Dodoma. Wakati serikali ikiwekeza nguvu kwa vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo, baadhi ya vijana wamesema kuwa uwekezaji huo haujawafikia na kuwanufaisha.
Baadhi ya vijana wamesema bado wanahangaika kwenye shughuli zao za kila siku hasa za kuongeza thamani mazao ya kilimo kwa kukosa masoko ya bidhaa wanazozalisha, mitaji na elimu kutoka kwa maofisa ugani na masoko.
Vijana hao wametoa wito kwa serikali na sekta zote zinazojishughulisha na vijana kuyafikia makundi ya vijana na kuwapa mafunzo na fursa za masoko za bidhaa wanazozizalisha.
Esta Mtwale kutoka Mkoani Morogoro amesema kuwa pamoja na kujiunga kwenye vikundi na kufanya biashara ya kusindika mazao mba-limbali lakini uwezeshaji kutoka serikalini ni mdogo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 30, 2025 kwenye kongamano la kujadili vikwazo na viwezeshi vya kisera kwa vijana kushiriki kilimo biashara kwa mazao ya misitu lililoandaliwa Shirikisho la Vyama vya Wakulima Wadogo Tanzania (Shiwakuta) jijini Dodoma.
Esta amesema kikundi chao kinajishughulisha na usindikaji wa mazao mbalimbali kama vile mananasi, ndizi, utengenezaji wa siagi mbalimbali lakini mtaji wao walijitafutia wenyewe baada ya kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa.
“Msaada mkubwa tunaouhitaji kutoka serikalini ni fursa za masoko na elimu ya ujasiriamali hasa kwenye mazao ya kilimo ambayo sisi tunajishughulisha nayo kwenye mnyororo wa thamani. Kwa sababu hatupati ushirikiano wowote kutoka kwa maofisa ugani na maofisa masoko zaidi ya kujiendesha sisi wenyewe,” amesema.
Kwa upande wake mfugaji wa nyuki Joseph Kaisi kutoka mkoani Arusha amesema biashara ya nyuki na mazao yake imemfanya kukutana na watu wengi ambao wanafanyabiashara kama yake na hivyo kupata ujuzi kupitia watu hao.
Amesema wakati anatafuta shughuli ya kufanya kwa ajili ya kujiingizia kipato aligundua kuwa ufugaji wa nyuki pamoja na mazao yake ndiyo ingemfaa zaidi.
Amesema kinachotakiwa ni vijana kubadilisha mtazamo na fikra zao ku-husu shughuli za kilimo na badala yake wajishughulishe ili serikali iweze kuwasaidia kwa kile ambacho wameanza kukifanya.
Amesema biashara hiyo imemsaidia kujikimu na kuendesha maisha yake ya kila siku tofauti na siku za nyuma ambapo alikuwa hana shughuli za kufanya.
Amesema mtaji wa biashara hiyo aliupata kutoka kwa wadau wanaojishughulisha na kuwawezesha makundi ya vijana ambao wali-wapatia elimu ya ufugaji nyuki pamoja na mnyororo wa thamani wa mazao yanayotokana na nyuki
Naye Vaileth Noel amesema zipo fursa nyingi za vijana kwenye sekta ya kilimo ambapo kama watakuwa waaminifu watafanikiwa kwani serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuwawezesha vijana kwenye sekta hiyo kwa kuwawezesha mitaji na miundombinu ya kufanya shughuli za kilimo.
Amesema hivi sasa kila kijana kupitia halmashauri anayoishi ana fursa ya kupata shamba na kulima kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya muda mfupi ambayo yana soko na hivyo kujipatia kipato cha kutosha kupitia kilimo.
Mratibu wa programu ya Jenga kesho iliyo Bora (BBT), Florence Nda-bagoye amesema serikali imeweka mazingira mazuri kwa vijana kujishughulisha na kilimo kwa kuwapatia mashamba na kuwawekea mi-undombinu ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha muda mfupi na kujipa-tia kipato cha kutosha.
Amesema kundi la vijana ni kundi ambalo haliwezi kulima kilimo cha muda mrefu hivyo wamewazesha kulima mazao ya muda mfupi ambayo huwa wanayauza na kujipatia kipato kwa haraka kwa sababu hawawezi kusubiri kwa muda mrefu.
“Kwa kutumia programu ya BBT tumewawezesha vijana 812 ambapo kwa sasa wamebaki vijana 686 ambao wana umri kati ya miaka 18 hadi 40 bila kujali elimu yao na mahali wanapotoka kwa sababu tuliona changamoto kubwa ya vijana ni kwamba hawana mashamba hivyo serikali iliamua kuwamilikisha mashamba ambayo watalima kilimo cha umwagiliaji badala ya kusubiria msimu wa mvua,” amesema na kuongeza kuwa,
“Lakini pia Halmashauri zote sasa zimetenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana ambapo kama kuna kijana anahitaji kujishughulisha na kilimo anapewa shamba na sisi wizara yetu itakuwa ni kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba hayo ili kufanikisha azma ya vijana kujiajiri kwenye kilimo,” amesema.
Amesema ili kuleta tija kwenye sekta ya kilimo Wizara imeanzisha vituo atamizi 13 nchi nzima kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa vi-jana kwa nadharia na vitendo kwani programu ya BBT inachukua vijana wote ambao hawajasoma hadi wale wenye digrii.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shiwakuta, Elias Kaweya amesema changamoto kubwa inayowakabili vijana kuingia kwenye kili-mo ni kuwaona wazazi wao hawajafanikiwa kupitia kilimo.
Amesema kazi iliyopo hivi sasa ni kuwashawidhi vijana hao kujiajiri kwenye sekta ya kilimo kwa kuwapa elimu kuhusu kilimo biashara, mitaji na fursa zinazopatikana kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo ili wa-zitumie.
Amesema serikali imewekeza nguvu kubwa kwa vijana kwenye sekta ya kilimo ili kuwaonyesha kuwa wanaweza kufanikiwa kupitia kilimo kama watajizatiti na kulima kibiashara badala ya kulima kwa mazoea.
Naye Aneth Ngowi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya maeƱdeleo ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kutoka Wizara ya viwanda na bi-ashara amesema kupitia shirika la viwanda vidogo (Sido) vijana wengi wamepata mafunzo ya kusindika mazao yao na kuyaongezea thamani lakini pia kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali.
Amesema milango iko wazi kwa vijana ambao wanataka kufanya biasha-ra ya mazao kwa kufungua viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwani hivi sasa serikali inahamasisha uchumi wa viwanda kwenye sekta zote.