Ripoti ya Mwaka ya Mfumo wa Malipo wa Taifa iliyotolewa hivi karibuni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), 2024 ilionyesha kuwa miamala ya mikopo ya kidijitali nchini Tanzania imeongezeka kwa asilimia 91.49 hadi kufikia Sh4.22 trilioni kutoka Sh2.20 trilioni mwaka 2023.
Hali kadhalika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya miamala pia iliongezeka kwa asilimia 64.77, ikipanda kutoka milioni 163.42 hadi milioni 269.30, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mfumo wa Malipo wa Taifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2024.
Ongezeko hilo, ambalo linaenda sambamba na ongezeko la watumiaji wa huduma za simu linaonyesha kukua kwa mahitaji ya huduma za kifedha kidijitali, huku simu ikiendelea kuonyesha kuwa ni nyenzo muhimu katika kukidhi mahitaji ya kifedha kwa Watanzania wengi.
Hivi sasa kupitia huduma mbalimbali za kidijitali unaweza kukopa, kulipia huduma mbalimbali, kutunza akiba, na hivi karibuni kumekuwa na huduma mpya ya uwekezaji katika mifuko ya uwekezaji na unachotakiwa kuwa nacho ni simu yako ya mkononi tu.
Mathalani, wakati wa kutangaza hesabu za awali za mwaka wa fedha wa Vodacom ulioishia Machi 31, 2025, Mkurugenzi Mkuu, Philip Besiimire alieleza mafanikio ya huduma za uwekezaji kupitia simu (M-Wekeza), akisema tangu ulipoanzishwa Novemba mwaka jana mapokeo yamekuwa ni mazuri.
Alisema katika kipindi cha chini ya miezi mitano, watumiaji wa huduma hiyo wamewekeza jumla ya karibu Sh25 bilioni, jambo linalodhihirisha mwitikio mkubwa na uaminifu mkubwa kwa huduma hiyo.
“Nina matumaini makubwa kuhusu athari chanya na ya kubadilisha maisha ya bidhaa yetu ya usimamizi wa mali, M-Wekeza, katika kuwawezesha watu kujenga uimara wa kifedha. Inawawezesha watumiaji kuweka akiba ndogo ndogo na kuwekeza katika hisa na dhamana kupitia wasimamizi wa mifuko ya uwekezaji,” alisema Besiimire.
Bosi huyo wa kampuni ya simu inayoongoza nchini kwa idadi ya wateja, alisema miongoni mwa sifa za kipekee za bidhaa hii ni kiwango cha chini kabisa cha uwekezaji kinachohitajika kuanzia Sh1,000, pamoja na urahisi na wepesi wa kufanya miamala kupitia simu ya mkononi, na pia uwezekano wa kuvuna uwekezaji muda wowote.
Besiimire alisema huduma hiyo inayotolewa kwa ushirikiano na Sanlam Investments East Africa Tanzania, inatoa uwezekano mkubwa zaidi wa kupata faida kuliko viwango vya wastani vya riba vinavyopatikana kwenye akaunti za akiba nchini Tanzania ambapo kiwango cha riba kinacholipwa ni hadi asilimia 13.
Aidha, wakati wa uzinduzi wa huduma ya M-Wekeza, Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni alisema hiyo ni hatua nyingine muhimu katika dhamira ya kampuni yao kuwawezesha Watanzania, kwa kutoa huduma mbalimbali za kifedha kidijitali.
“Tumebuni huduma hii ili iwe rahisi, ipatikane kwa wote na yenye kuwaletea faida. Iwe wewe ni mwekezaji mzoefu au mpya, M-Wekeza inatoa fursa salama na rahisi ya kuongeza kipato chako kupitia simu yako ya mkononi,” alisema.
Kama ilivyo kwa mifuko mingine ya uwekezaji, uwekezaji kupitia simu unadhibitiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Usalama (CMSA), ambayo inahakikisha uwazi na usalama, hivyo kuleta imani katika mchakato wa uwekezaji.
Wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, Nicodemus Mkama alisisitiza umuhimu wa huduma hizi, akisema ni hatua ya mabadiliko kuelekea kurahisisha upatikanaji wa fursa za uwekezaji hapa Tanzania.
“Ushirikiano huu kati ya Vodacom, Sanlam Investments na CMSA unaleta daraja linalowaunganisha Watanzania na masoko ya mitaji na hivyo kuwawezesha watu kutoka tabaka zote za kijamii kuwekeza na kujenga mustakabali wao wa kifedha kiurahisi.”
Jonathan Stichbury, Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Investments East Africa, anasema huduma ya M-Wekeza siyo tu inatoa riba ya kila siku kwa mapato, bali pia inaruhusu kutoa pesa papo hapo, hivyo kufanya uwekezaji kuwa rahisi na haraka kwa kila mtu.
Mchambuzi wa uchumi, Dk Lutengano Mwinuka anasema watu wanavutiwa na urahisi wanaoupata kupitia uwekezaji kwa njia ya simu, lakini pia faida inayovutia kwa wakezaji.
“Mwekezaji yeyote mara nyingi hutazamia faida kabla ya kuweka fedha zake. Mfano, M-Wekeza inaweza mpa mtu faida ya hadi asilimia 13 ya fedha aliyowekeza, kiasi ambacho kiko juu kidogo kuliko mifuko mingine kadhaa, suala linaloweza kuvutia wengi zaidi,” anasema Lutengano, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Pamoja na hilo, anaongeza kuwa kuwekeza moja kwa moja kutoka kwenye akaunti ya simu kunatoa urahisi zaidi kwa wateja wa mtandao husika, suala ambalo ni zuri pia.
“Uwepo wa mifuko mingi unaweza kuongeza ushindani. Fedha, kama ilivyo rasilimali nyingine huwa hazitoshi. Kwa hiyo, mwekezaji ataigawanya fedha yake au kuwekeza pale kwenye faida zaidi,” anasema, akifafanua kuhusu ongezeko la watoa huduma.
Naye, Mhadhiri wa uchumi wa fedha wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Aziz Rashid anasema majukwaa ya uwekezaji kupitia simu yanatoa urahisi wa kuwekeza wakati wowote bila mlolongo mrefu na kwa kuwa watu wengi wanatumia simu za mkononi, inakuwa ni rahisi kuwafikia watu wengi.
“Watu wengi, hususan wasio katika sekta rasmi, wanaweza kuwa wanaona majukwaa ya uwekezaji kupitia mitandao ya simu ni rahisi kwao, kwa kuwa hawana akaunti za benki. Kupitia simu zao, wanaweza sasa kuwekeza kiasi kidogo kadiri wawezavyo. Inawapa urahisi,” anasema Rashid.
Anasema majukwaa ya kidijitali huondoa ulazima wa kutumia mawakala wa uwekezaji au benki katika kununua vipande vya uwekezaji. Mteja anaweza kununua anavyotaka na wakati wowote bila kuingia gharama za ziada.
Hata hivyo, anasema kuna haja ya kuwa na jicho la udhibiti, mfano wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMSA), kwa sababu zinazokusanywa na amana za umma kwa mfumo wa mifuko ya uwekezaji mitandaoni, uendeshaji wao, uwekezaji unapaswa kuongozwa au kufuata miongozo kama walivyo wengine.
Zaidi kuhusu miamala ya simu
Kwa mujibu wa BoT, thamani ya malipo ya huduma kupitia simu za mkononi imefikia Sh198.85 trilioni katika mwaka 2024 kutoka Sh154.7 trilioni katika mwaka uliotangulia, huku idadi ya mawakala ikifikia 1,475,281 mwaka 2024 kutoka 1,240,052, mtawaliwa.
Uchambuzi unaonyesha kuwa, mwaka 2024, miamala ya mtu kwa mtu iliongezeka hadi kufikia milioni 479.11 yenye thamani ya Sh15.702 trilioni ikilinganishwa na miamala milioni 364.36 yenye thamani ya Sh11.323 trilioni iliyokuwapo mwaka uliotangulia.
Malipo kwa Biashara (P2B), pia, ukuaji wake ulishuhudiwa kuanzia mwaka 2020, ambapo idadi ya miamala iliongezeka kwa asilimia 28.52 na thamani ya miamala ilikua kwa asilimia 45.76 mwaka 2024.
Jumla ya miamala ya malipo ya huduma na bidhaa bilioni 1.74 yenye thamani ya Sh26.602 trilioni ilishuhudiwa mwaka 2024.
Ongezeko hili kwa mujibu wa Benki Kuu linaonyesha kuongezeka kwa matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wafanyabiashara na kuashiria mabadiliko makubwa kuelekea miamala ya biashara yenye ufanisi zaidi na inayopatikana kwa urahisi.