Dodoma. Kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan juu ya ‘wenye dhamira ya kukipasua chama hicho’ imekuwa kama fumbo ambalo limewaacha wanachama wa chama hicho na tafakuri tofauti, kila mmoja akiichambua kivyake.
Aidha, kauli hiyo imeelezwa na wasomi wa sayansi ya siasa kuwa inaashiria kwamba ndani hakuko shwari.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Mei 29, 2025 katika mkutano mkuu wa chama hicho, uliofanyikia jijini Dodoma, akisema kama kuna mwana CCM anayewaza kukpasua chama hicho ajitafakari.

Ilikuwa baada ya kuonyeshwa picha mnjongeo ya ramani ya jengo jipya la kisasa la makao makuu ya chama hicho, litakalogharimu Sh34 bilioni, ambalo jiwe la msingi liliwekwa jana Jumatano. Linatarajia kuikamilika mwaka 2027.
Rais Samia amesema chama hicho kwa maendeleo hayo kinakua, kina wapenzi na mashabiki wengi.
“Baada ya kuwa na jumba kama lile, heshima ile, wewe kama mwana-CCM, jiulize moyoni kwako, kweli una dhamira na moyo wa kupasua chama kama hiki? Tukishafika hatua kama ile, kweli utashawishika kupasua chama hiki? Sasa hiyo ni assignment (kazi ya kufanya), kila mtu akae ajiulize mwenyewe. CCM oyeee,” amesema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa pindi litakapokamilika jengo hilo litakuwa ni ishara ya ukuaji na uimara wa chama, akiwataka wanachama wote kushirikiana katika kukitumikia kwa umoja badala ya kukipasua.
Baada ya kauli hiyo iliyoibua shangwe, nje ya ukumbi huo, Mwananchi limezungumza na wajumbe mbalimbali wa mkutano huo kila mmoja akizungumza alivyoielewa.
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu amesema kitu kimoja ambacho wana CCM hawajui, CCM sio wao, bali ni wananchi na hakuna mtu atakipasua hicho chama afanikiwe.
“Kwa namna ambavyo Rais Samia ametekeleza ilani, jamani huyu Rais amefanya kazi kubwa kwa hii nchi kwa muda mfupi. Unataka kukigawa chama ili iweje kipindi hiki? Nataka nikwambie, amini maneno yangu, tembelea vijijini na mijini katoka sekta za miundombinu, maji, afya, elimu, kilimo na uwekezaji, usafirishaji na ujasiriamali,” amesema.

Kauli kama ya Kingu imetolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Mbunge wa zamani wa Kilolo, Venance Mwamoto kuwa kwa mafanikio yaliyofikiwa kwa utekelezaji wa miradi mikubwa, ni kichaa tu anayeweza kufikiria kukipasua chama.
“Mimi nachoweza kusema ni kichaa tu ndiye anaweza kufikiria kukipasua chama. Kwa mambo makubwa aliyoyafanya (Rais Samia) sisi wanachama tunamuunga mkono na tunamuombea kwa Mungu ili aweze kuyafanya makubwa zaidi,” amesema Mwamoto.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Ndele Mwaselela amesema kauli ya Rais Samia inafanana na maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa bila CCM madhubuti nchi itayumba.
“(Rais Samia) alikuwa akimaanisha kuwa kwa mwonekano, uzuri wa jengo na kwa uimara, sidhani kama kuna mtu atakuwa na dhamira ya kukipasua chama, bali uzuri huo utaleta umoja na kulinda chama,” amesema.
Kauli kama hiyo pia imetolewa na Jane Mihanji, mjumbe wa mkutano huo: “CCM ni chama imara na madhubuti kilichojengwa na kuimarishwa vema na viongozi wake katika awamu zote.”
Jane amesema uimara huu wa CCM umeifanya Tanzania pia kuimarika kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na kimaendeleo kwa jumla. Uimara huu wa chama na nchi umekuwa ukiwakera wenye husda ambao wanapenda kuona Tanzania ikianguka.
Amesema CCM ni moja ya vyama vikongwe na tangu kianzishwe hakijawahi kuyumba, ni imara kinachounda Serikali imara.
“Alichosema Rais ni tafakuri ya kutaka tujue tulikotoka, tulipo na wapi tunakwenda kwa mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Mihanji kuongeza:
“Mwenyekiti ametukumbusha tusilale fofofo, tuwe macho kukilinda chama chetu.”
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba amesema yeyote mwenye dhamira mbovu ya kukichafua chama hicho hawezi kufanikiwa kwa sababu chama hicho ni taasisi moja kubwa.
Amesema wananchi na wana CCM wanatambua ili kupata maendeleo ya haraka, kuwe na ustawi wa kutosha na wananchi waweze kuneemeka, wanahitaji CCM imara.
“CCM iko katika nafsi yetu, hadi uje uipasue utupasue sisi na si rahisi ukaja kutupasua watu ambao tuna mapenzi makubwa na chama hiki,” amesema.
Tarimba amesema kauli ya Rais Samia ilikuwa ni tahadhari tu, lakini anatambua kwamba wao wanaipenda Serikali inayoundwa na CCM, yeye na chama cha kwa sababu wanaona ustawi wa Taifa unategemea chama hicho.
“Msitie wasiwasi kwamba anaweza kuja mtu kupasua chama hiki, hawezi kutokea na sisi tutamparamia. Huyo mtu atakayethubutu kujitokeza eti anaonyesha ishara za kutaka kutupasua tutampasua yeye kwanza, tutamshukia kama mwewe,” amesema.
Amesema wako tayari kwa lolote lile kukilinda chama chao, kumlinda Rais na Serikali yake kwa nguvu zote.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na mkutano mkuu, Dk Saada Mkuya amesema tangu kuzaliwa kwa chama hicho sasa wanakwenda kujenga jengo kubwa ambalo ni la kisasa litakalokuwa na mahitaji yanayohitajika katika ulimwengu wa leo.
Dk Saada amesema wakati yote yanafanyika na chama hicho kikiwa ni rejea kwa vyama vingine vya ukombozi barani Afrika, litakuwa jambo la ajabu wakiona kwamba miongoni mwao sasa wanageuka na kuondosha dhamira za kusaidiana na viongozi wao katika kufanikisha yale waliyoahidi.
Amesema ukiona kuna mtu anafanya hivyo, ina maana huyo tangu mwanzo hakuwa na dhamira ya kuwa katika chama cha CCM.
Dk Saada amesema hiyo ni dhamira yake inayomsuta na pengine hakutaka maendeleo yote yatokee na sasa inamuumiza kuona hayo yote yanatokea kupitia usimamizi wa CCM nchini.
“Kwa hiyo kama mataifa yanatutambua, sisi ni chama pekee ambacho ni chama cha ukombozi na sasa hivi tumeona vyama mbalimbali vinakuja tunazungumza navyo tumefanyaje, basi wewe kama mtu mmoja lazima ujitafakari,” amesema.
Amesema mtu mwenye dhamira hiyo, inawezekana alikuwa CCM kwa masilahi yake, lakini inaonekana ameumizwa na maendeleo yanayofanyika na hivyo taswira halisi aliyonayo inajitokeza.
“Wanajiita ni wanachama wa CCM lakini hawasimamii kile ambacho kila mmoja anasimamia. Chama cha CCM hakina matatizo, kimeweka mifumo, vikao ambayo mtu yoyote aliye na mawazo tofauti hakatazwi kuyasema kwa utaratibu uliowekwa,” amesema.
Amesema kutoka hadharani kuzungumza kinyume cha mambo yanayotokea, huo ni ukiukwaji mkubwa na unaonekana kuwa haukuwa na dhamira ya dhati kuwa katika chama hicho.
“Kama hufuati katiba na kanuni za CCM maana wewe tunaweza kusema kwenye fedha, kule kwenye akaunti kuna madeni yasiyolipik,a tunaita doubtful debit kwa hiyo inawezekana ni doubtful debit kwa Chama cha Mapinduzi,” amesema Dk Saada ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar.
Mbali na kauli hizo za wana CCM, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema kauli ya Rais Samia ni ujumbe wa kukiri ndani ya chama hakuko shwari.
“Ni taarifa kwamba ndani ya chama hakuko shwari ingawa hawajasema nini kinaendelea, mambo hayako shwari, kuna msigano wa hoja na kutokukubaliana na mambo fulani Fulani, ambao unaweza kutafsirika kwamba unaweza kuleta makundi,” amesema
Kwa mujibu wa Dk Masabo, mara nyingi tunapokaribia kwenye uchaguzi, huwa kunakuwa na pilikapilika nyingi za wanasiasa.
“CCM walikuwa na pilikapilika ya suala la mgombea na mgombea mwenza wa urais wa Tanzania, hilo walishalimaliza kwa mbinu waliyoitumia, sasa kuna watu ambao hawaendani na msimamo ndani ya chama na kwa nyakati tofauti wamekuwa wakijaribu kutoa maoni kizani,” amesema.
Akichambua hoja hiyo, Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Matrona Kabyemela amesema kauli hiyo inaashiria kuna makundi yameanza kuibuka ndani ya chama hicho.

“Na haya makundi hayajaanza leo, yapo tangia tupate uhuru, makundi ni sehemu ya siasa na kiongozi mzuri hutambua makundi, tofauti zao na kuzitumia kujenga taasisi imara,” amesema.
Dk Matrona amesema kwa mukitadha wa nadharia ya taasisi, makundi ndio uhimarisha taasisi kama yatatumika vizuri, ingawa yakipuuzwa huwa yana uwezo mkubwa kuangusha taasisi.