Moshi. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, amesema uamuzi wake wa kumuunga mkono Tundu Lissu aliyeshinda uenyekiti wa chama hicho, katika uchaguzi mkuu wa ndani uliofanyika Januari 21, 2025, ulikuwa wa Kimungu na baraka.
Amesema licha ya kutoka eneo moja (Machame-Hai) na Freeman Mbowe, lakini katika demokrasia aliamiani kwa Lissu, akisema uamuzi huo umekuwa na baraka zaidi kuliko wakati wowote katika safari yake ya maisha yake kisiasa.
Lema aliyasema hayo jana Ijumaa Mei 30, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Manyema, wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni mwendelezo wa kunadi ajenda ya ‘No reforms no election’.
Ajenda ya ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ ina lengo la kushinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa chaguzi ili kuwepo kwa uwanja sawa wa demokrasia kwa vyama vyote vya siasa.
Katika mkutano huo, Lema alisema, “Mimi ni Mmachame na Mbowe Mmachame, lakini kwa Lissu, sioni aibu kusema mbele ya Mungu nimefanya uamuzi wa Kimungu.”
Amesema anafahamu tabia za watu wa nyumbani kwao, anaposimamia ukweli na haki haogopi jambo lolote kwa mtu yeyote hata awe na cheo chochote.
“Kwa sababu nilipowaita watu kwenye maandamano mbele yao niliwaambia tutapigania haki,” amesema Lema.
Kwa mujibu wa Lema ambaye ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, ndoto ya Chadema si Lissu kuwa Rais wa nchi, bali kuhakikisha nchi inakuwa na uhuru, haki, ustawi na utu kwa kila Mtanzania
“Chama chochote cha siasa cha mageuzi, kitu cha kwanza kinachopigania kabla ya kuingia madarakani ni mabadiliko ya fikra, tutapigania haki ya watu wa nchi hii, si kwa sababu ya fedha bali tunahitaji kuwa na mabadiliko,”amesema Lema.
Mbali na hilo, Lema amewataka wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na ukanda wa Kaskazini kuendelea kulinda heshima yao kwa kuwa ndio waasisi wa siasa za mageuzi katika nchini.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob ‘Boni Yai’ amesema wanatambua mchango wa mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Mbowe, akimtaka kutokaa kando kwa kuwa bado wanamhitaji.
Boni Yai amesema mchango wa Mbowe ndani ya Chadema ni mkubwa na wana kila sababu ya kujivunia utumishi wake na hapaswi kuwa mnyonge.
“Sisi wazee wakishashuka wanakaa pembeni, wamemaliza dhumuni lao, wajibu wetu kama chama ni kuwatumia kwa ushauri, wasuluhishi kwenye migogoro ya chama, lakini pia kuwalinda na kuwaheshimu,”amesema Boni Yai.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesema kila Mtanzania anashiriki kuijenga nchi kutokana na nafasi aliyopo, hivyo chama hicho kikishika dola kitahakikisha kila mtu anakuwa na bima ya afya.
“Siyo watu wa Serikali pekee wanajenga nchi hii, kila mmoja wetu anaijenga nchi hii kwa namna moja au nyingine. Chadema tutabadilisha nchi hii, tunahitaji tusimamie rasilimali zetu ili kila mwananchi aishie vizuri,”amesema. Heche.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Sharifa Suleiman amewataka wananchi wa Moshi, kuiunga mkono ‘No reforms, no election’ ili kuleta mabadiliko nchini.
“Hii ndiyo Moshi ninayoijua mimi, Moshi ya watu wenye kujielewa, wenye msimamo, watu wazalendo katika eneo lao na ninafahamu ninyi hamuhitaji muelekezwe nini cha kufanya.
“Ninyi ni watu wa mabadiliko, Sasa tuungeni mkono matokeo yake mtayaona baada ya kupatikana mabadiliko ya sheria mbalimbali za uchaguzi,”amesema Suleiman.