Bunge lampa tuzo Rais Samia, ataja alivyopitia wakati mgumu

Dodoma. Bunge la Tanzania limemtunuku Rais Samia Suluhu Hassan tuzo maalumu ya heshima ya kutambua mchango wake kwa maendeleo ya Taifa.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwake leo Jumamosi Mei 31 na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kwa niaba ya wabunge, kwenye hafla iliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Rais Samia aliapishwa kushika wadhifa huo, Machi 19, 2021 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa tano, Hayati Dk John Magufuli, kilichotokea Machi 18, 2025.

Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inasema endapo Rais aliyeko madarakani atafariki dunia, Makamu wa Rais ataapishwa kushika wadhifa huo hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Akizungumza muda mfupi baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo yenye umbo la Siwa ya Bunge, Rais Samia ametaja mambo manne ambayo yalimpa wakati mgumu wakati wa kuanza majukumu yake mapya baada ya kukabidhiwa uongozi wa nchi.

“Kwanza ilikuwa ni ugonjwa wa corona (Uviko 19), pili nchi ilitoka kwenye kifo cha mpendwa wetu Rais (Magufuli), tatu hali ya siasa nchini na nne ni hali ya mtikisiko wa uchumi kutokana na ugonjwa wa Covid 19,” amesema Rais Samia.

“Alitakalo Mola huwa, na Mungu akikupa ulemavu atakupa na njia ya kutokea, nami namshukuru Mungu imekuwa hivyo,” amesema Rais Samia.

Amesema kutokana na hali hiyo, kulikuwa na minong’ono na mashaka iwapo angeweza  kuhimili nafasi hiyo.

Hata hivyo, amesema uwepo wake katika Bunge la 10 pamoja na Bunge la Katiba mwaka 2014 vilimuimarisha kwa kiasi kikubwa hadi hatua aliyofikia sasa.

Amesema kazi hiyo aliiweza kutokana na ushirikiano mkubwa ambao amekuwa akiupata kutoka kwa viongozi wa chini yake, vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama.

“Nilimwomba Mungu anisaidie na kuniongoza kama alivyomwongoza Suleiman na manabii wengine, nchi inahitaji mambo mengi na wakati huo hujui unapata wapi madawa ya kutibu watu, lakini alinisikia na leo nafurahi kuwa hata Bunge ambalo ni chombo cha wananchi mmetambua mchango wetu,” amesema Rais Samia.

Kabla ya kumkabidhi tuzo hiyo, Spika Ackson ameeleza sababu za Bunge kufikia uamuzi wa kumtunuku tuzo hiyo ya heshima na maalumu, kuwa ni namna alivyofanya mageuzi makubwa katika Taifa ikiwemo matumizi mazuri ya falsafa za 4R.

Spika Ackson amesema nchi imepata mafanikio, utulivu na amani, huku sekta mbalimbali zikionyesha kukuza uchumi wake.

“Katika kipindi chako tumeshuhudia uwepo wa utawala bora, uaminifu, uwajibikaji na uwakilishi mzuri lakini kumekuwa na uwazi na usawa unaozingatia ustawi na maendeleo ya nchi,” amesema Dk Tulia.

Ametaja mchango mwingine kuwa ni namna alivyotumia muda mfupi katika utatuzi wa kero 15 za Muungano, hali iliyosaidia kupungua kwa malalamiko ya wananchi wa pande hizo mbili na vilio vya wafanyabiashara.

Katika hatua nyingine, Dk Tulia amesema mafanikio mengine yamechangiwa na uhusiano mwema na mataifa mengine.

Amesema hilo limewasaidi Watanzania kuendelea kung’ara na kuchaguliwa kimataifa, akiwamo yeye (Dk Ackson) ambeye alichaguliwa Rais wa Mabunge Duniani na Profesa Mohamed Janabi aliyechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Related Posts