Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kimebaini watoto wanaozaliwa na changamoto katika ubongo wao, wanaweza kurudi katika hali ya kawaida iwapo watapatiwa mafunzo maalumu wakiwa chini ya umri wa miaka mitano.
Katika utafiti walioufanya kwa watoto 23,000 waliozaliwa mwaka 2016 ambao walihusishwa katika utafiti huo, 500 walibainika kuzaliwa na changamoto hizo na baada ya kupitia mafunzo hayo waliimarika.
Matokeo ya utafiti huo ni kengele kwa wadau wa elimu na watunga sera kufikiria namna ya kuanzisha mtalaa kwa watoto wa chekechea kabla ya umri wa kuanza shule.
Akizungumza leo Jumatano, Mei 28, 2025 wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya utafiti huo unaofanyika kupitia mradi wa N_REACH-ED, Mtafiti Mkuu, Profesa Karim Manji amesema awamu hii ya pili itahusisha watoto 3000 kutoka nchi tatu ikiwemo Nepal, Bangladesh na Tanzania kila nchi ikitoa watoto 1,000.

Watoto hawa ni wale waliopata ukosefu wa hewa safi wakati wa kujifungua au walizaliwa na uzito pungufu chini ya kilo 2.5 au walikuwa na maambukizi yoyote ya bakteria au walikuwa hawajatimiza muhula au hawajatimiza umri wa mimba, yaani njiti.
“Katika watoto 500 ambao walikuwa wana shida wakati ule, tuliwafuatilia mpaka wanafika umri miaka mitano tukaona kwamba asilimia kubwa yao 63 wanakuwa na upungufu kidogo wa hapa na pale na asilimia 4.8 walikuwa na matatizo makubwa ya mahitaji maalumu yaani disability,” amesema.
Profesa Manji ambaye ni daktari mbobevu wa watoto na mkufunzi wa chuo cha Muhas, amesema kisayansi hiyo ni njia mojawapo ni kuchangamsha na kuwafanya wawe na mawazo mapana zaidi, waweza kutafakari na kufikia kile kiwango cha kawaida.
“Tuliwahusisha wazazi wao na walimu wale waliokuwa shuleni, programu ya awali tukawa na hatua nane za kufundisha, kujitambua mwenyewe, kuchora, kuhesabu, kuzungumza, kusimulia na kusikiliza hadidhi, kujieleza, kuonyesha hisia kama furaha, huzuni nk…
“Ilikuwa kazi kubwa sana baada ya kumaliza ukiangalia walipoanzia tuliona tofauti kubwa sana kuwa na uwezo na uelewa kwa upana zaidi. Baada ya utafiti huu tumeona tufanye kwa watoto 3,000 kabla ya kuingia hatua ya tatu ikihusisha mikoani,” amesema.
Mkazi wa Temeke Rabia Abdalah ni miongoni mwa wazazi wa watoto walionufaika na mradi huo.

“Nilijiunga na huu mradi na kujifunza mengi kuhusu lishe yake na makuzi na pindi alipoanza shule. Ilinisaidia namna ya kumfundisha kuhesabu, kuchora, imenisaidia na kusaidia wazazi wa jamii yangu namna gani wafanye kumkuza na maandalizi yake ya shule,” amesema Rabia.
Baadhi ya watoto waliopata mafunzo hayo, wameonyesha uwezo wao wa kuimba, kucheza na kuzungumza wakati wa uzinduzi huo.
Awali akizindua mradi huo, Ofisa elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Mwalimu Gift Kyando amesema utafiti huo umekuja wakati sahihi, na kwamba uzinduzi wa mradi huo ni ishara mpya ya dhamira ya kitaifa kuhakikisha mtoto mwenye ulemavu anapata elimu jumuishi iliyo bora kuanzia awali.
“Changamoto bado zipo hasa kwa watoto wenye ulemavu kutoka familia duni na waliotengwa, wengi huingia shule wakiwa hawajajiandaa, walimu, wazazi na jamii haijajiandaa pia. Utafiti huu huenda ukatuletea kitu kingine kikubwa cha kufanya kwa watoto hawa,” amesema.
Mtafiti mwenza Dk Mustapha Miraji amesema utafiti huo utakweda kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum na wanaotarajia kuanza elimu ya awali.
“Tumeshafanya upembuzi yakinifu kusaidiana na maofisa elimu na wakuu wa shule zote katika wilaya mbili ambazo utafiti huu utafanyika. Wilaya ya Temeke tumepita katika shule 87 zilizopo katika Kata 26 na tukachagua shule 20 na Kigamboni shule 39 ndani ya Kata tisa pia tukachagua shule 20,” amesema Dk Miraji.
Amesema walimu watakaochaguliwa watapewa mafunzo maalumu na wakufunzi wa kimataifa, watakaokuwepo kwa ajili ya kufundisha maofisa elimu na walimu wakuu wote katika wilaya hizo mbili.