Shinyanga. Baadhi ya wakulima wa zao la pamba mkoani Shinyanga wametoa sababu inayowazuia kusajili biashara zao katika mfumo wa ununuzi na uuzaji ni matumizi ya mizani feki kwa wanunuzi ambayo inawasababishia hasara.
Hayo yamebainishwa leo Mei 29, 2025 katika mkutano wa wakulima wa zao la pamba, kampuni ya ununuzi, pamoja na vyama vya ushirika wa kilimo na masoko (AMCOS) uliofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga,
“Tatizo kubwa ambalo linatukumba sisi wakulima ni matumizi ya mizani feki ambayo inasababisha hasara kwa mkulima mtu anaona ni bora aendelee kufanya biashara kama zamani,” amesema Juma Kija.
Baadhi ya wakulima wa zao la pamba mkoani Shinyanga.
“Serikali ifanye mchakato wa kutambua mizani itakayotumika katika upimaji ili kuepuka hasara kwa wakulima sababu lengo la huu mfumo ni kumnufaisha mkulima” amesema Jackson Emmanuel.
Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Revocatus Lutunda amesema kuwa manispaa hiyo kwa kushirikiana na wakala wa vipimo, imejipanga kuhakikisha mizani hazitachezewa na baadhi ya wanunuzi wasio waaminifu,
“Tutahakikisha mkulima anapata malipo stahiki kulingana na uzito halisi wa pamba anayoifikisha kwenye kituo cha ununuzi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wakala wa vipimo husika” amesema Lutunda.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amewataka wakulima wa zao la pamba, kampuni za ununuzi, pamoja na AMCOS kuhakikisha wanazingatia taratibu rasmi za ununuzi na uuzaji wa pamba kwa msimu wa 2025/2026,
“Pamba yoyote itakayobainika kununuliwa nje ya mfumo rasmi, itataifishwa mara moja, wakulima mnatakiwa kufanya biashara kupitia mfumo wa ununuzi na uuzaji” amesema Mtatiro.
Ameongeza kuwa, “Serikali haitavumilia vitendo vya udanganyifu, na kwamba usimamizi madhubuti utaimarishwa ili kuhakikisha mfumo wa ununuzi wa pamba unaendeshwa kwa uwazi na kwa masilahi ya mkulima” amesema Mtatiro.
Mwakilishi kutoka Bodi ya Pamba, Benson Mhimba amesema kuwa mwongozo wa usimamizi wa ununuzi wa pamba kwa msimu wa 2025/2026 unaelekeza kuwa AMCOS itaruhusiwa kuuza pamba kwa kampuni itakayotoa bei ya juu zaidi kwa siku husika,

“Kila mnunuzi anapaswa kuweka bango la kuonyesha bei ya ununuzi kwa siku hiyo kwenye kituo cha ununuzi, na bei hiyo haitaruhusiwa kushuka chini ya bei ya dira iliyowekwa” amesema Mhimba.