Teknolojia ya IIT Madras kuibua fursa za ajira Zanzibar

Unguja. Kutokana na umuhimu wa teknolojia katika dunia ya sasa, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras tawi la Zanzibar kimeanza kutoa mafunzo kwa vijana na watendaji wa taasisi mbalimbali ili kuwajengea uwezo na umahiri wa kutumia teknolojia katika kuendeleza taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Mei 28, 2025, na mkufunzi wa chuo hicho, Profesa Kannan Moudgalya, wakati wa mafunzo maalumu kuhusu matumizi ya kompyuta yaliyowahusisha wanafunzi wa shule za sekondari, vyuo vikuu, pamoja na watendaji wa taasisi mbalimbali.

Amesema kuwa chuo hicho kinaendelea kutekeleza mpango mkakati wa kuwajengea uwezo wanafunzi wa Zanzibar kupitia programu maalumu ya matumizi ya kompyuta, ambayo imelenga kuwasaidia kufanya kazi kwa weledi, kujiamini, pamoja na kuibua fursa za ajira baada ya kumaliza masomo yao.

Profesa Moudgalya amesema kuwa, kutokana na umuhimu wa teknolojia katika dunia ya sasa, chuo hicho kimeona ni vyema kutoa fursa kwa wanafunzi na wafanyakazi kujifunza matumizi sahihi ya kompyuta, hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia imekuwa chachu ya mabadiliko chanya katika elimu na utendaji kazi kwa ujumla.

Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kuwa chuo kinaongeza idadi ya wanafunzi wenye uwezo wa kutumia teknolojia kwa ufanisi, ili kuwawezesha kuboresha taaluma zao katika fani mbalimbali kupitia programu hiyo.

“Programu ya totoria ni nyepesi kuifahamu kwani inafundisha kwa maelekezo ya sauti na vitendo. Mfumo huu ni mwepesi na mtu yoyote ana uwezo wa kuufahamu,” amesema.

Profesa Kannan ameeleza kuwa mpango wa baadaye wa chuo hicho ni kufundisha taaluma ya teknolojia kuanzia ngazi ya sekondari ili kuwaandaa wanafunzi watakapoingia vyuoni kuwa na ujuzi wa kutumia kompyuta kwa ajili ya masomo yao sambamba na kuwa wataalamu wa IT wa baadaye.

Amefahamisha kuwa hiyo ni fursa muhimu kwa Zanzibar, hasa katika sekta ya elimu, kwani itasaidia kuleta mageuzi makubwa ya mifumo na kukuza teknolojia nchini.

“Mafunzo haya zaidi tunafundisha kwa njia ya vitendo ili washiriki wote watambue masuala ya IT, na wakitoka hapa waweze kuitumia kompyuta kwa malengo watakayokusudia,” ameeleza.

Naye mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha IIT, Ali Hamadi, amesema programu hiyo inawezesha kufanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuandaa ripoti, kufanya utafiti na uvumbuzi.

Amesema kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ulimwenguni, chuo hicho kitasaidia vijana kuingia katika mabadiliko ya sayansi na teknolojia, pamoja na kutumia fursa ya kujiajiri wenyewe.

Mbali na hayo, ameahidi kutumia teknolojia kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya maendeleo ya nchi na watu wake kielimu na kiuchumi.

Naye Kauthari Omar kutoka Sekondari ya Biashara amesema mfumo huo una lugha mbalimbali, hivyo unarahisisha kujifunza kupitia lugha unayoifahamu zaidi.

“Kwa kweli tunajifunza katika mazingira wezeshi, hakuna changamoto, kwani unafahamishwa kwa sauti na kwa lugha unayoipenda mwenyewe,” amesema.

Related Posts