Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema kuwa nafasi za uongozi ambazo viongozi mbalimbali wa Tanzania wamepata katika taasisi za kimataifa si matokeo ya juhudi zao binafsi bali ni juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameimarisha mahusiano ya kidiplomasia kwa kiwango kikubwa.
Dk Tulia amesema: “Mheshimiwa Rais, umeendelea kukuza diplomasia kwa kushiriki mikutano mbalimbali ya kimataifa ambayo imeliletea tija kubwa Taifa letu, ikiwa ni pamoja na Tanzania kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Amani Barani Afrika.”
Akizungumzia Watanzania kuchaguliwa kuongoza taasisi mbalimbali za kimataifa, Dk Tulia amesema “Umewezesha Watanzania wengi kupata nafasi za uongozi katika taasisi za kikanda na kimataifa. Aidha, hata mimi niliyesimama mbele yako pamoja na kuwa Spika lakini ni Rais wa Mabunge Duniani. Kama tunavyotambua kuhusu wengine, nafasi hizi si kwa juhudi zao bali ni kwa juhudi zako. Vivyo hivyo, nafasi yangu ya Urais wa Mabunge Duniani isingewezekana bila juhudi zako.”
Akitaja baadhi ya viongozi waliopata nafasi kwenye mashirika na taasisi za kimataifa, Dk Tulia ametaja akina Benjamini Kapela, Profesa Mohamed Janabi, Dk Deo Mapinga na Balozi Profesa Kennedy Gastorn.
Hayo yamesemwa leo kwenye hafla ya Bunge kumpa Rais Samia Suluhu Hassan tuzo maalumu ya heshima inayofanyika katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma leo Mei 31, 2025.