Unguja. Sensa ya miti Zanzibar, inaonyesha misitu ya mikoko imepungua ujazo wake kutoka mita za ujazo 41 hadi mita za ujazo 18.9 kwa upande wa Unguja na Pemba kutoka mita za ujazo 39.8 hadi mita za ujazo 38.3.
Ripoti hiyo inaonyesha ukataji na upoteaji wa misitu Zanzibar upo kwa wastani wa asilimia 1.2 ya kiwango cha misitu kilichopo, sawa na hekta 1,277 kwa mwaka.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis amesema hivi karibuni barazani kwamba upungufu huo unatokana na shughuli za kibinadamu, kama ukataji wa miti kwa ujenzi, nishati ya kupikia, shughuli za maendeleo na mabadilko ya tabianchi.
Wakati ripoti ikionyesha hivyo, zaidi ya mikoko 2,000 imekatwa kutokana na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa mbili kati ya Unguja Ukuu na Uzi na Ng’ambwa Mkoa wa Kusini Unguja, unaoendelea.
Hata hivyo Serikali imesema itahakikisha miti yote iliyokatwa inapandwa kwa kushirikiana na jamii husika, si tu eneo hilo pekee bali katika maeneo mengine kisiwani humo.
“Katika kipindi cha miaka 16, kuanzia 1997 hadi 2013, misitu ya mikoko imepungua ujazo wake kutoka mita za ujazo 41 hadi mita za ujazo 18.9 kwa upande wa Unguja na kwa upande wa Pemba imepungua kutoka mita za ujazo 39.8 hadi mita za ujazo 38.3,” hii ni kutokana na shughuli za binadamu na kukata miti.
Utafiti huo wa sensa ya misitu uliofanywa na Wizara Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, kupitia Idara ya misitu, mwaka 2013 na kubaini kuwa Zanzibar ina eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta 37,801.38 kati ya hiyo Unguja hekta 22,137.38 na Pemba hekta 14,970 ikiwemo misitu ya kawaida na mikoko.
Maeneo ya miti ya mchanganyiko (agroforestry) yamepungua kwa hekta 20,649 kwa Unguja na hekta 14,338 kwa Pemba.
Wanawake vinara urejesha uoto
Licha ya uharibifu huo, jithada zimeanza kufanyika kurejesha uto wa asili huku wanawake wakiwa mstari wa mbele kushiriki katika upandaji wa miti.
Hatua hiyo, inaelezwa si tu itasaidia kurejesha misitu, bali itaongeza vipato vya na kujenga uchumi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, wamesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kukosa nishati mbadala, hivyo kutumia misitu kwa ajili ya shughuli zao.
“Kwa huku pembezoni bado tuna changamoto kubwa ya nishati kwa hiyo unakuta wananchi wengi wanatumia kuni na ili kutumia kuni lazima ukate misitu kupata nishati hiyo,” amesema Asha Abdalla mkazi.
Ripoti ya hali ya mazingira Zanzibar ya mwaka 2021 inaonyesha kuwepo kwa utegemezi mkubwa wa misitu kwa ajili ya nishati ya kupikia, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa vijijini wanategemea kuni kwa ajili hiyo. Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa ukataji wa miti.
Fatma Said Abdala, mkazi wa Unguja amesema kutokana na elimu wanayopata kupitia wadau wa mazingira, wameanza kutambua umuhimu wa uhifadhi wa misitu, hasa kwa kupanda mikoko ili kurejesha mazingira katika hali yake. “Wakati mwingine huwezi kuona umuhimu wake lakini ukishapata elimu ndiyo unakuja kutambua madhara na hasara zake. Kwa sasa tunajikita katika kuotesha miti ya mikoko na kutoa elimu kwa wananchi wenzetu katika utunzaji wa misitu,” amesema.
Mwanamke mwingine, Hajra Hassan Haji, amesema licha ya kwamba si kazi rahisi—kuna wanaowaona kama wanapoteza muda katika kushughulikia miti—lakini manufaa yake ni makubwa.
AmeiombaS kuongeza jitihada katika kutoa elimu na kusambaza miti hiyo ili kuokoa Zanzibar dhidi ya athari zitokanazo na ukataji wa miti.
“Bado jamii inahitaji elimu kubwa kuhusu jambo hili kwa sababu wapo wanaoona ni jambo la kawaida, lakini wengine hawajashtuka,” amesema.
Ameongeza kuwa ipo haja ya kuwashirikisha wananchi katika hatua zote za mchakato huo, ili waelewe madhara ya kukata miti, kwa kuwa rasilimali za asili ndizo tegemeo la wananchi wengi, hasa wale wenye kipato cha chini.
Mchango asasi za mazingira
Asasi za kiraia zinazofanya kazi za uhifadhi wa mazingira zinatajwa kushiriki kikamilifu na kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mijini na vijijini.
Idadi ya asasi hizi imeongezeka kutoka 25 mwaka 2016 hadi 60 mwaka 2021 kwa upande wa Unguja na Pemba. Ripoti ya mazingira inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2016 hadi 2021, wastani wa hekta 233.5 za mikoko zimepandwa na zinatunzwa na asasi hizo katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Ofisa wa Teknolojia ya Uzalishaji wa mradi wa Zanzibar Women Leadership in Adaptation (ZanzAdapt), Shaaban Peter, amesema kupitia mradi huo wanatarajia kuwafikia wakulima 4,000 ambapo asilimia 80 ni wanawake.
Mbali na kufundishwa kilimo mseto, wanapewa pia mafunzo ya kuotesha miti ya mikoko kwa ajili ya kurejesha misitu. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Shirika la Kimataifa la Misitu (CFI), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa Zanzibar na Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP), kupitia ufadhili wa Global Affairs Canada.
“Tunalenga wanawake kwa sababu wengi wao ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Lakini wakielimika na kuelewa namna ya kukabiliana na changamoto hizi, si tu watapanda miti, bali pia wataongeza vipato vyao,” amesema.
Sabrina Haji, mkulima kutoka Kijiji cha Bungi, amesema baada ya kupata elimu, ameunda kikundi cha kuotesha miti ya matunda na mikoko. Miti mingine huipanda mwenyewe na mingine huuza kwa ajili ya kulinda mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar, Dk Mzuri Issa, amesema kwa sasa wanawake wana fursa sawa kushiriki katika maendeleo ya taifa, tofauti na zamani ambapo walikuwa wakichukuliwa kama watu wa kukaa nyumbani na kulea familia.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika fursa zinazopatikana, kwani mbali na kusaidia maendeleo ya taifa, husaidia pia kuongeza vipato vyao na kuondokana na utegemezi.
Mjumbe wa Shehia ya Unguja Ukuu, Ali Hamadi Ali, ameziomba taasisi husika kuwapa ushirikiano, vitendea kazi na elimu ya ulinzi ili kudhibiti ukataji wa mikoko kwa masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
“Ili wananchi waachane na ajira ya ukataji wa mikoko, ni muhimu waelimishwe kuhusu athari zake kwani mikoko ndiyo huchukua hewa chafu inayosababisha ongezeko la joto katika mazingira yetu,” amesema.