Unguja. Mkutano Mkuu wa Shirika la Viwango Barani Afrika (ARSO) unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 300, wakiwemo wadau wa viwango kutoka nchi zaidi ya 50, ndani na nje ya Bara la Afrika.
Mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika kisiwani hapa kuanzia Juni 23 hadi 27 mwaka huu, utaifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatano Mei 28, 2025, Mkurugenzi wa Idara ya Uandaaji wa Viwango kutoka Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Hafsa Ali Slim, amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni ishara ya mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha uandaaji wa viwango na udhibiti wa ubora nchini.
Ameongeza kuwa uwepo wa wageni kutoka nchi mbalimbali utatoa fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kupitia bidhaa na huduma zinazozalishwa pamoja na kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
“Hii ni fursa kubwa kwa wazalishaji kupata masoko ya nje ya Tanzania, hivyo wajasiriamali waitumie vizuri ili kukuza biashara zao,” amesema Hafsa.
Pia, amesema mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo atakuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Ameeleza kuwa kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Kuharakisha haki katika biashara ndani ya eneo la biashara huria barani Afrika kupitia mifumo madhubuti na viwango vilivyoainishwa.”
Akitoa historia fupi ya ARSO, amesema shirika hilo lilianzishwa mwaka 1977 nchini Ghana kupitia Umoja wa Afrika (AU) kwa kushirikiana na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (Uneca).
Amesema shirika hilo linaundwa na nchi wanachama 43 kupitia mashirika ya viwango kitaifa kutoka Afrika.
Amefafanua kuwa jukumu la msingi la shirika hilo ni kuoainisha viwango na utekelezaji wa mifumo ya udhibiti, ili kuongeza uwezo wa kibiashara wa ndani ya Afrika na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma.
Baadhi ya wafanyabiashara wamesema hiyo ni fursa kwa Zanzibar, mbali na kujitangaza, pia wataweza kubadilishana uzoefu katika masuala ya viwango.
“Hii ni fursa kubwa kama nchi, lakini katika sekta hii ya viwango, maana zipo nchi ambazo zimeshapiga hatua kubwa, kwa hiyo lazima jukwaa hili litumike kikamilifu,” amesema Othman Ali Saleh, mjasiriamali wa kutengeneza sabuni.