Wananchi washauriwa kunywa maziwa siyo anasa, kiburudisho

Morogoro. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa yenye mifugo mingi ambayo sifa yake kubwa ni kusababisha migogoro huku tija ya uzalishaji wa maziwa ikiwa ndogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya teknolojia duni za ufugaji.

Aidha wananchi wameshauriwa kuhakikisha wanakunywa maziwa kwani siyo anasa wala kiburudisho bali yana vitamini zote ndani yake.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba wakati akifungua maadhimisho ya Wiki ya Maziwa ambayo kitaifa inafanyika mkoani Morogoro kuanzia Mei 27 hadi Juni 1.

Waryuba amesema kuwa pamoja na uzalishaji mdogo wa maziwa lakini pia hata unywaji wa maziwa hapa nchini umekuwa mdogo.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mtu mmoja anatakiwa anywe wastani wa lita 200 za maziwa kwa mwaka lakini hapa Tanzania mtu mmoja anakunywa wastani wa lita 68 kwa mwaka sawa na asilimia 34, wenzetu wa Kenya wanakunywa wastani wa lita 130 na Uganda ni wastani wa lita 170 kwa mwaka,” amesema Waryuba.

Ameongeza, “Suala la kunywa maziwa siyo anasa ama kiburudisho bali ni chakula chenye vitamini karibia zote lazima tuhakikishe mifugo inakuwa na tija na inaweza kuzalisha maziwa ya kutosha na hilo tunaweza kwa kuwa hapa nchini tuna ng’ombe zaidi ya 39 milioni.”

Naibu katika Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Sospeter Mtwale amezitaka mamlaka za Serikali za mitaa kuwawezesha maofisa ugani waweze kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wafugaji katika kuhakikisha wanafunga kisasa na kuongeza uzalishaji.

Aidha naibu katibu mkuu huyo amewataka maofisa ugani walioteuliwa kwa sheria ya maziwa kuwa wakaguzi wa maziwa kwenye mamlaka za Serikali za mitaa kutekeleza majukumu yao ya kuhimiza maendeleo ya tasnia ya maziwa na kuhakikisha maziwa yanazalishwa kwenye mazingira bora na kuchangia Pato la Taifa.

“Maziwa yanayozalishwa hapa nchini yanachangia kwa asilimia mbili kwenye pato la Taifa huku tasnia hiyo ya maziwa ikikua kwa asilimia 2.3,” amesema Mtwale.

Awali, akitoa taarifa ya maadhimisho hayo Msajili wa Bodi ya Maziwa, Profesa George Masalya amesema pamoja na kufanya kongamano na utoaji elimu kwa vikundi vya wafugaji na wasindikaji, lakini pia wameweza kugawa maziwa kwa wanafunzi wa shule mbili za msingi katika Manispaa ya Morogoro.

Amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kufungua fursa za kwenye tasnia ya maziwa kwa kutambua kuwa maisha ni lishe na uchumi.

Baadhi ya wafugaji wameeleza sababu za kuwepo kwa uzalishaji mdogo wa maziwa lakini pia mwamko mdogo wa wananchi kunywa maziwa.

Mmoja wa wafugaji hao ambaye pia ni katibu wa chama cha wafugaji Wilaya ya Kilosa, Petro ole Melen amesema ni pamoja na mifugo duni inayotokana ana na mbegu za asili ambazo hazina uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha, kukosekana kwa malisho na wafugaji wengi kukosa elimu ya ufugaji bora.

Amesema kama Serikali itatoa elimu kwa wafugaji itakayoendena na ugawaji wa mbegu bora za kisasa za mifugo mkoa wa Morogoro utaongeza uzalishaji wa maziwa na hivyo wananchi wataweza kunywa maziwa yaliyobora.

Related Posts