Pengo aliloacha Ngugi wa Thiong’o

Dar es Salaam. Afrika imepoteza mtu muhimu na mwanamapinduzi wa kweli, hivi ndivyo inavyoelezwa na waandishi wa kazi za fasihi wa Tanzania kufuatia kifo cha mwanafasihi na mwanataaluma Profesa Ngugi wa Thiong’o (87).

Ngugi ambaye ni raia wa Kenya alifariki dunia asubuhi ya Mei 28,2025 na taarifa ya kifo chake kuthibitishwa na mtoto wake Wanjiku wa Ngugi.

Mwanafasihi huyu anatajwa kama mwanamapinduzi aliyesimama imara kupinga fikra za kikoloni zilizotawala kwenye vichwa vya Waafrika walioshika hatamu baada ya kukoma utawala wa wakoloni.

Akizungumza na Mwananchi, mwandishi wa vitabu Richard Mabala amesema kifo cha Ngugi ni pigo kwa watunzi wa kazi za fasihi bali Afrika kwa ujumla kwani imepoteza mzalendo wa kweli.

Mabala amesema Ngugi amechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mwamko wa Waafrika katika matumizi ya lugha zao za asili na kuondokana na fikra za kikoloni.

“Lugha ni utamaduni, hili ni suala alilolisimamia katika maandishi yake ndiyo maana akiwa katika misukosuko ya kusumbuliwa na watawala akaanza kuandika kwa Kikikuyu lugha ambayo inatumiwa na jamii yake.

“Kubwa zaidi alikuwa tayari kuteseka akisimamia msimamo wake, alifungwa, akakaa gerezani na hata alipotoka hakubadilika. Alisimamia maono yake kama mwandishi siku zote aliandika akitaka watu wafungue macho na kupambana na unyonyaji,” amesema Mabala.

Msimamo huo wa Ngugi unathibitishwa na mwandishi wa vitabu Nyambari Nyangwine ambaye anaeleza kuwa miongoni mwa vitu alivyowahi kusisitizwa na nguli huyo wa fasihi,  ni kuandika maandishi ya kuwatetea na kuwafungua wananchi.

“Nilienda Chuo Kikuu cha Nairobi na kukutana na wabobezi mbalimbali wa fasihi akiwemo yeye, nilimueleza shauku yangu ya kujikita zaidi kwenye eneo hilo akaniambia siku zote nijikite kwenye kuandika maandishi ya kuwatetea wananchi wanyonge.

“Kifo chake ni pigo, ameacha pengo kubwa kwenye tasnia. Kwa kifupi Ngugi alikuwa shujaa wa kweli, mwandishi mwenye kuleta mabadiliko na alizipigania sana lugha za Afrika,” amesema Nyangwine.

Kwa upande wake, Profesa Emmanuel Mbogo amemtaja Ngugi kama Mwafrika aliyesimama imara kuhakikisha lugha za kienyeji zinatumika kwenye uandishi wa kazi za fasihi hivyo kuacha urithi wa Waafrika kujivunia Uafrika wao.

Kuna namna Ngugi alisukuma waandishi wa Afrika kutumia lugha za asili kwenye maandishi yao, alisisitiza hakuna sababu ya kuendelea kuandika kwa Kiingereza wakati Afrika ina lugha zake.

Aliweka msukumo kwenye kuandika kwa lugha za kienyeji na yeye akaanza kwa mfano aliandika vitabu vyake kwa Kikuyu kisha vikatafsiriwa kwa lugha nyingine. Nina kila sababu ya kusema tumepoteza sana katika ulimwengu wa fasihi na utamaduni wa Afrika,”amesema Profesa Mbogo.

Pamoja na hayo Ngugi anatajwa kama kinara wa mapambano ya utetezi dhidi ya udhalimu kama ilivyoelezwa na Profesa Penina Mlama.

Profesa Mlama amesema Ngugi alikuwa mstari wa mbele kupigania Waafrika wa kawaida ili wajikomboe kifikra na kuwa na sauti kwenye jamii zao.

Akizungumzia hilo Profesa Mugyabuzo Mulokozi amesema Ngugi ameacha somo kubwa kwa waandishi kuwa wapiganaji na watetezi wa wananchi wanyonge.

“Katika kazi zake nyingi alikuwa akiwaangalia watu wa kawaida na changamoto zao, aliweka msukumo kwenye kuwafundisha kutafuta namna ya kuzitatua.

Alifanya hivi kwa sababu aliona tabaka tawala la Afrika lina kasumba mbovu ya kuendeleza uonevu na udhalimu uliofanywa na wakoloni,”amesema Profesa Mulokozi.

Ngugi aljizolea umaarufu kupitia vitabu mbalimbali vya fasihi alivyoandika na kusomwa katika nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo riwaya za The River Between, Petals of Blood, Grain of Wheat na Decolonising the Mind: The Politics of Language in African Literature.

Ngugi pia aliandika vitabu vya tamthiliya zilizojizolea umaarufu kama want, This Time Tomorrow, The Trial of Dedan Kimathi na I will Marry When I want iliyomuingiza kwenye mgogoro mkubwa na viongozi wa Serikali ya Kenya iliyokuwa ikiongozwa na Jomo Kenyata.

Kazi hizo na nyingine nyingi zilimfanya mwanafasihi huyu kuingia kwenye mzozo na Serikali iliyokuwa ikiongozwa na hayati Rais Jomo Kenyatta hali iliyosababisha kukamatwa kwake na kufungwa gerezani kwa mwaka mmoja.

Kuanzia mwaka 1976 Ngugi alishirikiana na wanakijiji Wagikuyu karibu na Limuru kuanzisha maagizo ya tamthilia katika lugha yao ya Gikuyu.

Riwaya yake ya Petals of Blood ilichora picha ya watawala wapya Waafrika jinsi walivyochukua nafasi ya wakoloni wa awali wakidharau na kukandamiza wananchi.

Mwaka huo huo  aliandika tamthilia ya “Ngaahika Ndeenda” (I will Mary When I Want) iliyoibua mvutano mkubwa kati yake na viongozi wa Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Jomo Kenyatta.

Wakubwa katika serikali walikuwa na wasiwasi wakiogopa mwelekeo wa kimarxist wa Ngugi hasa alipotoka katika chuo kikuu na kuingia kati ya wananchi wa kawaida kwa njia ya maigizo yake katika lugha ya Gikuyu.

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi aliagiza kukamatwa Ngugi kwa misingi ya sheria ya usalama wa kitaifa.

Katika mwaka mmoja aliokaa gerezani, Ngugi aliandika riwaya ya kwanza kwa Gikuyu “Caitaani mũtharaba-Inĩ” (Shetani msalabani) akitumia karatasi inayopatikana chooni kwa ajili ya kujisafishia.

Ngugi aliamini kuwa kwa kutumia lugha za kienyeji pekee waandishi Waafrika watafikia wanachi wa kawaida na kushinda ukoloni mamboleo.

Hata alipoachiwa huru hakuruhusiwa kurudi kazini kwenye chuo kikuu alikokuwa akifanyia kazi,  ndipo mwaka 1982 aliamua kuondoka Kenya na kwenda kuanzisha maisha mapya nchini Uingereza.

Baada ya kuishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka 20 hatimaye mwaka 2004 Ngugi alirudi mara ya kwanza Kenya lakini hata hivyo alikutana na changamoto kadhaa ikiwemo yeye na mkewe kushambuliwa na kuibiwa vitu vyake.

Huyu ndiye Ngugi mwamba wa fasihi anayeungana na miamba mingine kama Chinua Achebe, Wole Soyinka, Okot P Bitek na wengineo wengi walioandika kazi  na kuonyesha utajiri wa  fasihi ya Mwafrika.

Related Posts