Wadau wakutana kujadili mifumo endelevu ya chakula

Arusha. Wadau kutoka taasisi za Serikali, mashirika ya umoja wa mataifa, sekta binafsi wamekutana kwa siku mbili jijini Arsuaha katika warsha ya kujadili namna ya kuboresha mifumo ya chakula nchini.

Wadau hao wamekutana kuanzia leo Alhamisi Mei 29, 2025 ambapo pamoja na masuala mengine watajadili namna ya kuongeza uelewa wa kina wa mifumo ya chakula na kuendeleza mifumo hiyo ikiwemo ushirikishwaji wa jamii na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mwakilishi na Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Sakphouseth Meng amesema kilimo ni sekta muhimu kwa uchumi wa Tanzania ikichangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa huku ikiaajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu wote.

Amesema wanakutana hapo kwa lengo la kuleta mabadiliko ya mifumo ya chakula nchini kuanzia uzalishaji na usambazaji wa chakula, kulinda mazingira na kushughulikia changamoto kama vile utapiamlo na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kilimo bado ni sekta muhimu kwa uchumi wa Tanzania, kwa hiyo mabadiliko yake ni muhimu kwa ukuaji wa kilimo na kwa ustawi na ustawi wa Watanzania wote. Na tangu mwaka 2021 Tanzania imekuwa ikitumia jitihada mbalimbali za Kimataifa kurekebisha mifumo yake ya chakula,”

“Mabadiliko haya yanahitaji uwekezaji katika kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabia nchi. Mabadiliko ya mifumo ya chakula inahitaji ushirikiano, uwekezaji wa kimkakati kutoka kwa wadau wote,” amesema.

Mwakilishi huyo amesema mpango wa kuendeleza mifumo endelevu ya chakula unaotekelezwa na Shirika la Chakula Duniani (Fao), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Ifad umelenga kusaidia kuimarisha mifumo ya chakula Tanzania na kuvutia uwekezaji.

Awali Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Abdul Mhinte, amesema kuna miradi miwili inafadhiliwa na wadau mbalimbali wakiwemo Ifad inayogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 200.

Amesema miradi hiyo miwili ya miaka mitano inatekelezwa hapa nchini kuanzia mwaka huu 2025 ni miradi inayoshughulika na masuala ya maziwa na uvuvi.

“Lengo la miradi hii miwili ni kukuza uzalishaji na kuangalia mifumo mizima ya uzalishaji wa vyakula katika maeneo hayo, kuanzia inavyozalishwa hadi inapomfikia mlaji hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.

Naibu huyo amesema Tanzania inajitosheleza kwa chakula licha ya baadhi ya kaya hasa za vijijini kutokana na sababu mbalimbali na kuwa miradi kama hiyo inasaidia kuboresha mifumo ya chakula ili kuona kinawafikia walaji vikiwa na ubora unaostahili, vitoe lishe inayokusudiwa kwenye afya ya binadamu.

Ofisa Kilimo Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo, Margaret Natai aliyemwakilisha Mratibu wa mifumo ya chakula nchini, amesema wao kama wizara wanashirikiana na wadau wengine ili kutekeleza mikakati ya kuhakikisha mifumo endelevu ya chakula nchini inatekelezeka.

Amesema mwaka 2021 waliandaa malengo katika sekta mbalimbali na wanayo miongozo inayowaongoza ikiwemo kuangalia usalama wa chakula, ulishaji wa watoto shuleni, upotevu wa chakula na usindikaji.

“Kutokana na hayo kila mdau hapa ana nafasi ya kushiriki na kikao cha leo tunaelimisha wadau waelewe namna ya kujipanga kufikia malengo ikiwemo namna ya kutumia teknolojia bunifu katika uzalishaji,” amesema Ofisa huyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar, Asha Zahran Mohamed amesema warsha hiyo itawasaidia kutoa elimu kwa wananchi katika kuboresha mifumo ya chakula, uzalishaji wa nyama na maziwa.

Related Posts