Pemba. Licha ya wajasiriamali kisiwani hapa kupewa mafunzo ya kutengeneza bidhaa zenye ubora, wameiomba Serikali, kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), kuanzisha maabara maalumu ya kupimia malighafi kabla ya kuchakatwa.
Wamesema hatua hiyo itawapunguzia gharama za uzalishaji na kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye viwango vinavyokubalika sokoni.
Mjasiriamali wa kusindika sabuni, Bimkubwa Khamis akizungumza kuhusu ukosefu wa maabara za kupima malighafi kabla ya kutengeneza bidhaa zao kisiwani Pemba
Wajasirialimali hao wametoa kauli hiyo wakati wakizungumza na Mwananchi Mei 30, 2025 Gombani Pemba baada ya kupatiwa mafunzo juu ya utengenezaji wa baidhaa zenye ubora.
Wamesema baada ya kuingiza malighafi kutoka nje ya Pemba wamekuwa wakisarifu bidhaa zao na baadaye hupeleka katika taasisi ya viwango, lakini huambiwa biadhaa wanazozalisha hazina ubora.
Bimkubwa Khamis ni mjasiriamali wa sabuni kutoka Wete amesema mara nyingi wamekuwa wakiingia gharama katika kusarifu bidhaa wanazozalisha kwa kukosekana maabara maalumu ya kuchunguza malighafi kabla ya kuisarifu.
Amesema hawana utaalamu wa kubaini ubora wa malighafi, lakini watakapowekewa maabara maalumu ya malighafi kabla ya kuzisarifu wataepukana na gharama zisizozalazima.
“Tunaiomba Serikali ituwekee maabara maalumu sisi wajasiriamali ya kuchukunguza malighafi tunazonunua maana baada kutengeneza tunapeleka kwenye taasisi ya viwango, lakini tunaambiwa bidhaa tunazozalisha hazina viwango hatuwezi kujua kwa vile tumekosa chombo maalumu cha kuzichunguza,” amesema.
Mwingine Husina Khamis Hamad amesema changamoto hiyo inapaswa kuangaliwa kwa karibu kwa kujengewa kituo maalumu cha kuzifanyia uchunguzi malighafi wanazotumia.
Amesema hatua hiyo ya kuwepo kwa maabara kutawawezesha wajasiriamali katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora zitakazoweza kuuzika katika soko la ndani na nje ya Zanzibar.
“Tunaomba jambo hili liangaliwe kwa ukaribu, tunapata shida na kushindwa kuimarika kwa vikundi vyetu vya ushirika jambo litaloongeza uzalishaji na kukuza uchumi wetu,” amesema.
Akizungumza kuhusu kadhia hiyo, Mkurugenzi wa ZBS Pemba, Salum Said Salum amekiri changamoto hiyo wameshaibaini na tayari imeshawasilishwa Serikali kuu kwaajili ya kufanyiwa kazi.
“Ni kweli tatizo hili lipo na tunahakikisha tunalipa lipaumbele lifanyiwe kazi kwani kuweka kituo maalumu cha maabara ya kupima malighafi itasaidia kwa kiasi kikubwa wajasiriamali ili waondokane na usumbufu na gharama ambazo wamekuwa wakizipata,” amesema