Usasa unavyoleta janga la lishe duni vijijini

Kigoma. Michael Mbago (61) ni miongoni mwa wazee wanaoumizwa na ulegevu wa vijana wa sasa,  ikiwa ni matokeo ya kula vyakula ambavyo havina tija kwa afya zao.

Anasema miaka ya nyuma changamoto hiyo ilikuwa inaonekana zaidi mijini lakini kutokana na utandawazi siku hizi hata vijijini kuna kundi kubwa la watu ambao wana changamoto ya lishe.

Ni kwa sababu hiyo mzee huyu anasema vijana wengi kwa sasa wanashindwa kufanya kazi zinazohitaji nguvu na kuishia kupenda shughuli nyepesi na kutafuta njia za mkato kujiingizia kipato ikiwemo kubeti.

Akitolea mfano wa Mkoa wa Kigoma ambao ameishi kwa zaidi ya miaka 40,  anasema licha ya kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha vyakula vingi lakini kuna changamoto ya lishe.

Kulingana na takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),  tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni asilimia 27.1.

Mbago anasema kinachowasumbua watu wengi wa mkoa huo ni kukosa mpangilio sahihi wa makundi ya vyakula na kuiga ulaji unaoendana na tamaduni za kigeni na hilo linafanyika hadi kwa watoto hivyo kuathiri ukuaji wao.
Mzee huyu ni miongoni mwa wanachama wa timu ya marafiki wa elimu mkoani Kigoma wanaofanya ufuatiliaji wa uwajibikaji wa jamii katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).

“Hivi karibuni tumefanya ufuatiliaji wa mpango wa mpango wa lishe na elimu ya awali ya mtoto katika kata nne za Mwandiga,Bitale, Kagongo na Mungonya. Tulichobaini bado watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu suala zima la lishe na hasa mpangilio wa makundi ya vyakula.

“Utakuta mtu anakula mchana ugali halafu usiku wali, yeye mwenyewe anaona amebadilisha chakula lakini kwa uhalisia hapo ni sawa amekula kundi moja la chakula. Halafu huku utakuta mtu analima viazi anachukua vyote anaenda kuuza sokoni vile vilivyoharibika ndiyo anawaachia watoto wachemshe,”anasema

Mbali na hilo Mbago anasema changamoto nyingine iliyoletwa na utandawazi ni jamii kuiga tamaduni za kimagharibi hata kwenye ulaji hivyo kujikuta wakikosa virutubisho muhimu mwilini kwa kuishia kula vyakula vya kutengenezwa.

Anasema: “Huku vijijini unakuta mtu analima viazi au anafuga kuku wa mayai lakini hivyo vitu kwake kula ni adimu, ataenda kuuza iwe ni viazi au mayai halafu yeye akanunue mkate. Kuna namna tunaona kula vyakula kama chips, kuku wa kisasa ndiyo unaonekana una maisha halafu yule anayekula mboga za majani ana hali mbaya.

“Hapa kwetu kuna matunda mengi, yapo maparachichi, maembe, machungwa lakini mtu anaweza kuwa akaenda kuuza hayo matunda sokoni halafu akaenda kununua juisi ya viwandani, sasa jiulize kuna virutubisho gani anavipata mwilini kwa juisi iliyotengenezwa kiwandani na kuwekewa kemikali ili kuhifadhiwa,”.

Anasema kukabiliana na hilo kuna haja kubwa kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu lishe na umuhimu wake kwa watu wa rika zote tofauti na ilivyo sasa ambapo inaonekana mkazo kuwekwa zaidi kwa watoto.

Mbago ambaye anajishughulisha na uelimishaji wa jamii katika masuala ya elimu na lishe anasema elimu ya lishe inapaswa kutolewa na kueleweka kwa wanajamii wote ili wawe na uelewa wa makundi ya vyakula na mpangilio sahihi kwa ajili ya afya.

Ofisa lishe Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,  Sara Kibindu anaeleza kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya lishe na kutambua makundi ya vyakula lakini changamoto iliyopo ni kipato.

“Elimu wanayo ila inawezekana utekelezaji wake ukawa mgumu kwa sababu ya kipato, jamii nyingi huku ni maskini na mlo wao mkubwa ni ugali, sasa kuna kuwa na elimu na kumudu hayo mahitaji. Watalaamu tunapambana kutoa elimu lakini ndio hivyo hali ya uchumi ni tatizo.

Kingine ni watu kukubali kubadilika, kuna wale wanaopata elimu lakini wanaendelea kuishi kwa mazoea anakwambia mbona mabibi na mababu walikula hivyo na hawakupata madhara yoyote au unamwambia usimpe chakula mtoto kabla ya miezi sita wanasema mbona wao walilishwa,” anasema Sara na kuongeza.

Kigoma hatuna hali nzuri sana ya lishe kwa sababu bado tuna tatizo la udumavu, natamani watu wangekuwa wanaelewa na kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili tuitokemeze changamoto hii na wote tuzungumze lugha moja inapofika suala la lishe,”.

Ofisa afya huyo anaeleza kwa sasa nguvu kubwa inawekwa katika kuhakikisha wanafunzi katika shule zote za wilaya hiyo wanapata chakula shuleni angalau mlo mmoja.

Anasema kwa sasa asilimia 93 ya shule katika wilaya hiyo zinatoa chakula kwa wanafunzi ikiwa ni ushirikiano wa shule na wazazi.

“Tumeanza kupiga hatua angalau sasa wanafunzi wanapata mlo mmoja, siwezi kusema unatosha au tuko vizuri sana kwa sababu mlo huu kwa shule nyingine ni uji na kwingine inaweza kuwa ugali. Kwa tulikotoka hii ni hatua kubwa na imani yangu tutaendelea kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanaona umuhimu wa chakula kwa watoto wao na kisiwe chakula tu bali kiwe chakula chenye manufaa kwa lishe zao,”anasema Sara.
 

Lishe bora ina faida gani

Mtaalamu wa lishe, Elizabeth Geofrey anasema lishe bora huathiri moja kwa moja afya, ustawi wa mwili na akili, pamoja na uwezo wa kufanya kazi za kila siku.

Mtaalamu huyo anasema lishe bora husaidia kuzuia magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, upungufu wa damu, na aina mbalimbali za saratani.

Pia huimarisha kinga ya mwili hii ina maana kwamba virutubisho muhimu kama vitamini (kama C na D), madini (kama zinki na chuma), na protini huimarisha kinga ya mwili dhidi ya maradhi.

Anasema lishe bora pia ina mchango mkubwa katika ukuaji na maendeleo ya mwili hasa kwa kwa watoto na vijana, akisisitiza kuwa lishe yenye virutubisho kamili ni muhimu kwa ukuaji wa mifupa, misuli na maendeleo ya ubongo.

Mtaalamu huyo anabainisha kuwa lishe bora ina mchango mkubwa katika hali ya kisaikolojia; inaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo, mfadhaiko, na kuboresha kumbukumbu.

“Ndiyo maana tunasisitiza umuhimu wa kuzingatia lishe bora hasa kwa watoto kwa sababu ndiyo inayomsaidia kukua vyema, unaweza kukuta mtoto hana uwezo darasani ukahisi ana changamoto nyingine ila ukifuatilia utagundua hapati lishe sahihi

“Chakula sahihi huupa mwili nguvu za kufanya kazi, kujiendesha kimaumbile, na kuongeza ufanisi kazini au shuleni. Katika hili niweke msisitizo kwenye kula vyakula vya asili na halisi tuachane na vile vya kusindikwa, vya kukaangwa au vile vyenye sukari nyingi ili kupunguza uwezekano wa kujaza sumu mwilini,”anasema Elizabeth.

Related Posts