Unguja. Ili kukabiliana na changamoto za umasikini na ukosefu wa ajira, kilimo mseto cha mwani na ufugaji wa majongoo bahari kimebainika kuwa mojawapo ya mbinu bora za kutatua tatizo hilo.
Kwa msingi huo, wakulima wanashauriwa kuwekeza na kujikita zaidi katika shughuli hizo za uzalishaji.
Hayo yamebainika kufuatia mafunzo ya kilimo hicho kutolewa kwa wakulima 80 katika shehia za Pwani Mchangani, Matemwe na Tazari, zilizopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mtaalamu wa Uvuvi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Hashim Muumin Chande, amesema kuwa ingawa hajataja aina ya tafiti wala waliozifanya, utafiti mbalimbali kuhusu kilimo mseto tayari zimefanyika Zanzibar na zimeonesha matokeo chanya.
Kwa msingi huo, amesisitiza umuhimu wa wakulima kujikita katika kilimo hicho ili kuchochea mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi pamoja na Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupewa mafunzo ya vitendo na nadharia ya kilimo mseto cha ukulima wa mwani na ufugaji wa majongoo bahari katika eneo moja huko Kibopwa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mei 30, 2025, baadhi ya wakulima hao wamesema hatua hiyo italeta mabadiliko makubwa katika kilimo chao kwani watapata mazao ya aina mbili tofauti katika eneo moja.
Mkulima wa mwani, Khadija Abdalla Makame wa Pwani Mchangani amesema mafunzo hayo yamewabadilisha kutoka hatua moja kwenda nyingine kutokana na ujuzi wa kupanda mwani na kufuga mazao mengine ya baharini ambacho italeta tija kwa upande wao.
“Tunashukuru kwa elimu hii, tupo tayari kuwa walimu kwa wengine kuwafundisha namna bora na nzuri ya kufuga majongoo katika eneo hilihilo unalima mwani,” amesema.
Amesema hatua hiyo itaongeza vipato vyao na kuzisaidia familia kutoka maisha ya chini na kuwa na maisha bora.
Mkulima mwingine wa mwani, Nuhu Haji Khamis kutoka Shehia ya Tazari amesema mradi huu umewapa mwamko mkubwa wa ukulima wa mwani na ufugaji wa majongoo jambo ambalo litaleta mabadiliko makubwa katika jamii yao.
Mkuu wa Kitengo cha ukulima wa mwani kutoka Idara ya Maendeleo na Mazao ya Baharini Zanzibar, Ali Makame ametoa wito kwa wahitimu wa mafunzo hayo kuitumia fursa hiyo na kuwa mfano katika kuleta matokeo mazuri hapa nchini.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa wakulima hao kuwa na ulinzi shiriki katika maeneo yatayofugiwa majongoo kutokana na thamani kubwa ya zao hilo ili kuondokana na changamoto ya wizi kutokana na Shirika kwa kushirikiana na Serikali lipo tayari kujenga mashamba ya kilimo hucho.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini Zanzibar Dk Salum Soud Hamed, amewataka wakulima hao kuchukulia kwa uzito wa mafunzo hayo ya kilimo mseto ili kuongeza thamani ya mazao ya baharini.
Dk Salum amesema mafunzo hayo yatasaidia kukuza sera ya uchumi wa buluu ikiwa ni miongoni mwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kupitia kilimo cha mwani na majongoo bahari.
Amesema mafunzo hayo yapo chini ya mradi wa mabadiliko ya mifumo ya chakula ili kukuza ukuaji wa uchumi jumuishi na usalama wa chakula na lishe nchini.
Vilevile ametoa wito kwa jamii kuitumia vizuri fursa ya mafunzo kwa ajili ya kutengeneza mashamba ambayo yataleta faida kwao na Taifa kwa ujumla.
Huo ni mkakati kuongeza uzalishaji wa mwani na majongoo bahari sio tu kwa ajili ya vipato vya wakulima, bali kukuza pato la taifa kwani mazao hayo yanathamani kubwa katika masoko ya nje ya nchi hususani China.