Vifo vya wajawazito na watoto vyapungua Pwani

Kibaha. Jitihada za wauguzi katika Mkoa wa Pwani zimezaa matunda katika kuboresha huduma za afya, baada ya kufanikisha kupungua kwa vifo vya wajawazito na watoto wachanga kati ya mwaka 2017 hadi 2024.

Taarifa hiyo imesomwa leo Mei 31, 2025, mjini Kibaha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani. Taarifa hiyo inaonesha kuwa mafanikio hayo yametokana na mshikamano, juhudi, na weledi wa wauguzi kwa kushirikiana na watumishi wengine wa sekta ya afya.

Akisoma taarifa hiyo, Katibu wa Chama cha Wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, Mohamed Mvunge, alisema vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 60 mwaka 2017 hadi kufikia 35 mwaka 2024. Aidha, vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 608 hadi 318 katika kipindi hicho, sawa na jumla ya vifo 675 vilivyoepushwa.

“Tumeweza kufikia mafanikio haya kupitia kampeni za chanjo, elimu ya uzazi wa mpango, ufuatiliaji wa karibu wa wajawazito, pamoja na utoaji wa huduma za dharura kwa mama na mtoto. Wauguzi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha uzazi salama na huduma bora zinapatikana kwa jamii,” alisema Mvunge.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zimeambatana na kuimarishwa kwa elimu ya afya kwa umma, kufuatilia maendeleo ya wajawazito kuanzia kliniki hadi kujifungua, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na dawa muhimu kwa wakati.

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Pwani wameitaka kada hiyo kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma yao, wakieleza kuwa bado kuna changamoto za lugha isiyofaa na ukosefu wa staha kutoka kwa baadhi ya wauguzi.

“Tunawashukuru wauguzi kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini tunawaomba wajirekebishe, hasa wale wachache wanaokiuka maadili. Tunahitaji huduma zenye huruma na heshima, kwani mgonjwa anahitaji faraja zaidi ya tiba tu,” amesema Mariam Juma, mkazi wa Kibaha.

Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani hufanyika kila mwaka Mei 12. Hata hivyo, kwa Mkoa wa Pwani, maadhimisho hayo yamefanyika leo, Mei 31, ili kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali wa sekta ya afya kushiriki kwa kina na kutoa michango yao katika kuinua huduma za uuguzi.

Related Posts