Dar es Saalam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wiki mbili kwa wafanyabiashara ndogondogo walio katika barabara za kuingia soko kuu la Kariakoo kuondoka.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni kuelekea ufunguzi wa soko hilo, lililokuwa katika ukarabati tangu Julai 10, 2021 baada ya kuungua.
Kutokana na tukio hilo, Serikali ilitoa zaidi ya Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati, ukarabati ulioenda sambamba na ujenzi mpya wa soko dogo.
Katika kipindi chote hicho wafanyabaishara waliokuwa wakifanya shughuli zao sokoni hapo, walihamishiwa katika masoko ya Kisutu, Karume na Machinga Complex.

Meneja wa Shirika la Masoko, Ashraph Abdulkarim
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano Mei 28, 2025 kuhusu maendeleo ya soko hilo, Chalamila amesema tayari limeshakamilika kwa asilimia 98 na kinachofuata ni maandalizi ya kulifungua japo hakuweka wazi tarehe rasmi.
Kati ya maandalizi hayo amesema ni pamoja na kuwaondoa Wamachinga waliopo barabara za kuingia sokoni hapo, na tayari wameshawapa maagizo viongozi wao.
“Mpaka sasa ninapozungumza soko limeshakamilika kwa asilimia 98 na kubakia matengenezo madogo madogo ikiwemo uzio.
“Baada ya hapo kinachosubiriwa ni Waziri mwenye dhamana wa Tamisemi, kufanya ziara ya mwisho kukagua na kujiridhisha ukamilifu wake kabla halijaja kuzinduliwa, uzinduzi unaotarajiwa kufanywa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Chalamila.
Hata hivyo ameleleza kuwa pindi soko hilo litakapofunguliwa kuna utaratibu umewekwa wa kuwapa baadhi ya maeneo wamachinga, ambapo kuna maduka madogo watawekwa ili kupunguza adha hiyo ya wao kukaa barabarani.
Wakati Chalamila akisema hayo, Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania na Mwenyekiti Soko la Kariakoo, Stephen Lusinde,amesema kazi ya kuwaondoa si kubwa kwao kwa kuwa hata wamachinga wenyewe wanajua maeneo hayo wameyavamia.
Lusinde amefafanua kuwa tangu awali wakati wanawapanga maeneo hayo ya Kariakoo, kuna barabara za mitaa walikubaliana waziache wazi na nyingi ndio hizo zinazoingia katika soko hilo.
Ametaja barabara hizo kuwa ni pamoja na ile ya Mtaa wa Nyamwezi -Mkunguni, Nyamwezi-Tandamti, Tandamti-, Sikukuu -Mkunguni na Mkunguni – Congo (Bigborn).
“Katika maeneo hayo wafanyabiashara wanaelewa kuwa tulishakubaliana pawe wazi ila kwa wale wakaidi waliamua tu kuvamia na wengine maeneo wanayo walishapangiwa, hivyo ikifika muda tutafanya kazi yetu na hakutakuwa na wa kumlaumu,” amesema Lusinde.
Kuhusu na wao kupata maeneo ya kufanya biashara ndani ya soko hilo la kimataifa, Mwenyekiti huyo amesema ni taarifa njema kwao ukizingatia ni kilio chao cha muda mrefu, huku akieleza vipaumbele vitakuwa kwa wale ambao hawakuwa na maeneo na tayari wapo katika kanzidata yao.
Mmoja wa machanga ambaye hakutaka jina lake liandikwe, ameshauri wangeachwa mpaka hapo uhakika wa soko litakapofunguliwa, kwa kuwa ni sehemu ambayo wanategemea kupata rizki kwa sasa.
Hali ya urejeaji wa wafanyabiashara
Akizungumza kuhusu urejeshwaji wa wafanyabaisaara waliokuwa sokoni hapo kabla halijaungua, Meneja wa Shirika la Masoko, Ashraph Abdulkarim amesema kati ya wafanyabaishara 1520 ni 1159 ndio waliojisajili kwenye mfumo kwa ajili ya kuomba kurejeshwa na mpaka sasa tayari asilimia 81 wameshapewa mikataba na kupangiwa maeneo.
Amesema wafanyabiashara hao wamewagawa katika makundi matatu, wakiwemo wa vizimba watakaokaa sakafu ya kwanza na ya pili, huku kundi la pili ni wake wanaouza bidhaa za nafaka, viatilifu na vifungashio ambao watakaa ghorofa ya tatu,nne na tano.
Wakati kundi la tatu ni wale ambao hawakuwepo sokoni hapo ambao kuanzia wiki ijayo watatangaziwa kuomba nafasi kwa wenye uhitaji na maeneo.
“Nawakaribisha wanaotaka kuja kufanya biashara katika soko la Karikaoo waje kwa kuwa tuna nafasi kubwa, ikiwemo ya kuegesha magari ambayo ina uwezo wa kubeba magari 900 kwa wakati mmoja kutoka 350 ilivyokuwa awali.
Kwa upande wao wafanyabiashara, wamesema wanashangazwa na idadi inayosemwa kwani tayari wamepangiwa maeneo.
Hamza Idd, amesema mpaka sasa waliopangiwa ni wafanyabiashara wa mbogamboga na kati yao ni 40 tu ndio walioonyeshwa maeneo.
“Inakuwaje asilimia 81 waseme wamepangiwa wakati hata asilimia 60 halijafika na yote waliyoyaanzisha hakuna hata lililokamilika ikiwemo uhakiki, Soko kuu, soko dogo hawajapewa mkataba na mbogamboga pia sio wote, iweje waseme ni asilimia 81,” amesema Iddi ambaye pia ni Mwenyekiti wa soko la wazi.
Naye Msuya Minja mfanyabiashara wa soko dogo, amesema bado kitengo chao hakijaonyeshwa maeneo mpaka sasa na wala hawajui ramani ya soko hilo ilivyo.
“Mie nadhani katika mchakato huu, kuwe na ushirikishwaji wa karibu kati ya uongozi wa masoko na wafanyabiashar, wani kumekuwa na vitu vingi tunfichwa ambavyo vinaongeza sintofahamu.
“Mfano hili la idadi ya waliopewa mkataba na vizimba, tunachojua ni kitengo kimoja tu mpaka sasa ndio wameonyeshwa maeneo hayo,” amesema.
Hilo linaungwa mkono na Mwenyekiti wa soko kubwa John Shao, amesema hawapingani na serikali ila shida yao ni kutoshirikishwa katika mchakato huo.
“Mimi ninavyoona mpaka sasa asilimia 75 bado hawajaonyeshwa nafasi zao waliokuwa ndani ya soko na hata kwenda kuliona soko kujua linafafananje badobado,” amesema Shao.
Hata hivyo ameeleza wafanybiashara wengi wana manung’uni katika hili, ikiwemo maeneo ambayo tayari wengine wamepangiwa kutoridhishwa nayo.