Unguja. Baada ya kuanzishwa kwa sera ya maji Zanzibar, wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi wameonyesha nia ya kushirikiana na Serikali katika kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa huduma hiyo mijini na vijijini.
Machi mwaka huu, Zanzibar ilizindua sera ya maji safi na usafi wa mazingira ambayo inaruhusu ushirikishaji wa sekta binafsi, kama inavyofanya katika sekta za afya na usafirishaji ambapo wameona mabadiliko makubwa na kuleta ufanisi.
Kutokana na mabadiliko hayo, huduma za maji kwa sasa Zanzibar zitaendeshwa na taasisi binafsi huku Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) itabaki kuwa mwangalizi na msimamizi mkuu kama ilivyo kwenye bandari na baadhi ya hospitali.
Akizungumza katika kikao cha wadau na wataalamu wa maji kisiwani hapa Mei 29, 2025 Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi amesema licha ya maji kuzalishwa kwa asilimia 98, lakini bado kuna changamoto kubwa na hayajawafikia wananchi kwa baadhi ya maeneo hususani vijijini na mkutano huo unalenga kuboresha huduma ya maji safi na salama pamoja na miundombinu yake.
“Uhalisia kuwa visiwa vya Zanzibar huduma ya maji inapatikana kwa kiwango kikubwa, lakini bado Serikali kupitia wizara imeona haja ya kuongeza nguvu na kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi,” amesema Kilangi.
Amesema tangu kuzinduliwa kwa sera ya maji safi na maji taka wafadhili mbalimbali wamejitokeza katika kuunga mkono hatua hiyo na utekelezaji ikiwemo Benki ya Dunia na wafadhili wengine kutoka nje kuisaidia Zanzibar.
Mbali na taasisi za kifedha katika mkutano huo pia umewashirikisha wasomi katika sekta ya maji kutoka nje ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kilangi amesema mindombinu ya maji iliyopo mingi imeshapitwa na wakati, lakini kupitia mkutano huo kutafanyika maboresho makubwa ili kutanua wigo katika miundombinu hiyo.
Amesema lengo ya kuanzishwa kwa sera ya maji safi na taka inaenda kuongeza kiwango cha maji na matumizi yake, kwani itakuwa njia moja ya kutumika katika kilimo na mambo mengine.
“Maji taka yana umuhimu wake na sera yetu imeonesha kuwa maji hayo yanaenda kuongeza shughuli za umwagiliaji katika kilimo, kwani yatakuwa hayana madhara,” amesema Kilangi.
Naye mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Dk Victor Kongo amesema mkutano huo una muhimu kwa Zanzibar, kwa vile unawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji na utajadili namna ya ukuaji na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama pamoja na miundombinu yake.
Amesema WB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa miradi ya Zanzibar hasa katika mambo ya huduma za jamii, hivyo itaendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa visiwa hivyo.
Kwa upande wake mwezeshaji msaidizi kutoka ActionAid, Anitha Bunono amesema wapo katika mipango kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wa Zanzibar wanapata huduma ya maji salama katika shule zao.