwa kuwa ni wanaharakati kutoka Kenya.
Dk Tulia amesema michango yote ya kibunge haipaswi kwenda kinyume na matakwa ya Katiba ya nchi na kanuni za Bunge na kwamba kauli hizo ni za wabunge na wala si msimamo wa Bunge.
Katika michango hiyo, wabunge Joseph Musukuma, Stella Manyanya, Elibariki Kingu, Jesca Msabatavangu, Mwita Getere, Tauhida Gallosi na Ferister Njawu walimtaja mwanasiasa Martha Karua kutoka Kenya wakimtuhumu kuwa ni mchchezi anayetaka kuruga siasa na amani ya nchi.
“Waheshimiwa wabunge, kifungu cha tatu cha sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge kinawapa nafasi wabunge kuchangia na kutoa maoni yao, lakini Kanuni ya 71 ya Kanuni za Kudumu za Bunge zinatoa nafasi ya uhuru wa majadiriano,” amesema Dk Tulia.
Hata hivyo, ameeleza kuwa baadhi ya michango iliyotolewa na wabunge ilionyesha kukiuka kanuni hiyo ya 71.
“Nawakumbusha kuwa mnapaswa kuzingatia matakwa ya Katiba, sheria na kanuni za Bunge, michango yetu iepuke kwenda kinyume na katiba na sheria tuliyojiwekea na mitazamo ya wabunge haipaswi kuonyesha kuwa ni msimamo wa Bunge na kwa kusema hayo, tuzingatie masharti tuliyojiwekea,” amesema Dk Tulia.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wabunge hao walisema wanaharakati kutoka nchini Kenya wanachezea amani na usalama wa nchi na wametaka kugeuza Tanzania kama choo cha kujisaidia na kuondoka bila kujua ni Taifa imara lenye nguvu na watu wenye akili za kujitambua.
Mwanasheria na Mwanaharakati wa Kenya, Martha Karua pamoja na Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga Mei 18, 2025 walizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kutakiwa warejee kwao kwa madai walikuwa wameingia nchini kinyume cha sheria walipotaka kwenda kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Kitendo cha kuzuia kwa wanaharakati hao kilizua maswali mengi kutoka kwa baadhi ya watu wakipinga kuwa haikuwa halali.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alizima kauli za waliopinga kuzuiwa kwa wanaharakati hao na kuonya kuhusu wanaharakati kutoka nje ya Tanzania wanaoingilia mambo ya ndani ya nchi yake.
“Tumeanza kuona mtiririko wa wanaharakati ndani ya kanda yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu sasa kama kwao wamedhibitiwa, wasije wakatuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibiwa, watu wanaishi kwa amani na usalama ni hapa kwetu,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania, ambapo aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama na Wizara ya Mambo ya Nje, kutotoa nafasi kwa aliowaita watovu wa nidhamu na kusema hakuwa na upande, lakini anachofanya ni kulinda nchi yake.
Kauli ya Rais Samia iliungwa mkono na Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri la Kenya, Musalia Mudavadi aliyesema kuna baadhi ya wanaharakati wamekuwa wkaitumia vibaya uhuru uliopo nchini humo.
Hata hivyo, mjadala huo haukupoa kwani siku moja baada ya kauli hizo, baadhi ya wabunge waliotoa kauli hizo walitajwa kushambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa watu waliowatuhumu kuwa wanatoka Kenya ama wenye vibaraka wao huko.