Ubunge wa Siha unavyomtesa Dk Mollel, awalalamikia Takukuru

Siha. Mbunge wa Siha mkoani Kilimanjaro, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameibua gumzo wilayani humo, akituhumu kuhujumiwa ubunge wake huku akivihusisha vyombo vya usalama ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambapo taasisi hiyo imejibu hoja hiyo.

Siyo mara ya kwanza Dk Mollel kulalamika kuhujumiwa ubunge wake, mara ya kwanza, Machi 2025 aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook, akidai kuandikiwa barua na kamati ya nidhamu ya CCM Wilaya ya Siha kwa kosa alilodai kuwa ni kuwafukuza wezi waliojaribu kupora rasilimali za Siha.

Mwanzoni mwa wiki hii, ilisambaa sauti ya Dk Mollel kwenye makundi ya Whatsapp, akivituhumu vyombo vya usalama kumfuatilia anakokwenda wakati akitekeleza majukumu yake ya kibunge.

Inadaiwa kuwa Mei 24, 2025, Dk Mollel alikuwa na mkutano na wenyeviti wa vijiji na vitongoji wilayani humo ambapo kulionekana watu waliodaiwa ni kutoka kwenye vyombo vya usalama na yeye kusikika akiwarushia maneno akiwataka kutumia nguvu wanazozitumia kumfuatilia kwenye ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.

Kwenye kipande hicho cha sauti ya Dk Mollel, alisikika akisema: “Wameshindwaje kupata habari ya kuibiwa Sh133 milioni mpaka madiwani ndio wanakuja kugundua, hata wao hawajui….?”

“Mimi ni jeshi la mtu mmoja linaloongozwa na watu wa Siha, kwani tumetukana mtu hapa? Tumesema tunanyooka, wanamwita mtu mmoja Takukuru, sawa, hatukatai mtu kuitwa Takukuru, inawezekana kuna kitu cha kisheria, lakini tunataka nguvu mnayotumia kwenye siasa kwamba mbunge sijui kafanya nini, sijui diwani kafanya nini kuitwa Takukuru, tunataka hiyo nguvu tuione kwenye miradi yetu,” anasikika Dk Mollel kwenye sauti hiyo.

Mbunge huyo anaendelea kusema: “Na nyie ndugu zangu wenyeviti, kwa kweli nimekuja kuwaambia sisi ni wana-Siha naomba tusimame tuwe kitu kimoja hata kama kuna mahali tumewahi kutembea pamoja tofauti wewe rudisha moyo twendeni kwa sababu kazi kubwa mbele ni ya kusaidia watu wa Siha. Watu wameungana wananishughulikia kama simba.”

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Dk Mollel amekiri ni maneno yake aliyoyatoa kwenye mkutano wake na wenyeviti wa vijiji na kudai kuwa yalitokana na watu waliofuatilia mkutano huo.

Mbunge huyo alienda mbali na kuwatuhumu baadhi ya watu kuwa marafiki na watia nia ya ubunge mwaka huu katika jimbo hilo na kuwa wamechukua rushwa kwao.

“Mimi ni mbunge wa Siha ambaye mpaka sasa Bunge halijavunjwa, kwa hiyo, kazi yangu ni kupeleka kwa wanachama wa CCM na wananchi kuwaelezea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ni kazi yangu kama mbunge ili  nitakaporudi kuomba kura na kuomba kura za Rais na madiwani, watu wajue walipotupa mwaka 2020 ni nini tumefanya.

“Sasa, kinachotokea baadhi ya watu kwenye vyombo vyetu wanachukua rushwa kwa wagombea, wanakuwa marafiki wa watia nia kupita kiasi. Kwa hiyo malalamiko ya watia nia yamekuwa kama ni hoja ya kumfuatilia mbunge,” amesema Dk Mollel.

Aidha, Dk Mollel amesema lengo kubwa la yeye kuita mkutano ule na wenyeviti wa vijiji ni kuwaeleza utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi kiwilaya na kitaifa ili watakavyokuwa vijiweni na kwenye mikitano yao, watakavyoshambuliwa na watu wa upinzani wawe na hoja za kuwajibu.

“Sasa cha kusikitisha wakatumwa watu wa Takukuru na watu wa usalama kunifuatilia kuja kwenye kikao changu. Kilichoniudhi, nikawaambia naombeni hao watu waingie ndani wakae pamoja na wenyeviti tuangalie hiki kitu tunachokifanya, wakakataa kuingia.”

Ameongeza kuwa: “Mimi nikasema hawa watu tumekuwa tunapambana, hapa kuna baadhi ya miradi haiendi vizuri, tulikuwa na matatizo ya ushirika ya fedha, kuna wananchi wanalalamika fedha za ushirika zimepotea lakini hatujawahi kusikia ripoti inakuja kwa viongozi kupitia madiwani na wananchi, hatujawahi kusikia vyombo vyetu vikituripotia kwamba kuna hatari ya wizi unafanyika pale.”

Ameendelea kufafanua kuwa: “Nikawa nimeuliza, hawa watu yaani wagombea wenzangu wanazunguka wanafanya vikao usiku na kuna mmoja sasa hivi ana Landcruiser, amekabidhi vijana wanazunguka, hatujawahi kusikia wakimfuatilia huyo, wananifuatilia mimi.

“Nikasema hivi hawa jamaa tunaibiwa kuna fedha hazionekani,kuna wananchi wanalalamika kwenye masuala ya ubadhirifu hatujawahi kuwaona wakisaidia hao watu kufaulu hizo shida lakini wao wanachokiona kikubwa ni kunifuatilia mimi. Kwa hiyo nikasema hizo ni bangi tu hakuna kitu cha maana,” amesema.

Mbunge huyo amesema kama ni viongozi wanaokipenda Chama cha Mapinduzi (CCM) walitakiwa wasaidiane naye wakati anaboresha kura za chama hicho na siyo kukaa upande wa walalamikaji.

Amesema kabla ya kikao hicho, aliandika barua kwenye chama akieleza kuhusiana na mkutano huo na kwamba kama walihitaji kujua wangefika kushirikiana nae.

“Nimeandika barua kwenye chama wakati naita hao wenyeviti wa vijiji, si wangekuja tushirikiane wote pamoja kama walihitaji kujua kinachoendelea,” amehoji Dk Mollel.

“Mimi ni mbunge wa Siha napiga kazi mpaka siku bunge litakapovunjwa kitakapopulizwa kipenga cha CCM kwamba wagombea wote kila mtu ni mgombea tutaendelea kupambana kwa kanuni zilizopo.  Ila kwa sasa siyo sahihi kumzuia mbunge au kumpangia aitisheje kikao chake anapokutana na wananchi.

“Ninachojaribu kusema, mimi ninawaheshimu wenzangu sasa wao wanakosa heshima sijui wanataka na mimi nikazunguke majumbani kwao makoridoni kama wanavyozunguka hao watia nia,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia madai ya Mollel, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo amesema taasisi hiyo haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa Dk Mollel na kwamba kama ana malalamiko ayawasilishe ili yashughulikiwe.

“Mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote ya Dk Mollel yaliyowasilishwa ofisini kwangu na kama ana taarifa, azilete. Takukuru tupo kwa ajili ya kuhudumia wananchi wote, tutaifanyia kazi,” amesema Chaulo.

Related Posts