Nini hatima ya siasa kwa Askofu Gwajima?

Moshi/Dar. Kuna usemi “A King’s word is law” ikimaanisha neno la mfalme ni sheria na hili linaakisi kile ambacho kinatarajiwa kumkuta Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, baada ya kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusiana mchujo wa wagombea 2025.

Rais Samia wakati akifunga mkutano mkuu maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Dodoma Ijumaa ya Mei 31, 2025 hakumtaja kwa jina lake halisi.

Akifunga mkutano huo, Rais Samia alisema mwaka huu ni wa uchaguzi, “Tunapokwenda huko kwa sababu kuna kugombea nafasi, awali huwa tuna makundi makundi, tutakapomaliza kugombea turudi chama kiwe kimoja.”

“Niwaombe au sijui niagize vikao vinavyokwenda kuchuja watu, vinavyokwenda kuchuja wagombea wakatende haki. Anayefaa aambiwe anafaa na asiyefaa aambiwe ana kasoro moja, mbili tatu hatufai kwa huko mbele tunapokwenda.”

“Tukitoa mwanya ndugu zangu, tukipitisha wanaotafuta tu na mie niwemo, ndio tunapata wale wanaokwenda huko. Chama kinakuwa Gwajimanised. Kwa hiyo kwa vyovyote vile tusi Gwajimanised chama chetu, Magwajima tuyaache nje.”

“Hakuna kuoneana aibu wala haya,” alisisitiza Rais Samia ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambayo ndio ya juu ndani ya chama tawala na kutolea mfano wa mtu mmoja aliyekuwa mwimbaji huko Zanzibar kukoleza kauli yake.

Rais Samia alisema mwimbaji huyo alipata kuimba kuwa mcheza ngoma si yake lazima ataharibu, atasema hawi sawa na wenzake, yeye anakuwa Majudhubu.

“Majudhubu ni mtu ambaye hazimo hazimo hivi. Kwa hiyo ukicheza ngoma si yako lazima utaharibu tu, utasema miye siye jamani na ndiyo haya yanayotokea,” alisisitiza Rais Samia bila kueleza ni mambo gani hasa yametoke ndani ya CCM.

Hata hivyo, leo Jumamosi Mei 31, 2025, Mwananchi imezungumza na baadhi ya wachambuzi wa siasa kuhusiana na hicho kinachoendelea hususan mustakabali wa kisiasa wa Askofu Gwajima baada ya kauli ya Rais Samia aliyoitoa jana.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi amesema; “Gwajima ndio basi kisiasa, sioni akitoboa tena. Maana siasa za nchi hii lazima uwe ndani ya chama. Sasa kama chama tawala kinakukataa na kwa asili ya siasa za Gwajima,  hawezi kuhamia vyama vya upinzani.

“Mimi si mkazi wa Kawe, lakini mwaka 2020 Gwajima aliahidi ahadi nyingi ambazo hajazitekeleza hadi sasa. Hawezi kwenda upinzani, hata akienda kupata nafasi ya kupeperusha bendera ya ubunge kwa chama hatakaenda,”amesema Dk Mushi.

Amesema Askofu Gwajima akitoka CCM hawezi kufanikiwa kwa sababu hawezi kujisimamia mwenyewe.

“Kila mmoja anafahamu alipataje ubunge wake pale Kawe, kwa hiyo sidhani,” amesema Dk Mushi.

Naye mchambuzi wa siasa, Deus Kibamba ametofautiana Dk Mushi akisema Askofu Gwajima ataendelea kupeta hata ikitokea akaondoka CCM.

Kibamba amesema kwa sababu siasa za Gwajima ni za kipekee sio za kila kitu kusema ndio kama ulivyo utaratibu wa chama tawala, ni wazi anaweza kuendelea na siasa zake hata nje ya Chama cha Mapinduzi au vya upinzani.

“Atarudi alikokuwa na huenda akawa mwiba, watu wasubiri kumuona, siasa zake ni tofauti ni za mapambano zaidi. Nafikiria Gwajima ataendelea kuwa Gwajima kwa kufanya siasa zisizo za vyama, hajawahi au kusema yupo upinzani.”

“Namuona Askofu Gwajima anarudi kufanya siasa za kujitegemea, lakini siasa za kugombea jimbo zitakuwa mwisho kwake, sidhani kama atapenya ndani ya CCM, sioni akiteuliwa kama ataomba… na sidhani kama atakwenda, tutarajie kumuona Gwajima sasa,”amesema Kibamba.

Ikumbukwe Askofu Gwajima hakuwa ameongoza kura za maoni CCM 2020, lakini alirudishwa kugombea ubunge jimbo la Kawe na msumeno huo huo ndio unaoweza kutumika kwake akishinda kura za maoni ili “Magwajima yabaki nje”.

Itakumbukwa hivi karibuni wakizungumza kwenye Bunge la Bajeti linaloendelea, baadhi ya wabunge ‘walimshambulia’ kutokana na kauli yake kuvisema vyombo vya dola na anayeteua wakuu wake.

Gwajima alionekana kwenye picha mjongeo iliyoambaa kwenye mitandao ya kijamii  akizungumzia kushamiri kwa matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji, lakini alisema kuna magenge ambayo anaamini yanafanya hivyoili  kulinda maslahi ya kisiasa ya anayewatuma.

Tamko hilo la Gwajima, ziliibua mjadala kwa baadhi ya wabunge wanaotokana na CCM akiwamo wa Kinondoni, Abbas Tarimba aliyeenda mbali na kukitaka CCM kumchukulia hatua Askofu Gwajima kupitia kamati ya maadili.

Talimba alisema; “Hivi huyu mtu bado ana kadi ya chama chetu? Kwa nini awe huru kuendelea kutoa maneno ya fedheha kwa Rais wetu. Anatoa mifano ya kutisha ya kumkosea heshima Rais na familia yake.”

Naye Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku maarufu Musukuma alisema wanasiasa nchini hawapaswi kuingilia uamuzi wa Rais Samia huku akimtaja Askofu Gwajima kuingilia uamuzi wa Rais Samia kwa kutumia upole wake huko ni kuvuka mipaka na kuingilia mamlaka na akaliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wote wanaoingilia mamlaka.

Mbali ya wabunge, pia makada wa CCM kwenye Jimbo la Kawe na maeneo mengine nchini, pia  walijitokeza wakitaka ashughulikiwe.

(Nyongeza na Bakari Kiango)

Related Posts