Viongozi barani Afrika wanakwama wapi?

Dar es Salaam. Hivi unajua kuwa Afrika ndilo bara pekee lenye zaidi ya asilimia 30 ya rasilimali zote za asili duniani? lakini ndilo bara lenye idadi kubwa ya watu masikini duniani.

Ukwasi huo wa rasilimali uliopo Afrika, hauakisi utajiri wa kiuchumi na maendeleo katika bara hilo kama inavyoeleza Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya watu milioni 460 wanaishi chini ya dola 2.15 (Sh5,773) kwa siku. Kwa maneno mengine, karibu nusu ya watu barani Afrika, wanakabiliwa na ukata, jambo linaloibua swali la Afrika inakwama wapi?

Upo uhusiano wa kisiasa na utawala kuhusu mkwamo wa Afrika, kama ilivyowahi kuelezwa na Mwandishi Nguli wa vitabu, Chinua Achebe katika Kitabu chake cha The Trouble with Nigeria.

Katika kitabu hicho, Achebe anaeleza, “tatizo la Nigeria (na Afrika) uongozi,” akisisitiza viongozi wa bara hilo wameshindwa kuyatafsiri madaraka kuwa chombo cha kuleta tija kwa wananchi.

Kwa sababu ya changamoto za uongozi, mataifa kadhaa ya Afrika yanajikuta yakiingia katika katika migogoro ya kisiasa na hatimaye kuathiri uchumi.

Hilo linasisitizwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki katika moja ya hotuba zake wakati wa Muhadhara wa Siku ya Afrika, akisema kuna changamoto katika muundo wa kiuongozi Afrika ndio sababu bara hilo halifikii linakotarajia.

Kwa mujibu wa Mbeki, muundo huo umekumbatia mifumo iliyoachwa na wakoloni, kiasi kwamba Waafrika wenyewe kwa wenyewe wanashindwa kuungana na hatimaye kila mmoja anatekeleza jambo lake.

Kiongozi huyo mstaafu anasema Afrika haikabiliwi na changamoto ya sera bora, bali inakumbwa na tatizo la ombwe la watekelezaji wa sera hizo kwa manufaa ya watu wake.

Ili kukabiliana na hilo, anasema kuna umuhimu kwa bara hilo, kuzalisha rasilimali watu itakayomudu utekelezaji wa sera hizo na hatimaye Afrika inufaike na rasilimali zake.

Sambamba na hayo, anasisitiza umuhimu wa Afrika kuwa na ujuzi wa kutosha wa ndani, ili kuepuka utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya bara husika.

Hata hivyo, anasema bara hilo lina wasomi na wataalamu wa kutosha kushughulikia changamoto zinazolikabili bila kutegemea usaidizi kutoka nje.

Kukosekana kwa taasisi imara zinazoyaweka pamoja makundi mbalimbali ya Waafrika kujadili kuhusu hatma ya bara lao, ni sababu nyingine inayotakwa na Mbeki kuikwamisha Afrika.

Kwa mujibu wa Mbeki, zamani Afrika ilikuwa na taasisi mbalimbali za vijana, wanawake na makundi mengine zinazowaweka pamoja kujadili na kujenga hatma njema ya bara kwa ujumla wake.

Katika muhadhara huo, anasema Afrika ilikuwa na taasisi ya vijana iliyowezesha kuwakutanisha wote kama Waafrika wakajadili kutafuta jawabu la changamoto za Afrika.

Kama hiyo haitoshi, anasema kulikuwa na taasisi ya wanawake iliyotekeleza jukumu hilo kwa upande wa jinsia ya kike, lakini kwa sasa zote hizo hazipo.

Kutoweka kwa taasisi hizo, anasema kunawafanya Waafrika wakose umoja katika kutafuta suluhu ya changamoto za ajira na maendeleo yao, hatimaye mataifa ya kigeni yanafanya kwa niaba.

“Bara letu linapaswa kujitegemea na linapaswa kutafsiriwa na sisi wenyewe na sio Wachina, Wahindi, Warusi na Wamarekani,” anasema.

Anasema taasisi za Afrika ndizo zinazopaswa kutafsiri sera za bara husika na kuonyesha namna bara hilo linavyopaswa kukua kiuchumi, kisiasa, ulinzi na mambo mengine.

“Bahati mbaya Waafrika hatulijui hilo na hilo ni tatizo kubwa. Rais Kikwete na watu wengine wa umri wake wanapaswa kujua, tulikuwa na taasisi zinazotuweka pamoja, lakini sasa hazipo tena,” anasema.

Awali, anasema kulikuwa na harakati za vijana kuhusu umajumui wa Afrika na walikutana na kujadiliana kuhusu nini linapaswa kufanywa kwa ajili ya Afrika.

Anasema lakini sasa hilo limepotea na hata ule umoja wa wanafunzi wa Afrika uliokuwepo na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu bara hilo, kwa sasa umepotea.

“Tunawezaje kupata jawabu la maswali kuhusu ajira na uwezeshaji wa vijana, ninachosema ni kwamba vijana nao wanapaswa kuwa sehemu ya watu wanaojibu swali hilo,” anasema.

Katika mahojiano yake na gazeti hili, Mwanazuoni Mkongwe, Profesa Issa Shivji anasema kuminywa kwa uhuru wa mijadala ya wanataaluma ni sababu ya mkwamo wa Afrika.

Anasema kuminywa kwa mijadala ya wanazuoni, kunazikosesha nchi uelewa wa wapi zinakosea, fikra mbadala na suluhu ya matatizo yake, ndio maana zinakosea kwa kujirudia.

“Maendeleo yanaongozwa na dira, itikadi, ufahamu wa hali ilivyo na hali unayotaka. Sasa hayo yote chanzo chake ni mijadala na nafasi nzuri ya kuwa na mijadala huru ni vyuo vikuu ndio kazi yao hasa,” anasema.

Profesa Shivji, anasema mwaka 2000 nchini ulianzishwa utaratibu uliowatambua wanazuoni kuwa sehemu ya watumishi wa umma na utaratibu huo umesababisha Serikali iingilie kila hatua ya uendeshaji wa vyuo.

“Sasa kama Serikali inaingilia utapata watu watakaokuwa na ujasiri wa kuzungumza? Na uongozi wa chuo utatakiwa kulinda uhuru wa chuo husika,” anasema.

Ili kutoka kwenye mkwamo huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi anasema kuna haja kwa Afrika kuimarisha taasisi zake, uchumi, miundombinu, utawala wa sheria na sekta nyingine muhimu.

Kufanya hivyo, anasema kutachochea ufanisi kwa Serikali, kadhalika kuhakikisha ustawi wa maendeleo ya wananchi.

Wakati hayo yanafanyika, anasema ni muhimu wananchi washirikishwe kwa kila hatua, ili nao wawe sehemu ya washiriki wa kuyafikia malengo kusudiwa.

“Wananchi wanaweza kushiriki kwa mawazo, ujuzi, ubunifu na namna nyingine zitakazowezesha kufikiwa kwa malengo yetu kama Afrika,” anasema.

Kutokana na rasilimali zilizopo, Profesa Kabudi anaona ni muhimu Afrika iwekeze katika ujuzi kwa watu wake, ili wawe na uwezo wa kuzitumia na kusimamia kwa manufaa ya kiuchumi wa bara lote.

Uwekezaji katika teknolojia ni jambo lingine lililotajwa na mwanazuoni huyo kama mbinu ya kuiinua Afrika kwa kile alichoeleza, utatanua wigo wa mafanikio ya sekta nyingine.

Sambamba na hayo, anasema bara hilo linapaswa kudumisha utawala wa sheria kwa kuanza kuifanyia mageuzi Bodi ya Ushauri kuhusu masuala ya rushwa, ili iwe taasisi imara inayowajibisha.

Related Posts