Dodoma. Marufuku ya biashara ya nyama ya punda na mazao yake barani Afrika inatarajiwa kusaidia katika kulinda na kuongeza idadi ya wanyama hao, ambao walikuwa hatarini kutoweka kufuatia kuongezeka kwa mahitaji kutika nchi za Bara la Asia.
Aidha, kufuatia marufuku hiyo, Serikali ilifunga viwanda viwili vikubwa vya kuchakata nyama ya punda kwenye mikoa ya Dodoma na Shinyanga, ili kuruhusu waendelee kuzaliana katika kipindi cha miaka 15 ambacho marufuku hiyo itatekelezwa.
Punda ni mnyama mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi za nyumbani, hasa kubeba mizigo mizito ambayo wanyama wengine hushindwa kuhimili.
Kutoweka kwake kungeathiri kwa kiasi kikubwa familia nyingi, hasa za vijijini, ambazo hutegemea nguvu kazi ya mnyama huyo katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 29, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Benezeth Lutege amesema kuwa ili kunusuru mnyama huyo kutoweka wakuu wa nchi za Afrika walikubaliana kupiga marufuku biashara ya punda na mazao yake.
Lutege amesema takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2021 Bara la Afrika linakadiriwa kuwa na jumla ya punda milioni 53, lakini kila mwaka punda milioni 5.9 walikuwa wanachinjwa hivyo kutishia kutoweka kwa mnyama huyo duniani.
Amesema kuwa kwa kuliona hilo, wakuu wa nchi za Afrika walikutana jijini Dar es Salaam kujadili mustakabali wake ambapo walifikia azimio la kusitisha biashara ya punda na mazao yake kwa kipindi cha miaka 15, ili kutoa fursa kwa wanyama hao kuendelea kuzaliana na kurejesha idadi yao.

“Kwa hiyo nchi za Afrika zilikubaliana kusitisha biashara ya punda na mazao yake tangu mwaka 2021 ili kumnusuru mnyama huyo asitoweke duniani kwa sababu idadi ya vifo takriban milioni sita kila mwaka ilikuwa inatisha,” amesema Lutege.
Amesema baada ya miaka hiyo 15 kupita watakutana tena na kufanya tathmini ya idadi iliyoongezeka ili waone kama wataruhusu biashara hiyo kuendelea bila kuleta madhara ya kutoweka kwa mnyama huyo.
Amesema biashara ya nyama ya punda na ngozi yake imeshamiri katika nchi za bara Asia ambapo inasemekana ngozi ya mnyama huyo hutumika kutibu baadhi ya magonjwa, na kuwataka Waafrika waitumie fursa hiyo kufanya biashara pindi itakaporuhusiwa.
Naye daktari wa mifugo kutoka shirika lisilo la kiserikali la Inades Formation Tanzania, Charles Bukula amesema punda ni mnyama ambaye anavumilia mazingira magumu ya hali ya hewa pamoja na kufanyishwa kazi ngumu ambazo mnyama mwingine hawezi kufanya.
Aidha amesema mnyama huyo amekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hasa wanaoishi vijijini kwa sababu amekuwa akifanya kazi za kubeba mizigo ya kuni, maji, mazao na hata kwenye machimbo ya madini anatumika kubeba mizigo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Inades Formation Tanzania, Mbarwa Kivuyo amesema elimu iliyotolewa kwa wananchi itawasaidia kumfuga mnyama huyo kwa faida, tofauti na sasa ambapo wanamfuga bila kumzingatia kuwa ana faida nyingi za kiuchumi.
Amesema moja ya elimu waliyoitoa ni kuwapatia wanyama hao chanjo ya kuzuia minyoo ambayo huwa inawadhoofisha na kushindwa kufanya kazi vizuri, magonjwa ya kwato na majeraha yanayotokana na kuchapwa mijeledi wakati wa kufanya kazi.
“Punda ni mnyama ambaye ni mwelewa kwa sababu ukimfundisha anafundishika kwa urahisi na siyo lazima kutumia fimbo na mijeledi kumfundisha, maana akipata majeraha hataweza kufanya kazi kwa ufasaha,” amesema Kivuyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Juma Mnyika amesema biashara ya nyama na ngozi ya punda ilitishia kutoweka kwa mnyama huyo kwani idadi ya punda waliokuwepo wilayani humo mwaka 2016 ni 12,611 lakini hadi kufikia mwaka 2022 idadi hiyo ilishuka hadi kufikia 8,228.
Amesema kupotea kwa punda hao kulitokana na kushamiri kwa biashara ya ngozi ya punda ambapo wengi waliibiwa na kuchinjwa huku wezi wakiondoka na ngozi iliyokuwa inauzwa kwa thamani ya Sh200,000.