Ilani mpya CCM kuzalisha ajira milioni nane kwa vijana

Dar es Salaam. Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2025/30 imeanisha hatua 11 za kuzalishaji ajira zenye tija zisizopungua milioni nane katika kipindi cha miaka mitano kupitia Serikali watakayoiunda endapo kitashinda kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba.

Katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho tawala ya mwaka 2020/25 waliahidi kutengeneza ajira zisizopungua milioni saba za sekta rasmi na isiyo rasmi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kitila Mkumbo ameeleza hayo leo Ijumaa Mei 30, 2025 wakati akiwasilisha ilani ya chama hicho,yenye vipaumbele vinane mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM uliofanyika jijini Dodoma.

“CCM inatambua kuwa nyenzo kubwa ya kuwawezesha wananchi ili waongeza kipato ni kuongeza fursa za ajira kwa kuongeza shughuli za kiuchumi,”amesema Profesa Mkumbo.

Profesa Kitila amezitaja miongoni mwa hatua hizo, kuwa ni kuanzisha programu maalumu ya ujenzi wa mitaa ya viwanda vidogo na vya kati vitakavyoongeza thamani ya mazao kwa kila mkoa na wilaya.

“Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itajenga angalau kiwanda kimoja kwa mtaa ikilenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi, ufugaji, misitu madini na bidhaa za ujenzi kwa kuzingatia fursa za kijiografia kwa kila mkoa na wilaya.

“Lengo ni kuona nchi yetu inaachana na taratibu za kusafirisha mazao nje ya nchi ambayo hayaongezwa thamani. Hii ndio njia pekee itakayotusaidia kuzalisha ajira kwa vijana,” amesema Profesa Kitila.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ilani, amesema hatua nyingine ni kuwawezesha wabunifu wa biashara changa kwa kuwapatia mitaji ya kuanzia, ujuzi, fursa za masoko na kuendeleza bunifu hizo.

Profesa Kitila amesema wataanzisha utaratibu maalumu wa wanafunzi wa elimu ya juu kutumia muda wao ziada kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

“Tuna changamoto vyuo vyetu vya elimu ya juu na taasisi zingine za elimu, wanafunzi wetu wa sasa wana (kula, kulala na kusoma).Tunataka kuwaongeza ‘K’ ya nne ya kula, kulala, kusoma na kazi ili wakimaliza mafunzo yao wawe na uzoefu na stadi zitakazowasaidia kujiajiri na kuajirika kirahisi wakiingia mtaani,”amesema Kitila huku akipigiwa makofi.

Kwa mujibu wa Profesa Kitila, jambo jingine ni kuweka mazingira wezeshi na kimkakati kwa kuhamasisha uanzishaji wa kampuni na vyama vya ushirika.

“Katika kuwajengea uwezo vijana wa kuajirika nje ya nchi, ndani ya miaka mitano Ilani imeweka utaratibu ambapo Serikali itaanzisha vituo vya mafunzo stadi maalumu kwa ajili ya kuwaanda vijana katika kushindana kupata fursa za ajira nje ya nchi,” amesema Profesa Mkumbo ambaye ni Waziri Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji).

Amefafanua kuwa ajira hizo zitazalishwa kupitia sekta rasmi na zisizo rasmi huku Serikali ikiendelea kukuza na kuwezesha shughuli za kiuchumi zitakazoanzishwa na Watanzania ili kuwapa fursa ya kuendeelea kushiriki katika   uchumi wa nchi.

Related Posts