Polisi yasisitiza matumizi sahihi ya bunduki

Serengeti. Askari wote nchini hasa wanaokaa na bunduki wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya silaha hizo ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea ikiwa  pamoja na mauaji ya binadamu kwa kutumia bunduki hizo kinyume cha utaratibu.

Maagizo hayo yametolewa wilayani Serengeti leo Jumamosi Mei 31 2025 na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Lazaro Mambosasa wakati akifunga mafunzo ya awali kwa walinzi wa Kampuni utalii ya Grumeti Reserves.

Mambosasa amesema matumizi sahihi ya silaha ni pamoja na kupunguza nguvu ya adui ili aweze kukamatwa na kufikishwa kwenye mamlaka husika kwa hatua zingine na sio kuuwa adui kwa maelezo kuwa mwenye jukumu na mamlaka ya kuuwa ni Mwenyezi Mungu pekee.

“Ni lazima askari anayekaa na bunduki ajue matumizi sahihi ya silaha hii, kazi ya bunduki sio kuuwa  kazi yake ni kukurahisishia wewe askari kuweza kufanikisha ukamataji wa adui au muhalifu na mkumbuke kuwa katika matumizi hayo ya kupunguza nguvu ya adui kuna namna ya kupiga risasi na maeneo ya kupiga sio unajipigia tu,” amesema

Amesema askari wanapokuwa kwenye lindo wanatakiwa kuwa makini muda wote ili eneo liwe salama badala ya kubweteka na kutoa nafasi kwa adui kuvamia hatua ambayo wakati mwingine inasababisha matumizi makubwa ya silaha hali ambayo kwa namna moja ama nyingine inasababisha bunduki kutumika kinyume cha utaratibu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Grumeti Reserves,  Martha Baare amesema zaidi ya walinzi 80 wa kampuni hiyo wamepatiwa mafunzo ya awali ya ulinzi huku lengo likiwa ni kuboresha utendaji wao wa kazi.

Amesema kampuni imeamua kutoa mafunzo hayo kutokana na uhitaji uliopo kwani licha ya walinzi hao kuwepo kazini kwa muda mrefu lakini wengi wao hawakuwa na mafunzo yoyote ya awali ya ulinzi.

“Kampuni ina watumishi zaidi ya 1,000 na asilimia 65 ya watumishi ni wale wanaotoka katika jamii inayotuzunguka, hapa kuna watu ambao wamechukuliwa na kampuni huku wakiwa hawana hata vyeti vya darasa la saba hivyo tuliona ipo haja ya kuwapa fursa za ajira na kuwapa mafunzo ya awali ya ulinzi ili waweze kuwa na sifa,” amesema Baare.

Amesema pamoja na mambo mengine kampuni hiyo ina jukumu la kuwajengea watanzania uwezo wa kufanya kazi na kunufaika na fursa zinazowazunguka licha ya wengine kutokuwa na elimu na sifa za kufanya kazi hizo hapo awali.

“Ingawa tumetoa fursa za ajira kwa  jamii lakini pia ilikuwa ni hatari kwetu kwani hawa walinzi hawakuwa hata na mafunzo ya awali ya ulinzi hivyo ingetokea changamoto yoyote ni vigumu kuwajibishana, tukaja na wazo hili la kuandaa mafunzo kwa walinzi ili waweze kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,” amesema.

Mkuu wa Idara ya Usalama kutoka Grumeti Reserves, John Senteu amesema mafunzo hayo yametolewa kwa muda wa siku 14  na kampuni hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ambapo wanaamini kuwa baada ya mafunzo hayo walinzi hao watafanya kazi kwa ufanisi.

“Kutokana na wengine kutokuwa na mafunzo ya awali ya ulinzi wapo wengine waliokuwa wakishindwa kufikia ule ufanisi tuliotaka hivyo mafunzo yatasaidia kujenga uelewa wa pamoja na kufanya kazi katika misingi ya kitaaluma,” amesema.

Senteu amesema pamoja na mambo mengine mafunzo hayo yalihusu silaha na usalama wa askari, mbinu za kuzuia uhalifu, usimamizi wa malindo na doria, saikolojia na msongo wa mawazo, ushirikishwaji wa jamii na huduma bora kwa wateja, upekuzi na ukamataji wa wahalifu pamoja na masuala jinsia na ulinzi wa watoto.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wamesema hivi sasa utendaji wao wa kazi utaimarika zaidi kwani awali wengi wao walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

“Sasa hivi nitafanya kazi kwa weledi tofauti na mwanzo ambapo nilikuwa nafanya kwa mazoea hivyo kusababisha kushindwa kupata ule ufanisi uliotakiwa,” amesema Paulina Musa.

Hamidu Dala amesema kupitia mafunzo hayo wameweza kufahamu dhana nzima ya intelijensia ambapo awali walikuwa wanafikiri kuwa suala zima la intelijensia  linawahusu watu maalumu.

Related Posts