Dar es Salaam. Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi, amevitaka vyombo vya habari kuandika na kuripoti habari zinazofuatilia mienendo ya viongozi wa umma, ili wale wenye tabia zisizofaa waweze kujirekebisha.
Jaji Mwangesi ameyasema hayo leo, Ijumaa Mei 30, 2025, alipokuwa akifungua kikao kati ya Sekretarieti hiyo na wahariri wa vyombo vya habari, kilicholenga kujadili majukumu na mafanikio ya taasisi hiyo.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kusaidia kuimarisha maadili ya viongozi wa umma kupitia vipindi vya runinga, vikaragosi, picha, tahariri na makala mbalimbali.
Amesema hii itasaidia kuwahimiza viongozi kufuata Katiba na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kusaidia Sekretarieti hiyo kutekeleza wajibu wake kikamilifu.
“Vyombo vya habari vina taarifa nyingi ambazo mara nyingi sisi hatuwezi kuzipata bila msaada wao. Ushirikiano wenu utatusaidia kukuza uwajibikaji na kuimarisha uadilifu katika uongozi wa umma,” amesema Jaji Mwangesi.
Ameongeza kuwa Sekretarieti hiyo ina jukumu la kusikiliza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili, kupokea na kuhakiki matamko ya mali za viongozi, kufanya uchunguzi wa malalamiko hayo, pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu maadili ya viongozi.
Ametumia fursa hiyo kuwasihi wanahabari waandike habari nyingi zitakazohimiza uadilifu na maadili katika utumishi wa umma, akieleza kuwa ongezeko la maadili litachochea maendeleo na kuongeza imani ya wananchi kwa viongozi na serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Maadili katika Sekretarieti hiyo, Fabian Pokela, amewasilisha mada kuhusu maadili na kusisitiza kuwa uadilifu unapaswa kuzingatiwa sambamba na kufuata sheria na kanuni pekee.
Pokela aneeleza kuwa ufuatiliaji wa matamko ya mali za viongozi ni muhimu kwa kuongeza uwajibikaji, kudhibiti mgongano wa masilahi na kuhakikisha rasilimali za umma zinanufaisha umma.