Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wajumbe wa chama hicho kuhakikisha mchujo wa wagombea unafanyika kwa haki na weledi ili kulinda hadhi ya chama, akisisitiza kuwa ni muhimu kuepuka kuwapitisha watu wasiostahili.
Akihitimisha Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa leo Ijumaa, Mei 30, 2025, jijini Dodoma, Samia amesema chama kisiruhusu kuathiriwa na tabia za baadhi ya watu waliopoteza mwelekeo wa kisiasa.
“Tukitoa mwanya ndugu zangu, tukapitisha wanaotafuta tu, na mie niwemo, ndiyo tunapata wale wanaokwenda huko – chama kinakuwa Gwajimanised,” amesema Rais Samia na kuongeza, “Kwa vyovyote vile tusigwajimanised chama chetu, Magwajima tuyaache nje,”
Amesisitiza umuhimu wa kuwapima wagombea kwa sifa, maadili na uwezo wao, siyo kwa mapenzi binafsi, hofu au mahusiano ya karibu. Aidha, ameonya kuwa mtu ambaye hana uhusiano wa kweli na chama hawezi kusaidia, bali atakivuruga.
“Mcheza ngoma si yake lazima ataharibu… Ukicheza ngoma si yako utaharibu na utajulikana tu,” amesema kwa mafumbo ya kinadharia yaliyolenga kuhimiza uaminifu na ushirikiano wa kweli ndani ya chama.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuhuisha na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kabla ya mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025–2030.
Akizungumza jijini Dodoma leo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya CCM, Profesa Kitila Mkumbo amesema hatua hiyo inalenga kudumisha demokrasia, utawala bora na mshikamano wa kitaifa.
Amesema CCM inaamini kuwa misingi ya utawala wa sheria, haki za binadamu na demokrasia ni msingi muhimu kwa maendeleo endelevu ya Taifa, na kwamba chama hicho kitaielekeza serikali kuweka mfumo wa kisheria wa kutekeleza falsafa ya uongozi ya 4R.