Morogoro. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na wataalamu wa ofisi ya Mkurugenzi imefanya ukaguzi wa maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa na kuendelezwa na wawekezaji, ili kufanya tathimini ya kina kuhusu uwekezaji uliofanyika ili kubaini kiasi cha upotevu wa fedha za mapato.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Takukuru mkoa, Ofisa wa Takukuru mkoani humo Bigambo Thomas amesema yapo maeneo mengi ya wazi ambayo yamevamiwa na watu kufanya uwekezaji katika maeneo hayo, hivyo halmashauri kupoteza mapato kutokana na kutokuwa na ufuatiliaji wa maeneo hayo.
Aidha Ofisa huyo amesema kuwa ufuatiliaji huo wa maeneo yote ya wazi yaliyopo ndani ya manispaa ya Morogoro utakuwa ni endelevu, ili kuwezesha matumizi sahihi ya ardhi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maeneo yanayomilikiwa na Halmashauri ya Manspaa.
‘’Kuwepo kwa hali hiyo tukabainisha baadhi ya maeneo ya wazi na kuweka nguvu kuhakikisha halmashauri inapata yale mapato yaliyokusudiwa, mataifa mengi duniani yanaendelea kupitia ukusanyaji imara wa kodi unaofuata sheria,” amesema Thomas.
Amesema katika kuhakikisha mapato ya Seikali hayapotei, Takukuru kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imefanikisha kuingiwa kwa makubaliano na mwekezaji anayejulikana kwa jina la SM Holding Msamvu.
Amesema katika kukusanya kodi itokanayo na maduka yaliyojengwa na mwekezaji huyo katika eneo la Msamvu Kiwanja namba 11 hadi 22 ambapo awali mwekezaji huyo amejenga maduka hayo bila kufuata sheria, kanuni na taratibu na miongozo ya mipango miji.
Ofisa huyo amesema kutokana na makubaliano hayo halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeanza kupata mapato ya kiasi cha zaidi ya Sh26.3 milioni kwa mwaka kupitia maduka hayo ambapo awali yalikuwa hayakusanywi na kwamba mapato hayo yatakusanywa kwa kipindi cha miaka kumi kama ambavyo imeainishwa kwenye mkataba wao wa upangishaji.
“Katika kipindi hicho cha miaka 10, halmashauri itapata zaidi ya Sh263.5 milioni na baada ya miaka hiyo 10 mkataba kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na SM Holding Msamvu utakapokoma na kuanzia hapo maduka yatakuwa mali ya halmashauri,” amesema Thomas.
Kuhusu ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo Thomas amesema kuwa Takukuru imefuatilia miradi ya maendeleo 26 inayohusu elimu, afya, maji na barabara yenye thmani ya zaidi ya Sh28.4 bilioni ili kubaini viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa rasilimali za umma na kujiridhisha na thamani ya fedha.
Hata hivyo kati ya miradi hiyo 12 yenye thamani ya zaidi ya Sh2.26 bilioni ilibainika kuwa na utekelezaji hafifu ambapo ushauri ulitolewa ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu, Thomasi amesema Takukuru imejipanga kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa na vinabainishwa ambapo amewataka wananchi kutia ushirikiano kwa Takukuru katika kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa wakati wote wa uchaguzi.
Baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusu uvamizi wa maeneo ya wazi ambapo wamesema hilo limetokana na baadhi ya wenyeviti wa mitaa kushindwa kuyalinda maeneo hayo.
Mmoja wa wananchi hao, Osward Nyamoga amesema kuna baadhi ya wenyeviti wamekuwa wakinufaika na maeneo hayo ya wazi, kwa kuwakodishia na wao wenyewe kuyafanya ni maeneo ya biashara.
“Mtu hawezi kutoka huko atokako akaingia kwenye eneo la wazi na kuweka kibanda cha biashara au akaamua kuliendeleza, maeneo yote yaliyovamiwa lazima Mwenyekiti atakuwa anahusika,” amesema.