Dar es Saalam. Wakati wananchi waliopisha mradi wa Bonde la Msimbazi wakitishia kwenda mahakamani wakidai kutolipwa fidia ya ardhi kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, Serikali imesema wanaostahili malipo ni wale waliokuwa na hati pekee.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), umefafanua suala hilo, ukisema mchakato wa kuwalipa fidia wale tu walio na hati za makazi, umekwishaanza na umefikia pazuri.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inatekeleza mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi kwa lengo la kukabiliana na mafuriko na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo la chini la bonde, suala ambalo litaiwezesha Serikali kuingiza zaidi ya Sh2 trilioni.
Hata hivyo, ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo unaosimamiwa na Tarura, Serikali ilifanya mchakato wa kuzihamisha kaya zaidi ya 2,000 katika eneo la mradi kwa kulipa fidia ya mali zinazoathirika. Mpaka sasa kaya 2,184 zimeshalipwa kati ya 2,212 zinazostahili kulipwa.
Aidha, katika mchakato huo, Serikali iliamua kuwalipa fidia ya ardhi Sh4 milioni kama kifuta jasho ambacho awali hakikuwepo zaidi ya kutakiwa kulipwa ya majengo tu, hali iliyoibua malalamiko.
Sababu za kufanywa hivyo kwa mujibu wa Tarura, ni kutokana na ardhi hiyo kuwa owevu ambayo si salama kwa makazi na kisheria na hivyo haipaswi kulipwa fidia.
Hata hivyo, uamuzi huo ulibatilishwa baadaye na na Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa alipokutana na wananchi hao Novemba 15, 2023 katika viwanja vya Jangwani kujibu ya malalamiko yao.
Mchengerwa aliagiza wananchi wote wa bonde hilo walipwe Sh4 milioni kila mmoja kama kifuta jasho.
“Tulisikia malalamiko yenu kupitia nyie wenyewe, viongozi wenu akiwamo mkuu wa mkoa, madiwani na wabunge, nami nikalifikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kwa kuwapenda, jana ameridhia kila mwananchi anayepisha mradi huu alipwe Sh4 milioni kama kifuta jasho kwa ardhi aliyoimiliki.
Akizungumza katika ofisi za Mwananchi zilizopo Tabata Relini jana Jumamosi, Mei 30, 2025, mwakilishi wa waathirika wa mradi huo, Godwin Cathbert amesema hawakuridhishwa na hatua hizo na Desemba 20, 2024 waliiandikia Tamisemi lakini mpaka sasa hawajapata majibu.
Amesema hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake, anabainisha kuna fedha ambazo Tarura ilipaswa kuzilipa kama fidia kwa waathirika kutokana na miradi yake ukiwamo huo wa Bonde la Msimbazi, lakini haijafanya hivyo.
Katika ripoti hiyo, CAG amebaini miradi saba ilikuwa na malimbikizo ya fidia zinazodaiwa jumla ya Sh24.75 bilioni, ikihusisha waathirika 1,879, wakiwemo wa Bonde la Msimbazi.
Ripoti hiyo inasema changamoto za kutolipa fidia, zinaathiri uhusiano na jamii. Pia, zinaweza kuhatarisha maendeleo endelevu ya miradi kwa siku zijazo, achilia mbali kuongeza gharama ya fidia kutokana na mabadiliko ya kiuchumi.
Kutokana na hilo, Cathbert amesema; “Tunapenda kuomba Ofisi ya CAG ishirikiane nasi kuona tunafikia mustakabali mwema, la sivyo tutakwenda mahakamani kudai haki yetu hii.”
Mwakilishi huyo amesema malalamiko ya madai yao yanasimamia muongozo wa uthamini wa fidia kifungu namba 11(1) cha Sheria ya Uchukuaji Ardhi, kinachosema kuwa pale itakapochukuliwa, Serikali inawajibika kulipa fidia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Walalamikaji Mradi wa bonde la Msimbazi Charles Swai akizungumza katika mkutano na wananchi.
“Aidha kifungu namba 3(1)(9) cha Sheria ya Ardhi (sura 113) kinaelekeza fidia hiyo ni lazima iwe kikamilifu na ya haki na ilipwe kwa wakati.
“Kwa bahati mbaya sana, sisi wakazi tunaolalamika kulipwa fidia ya ardhi, baada ya kupitia muongozo wa uthamini wa fidia hakuna mahali tunaona tumetendewa kama ambavyo muongozo umeelekeza,” amesema.
Kauli hiyo imeungwa mkoni na baadhi ya wananchi waliolipwa fidia akiwamo, Juliana Mtui, ambaye pia amesema wamepunjwa.
Mtui amesema licha ya kuwa na hati ya nyumba katika eneo hilo, amelipwa Sh4 milioni huku akihoji kama fedha hizo zipo, kwa nini wasipewe.
Mwathirika mwingine amesema si tu ardhi ililipwa fidia isiyolingana, bali hata nyumba yake ambayo ilikadiriwa kulipwa Sh550 milioni, amelipwa Sh52 milioni pekee.
Hali hiyo, amesema imesababisha ashindwe kumalizia ujenzi wa nyumba mpya Kibaha, Mkoa wa Pwani alipohamia, na kuwa sasa anaishi kwenye pagale alilojijenga kwa shida.
Naye Anaseta Kibala amesema kutokana na fidia ndogo aliyopewa, amelazimika kurejea kuishi nyumbani kwa wazazi wake mkoani Morogoro.
“Kwenye makazi, nilipaswa kulipwa kati ya Sh400 hadi Sh500 milioni, lakini nimelipwa Sh45 milioni tu kwa nyumba iliyokuwa na vyumba sita. Hapa nilipo mimi ni mjane, nina watoto wanne ambao ada zao zilitegemea vyumba nilivyokuwa nikipangisha kule Jangwani,” amesema.
Pia amesema kutokana na malipo aliyopokea, ameshindwa kumalizia nyumba aliyohamia Chalambe, Dar es Salaam na ameamua kuishi kwa wazazi wake mkoani Morogoro.
“Nitafurahi sana kama Serikali itatupatia nyongeza ili tukamilishe ujenzi wa nyumba zetu, kwani hakuna kitu kinaumiza kama kuzoea kuwa na kwako halafu unaishia kuomba hifadhi kwa watu wengine,” amesema Anaseta.
Tarura yawajibu
Akizungumzia madai hayo, Ofisa Habari Mwandamizi wa mradi huo kutoka Tarura, Raphael Kalapilo amesema wanaostahili kulipwa fidia ya ardhi ni wale wenye hati za makazi pekee.
Amesema tayari mazungumzo na walengwa wenye sifa yamefanyika na kwa sasa wanasubiri kuidhinishiwa fedha na Serikali ili waanze mchakato wa malipo.
“Kama ilivyoamuliwa, wale wasio na hati za makazi wanalipwa kifuta cha Sh4 milioni na huo ndio msimamo wa Serikali, lakini kwa wale wenye hati, malalamiko yao yamesikilizwa na tayari imeamuliwa walipwe; tunachosubiri sasa ni fedha zao kuidhinishwa ili tuanze kuwalipa,” amesema Kalapilo.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto zilizopo, mradi unaendelea kama kawaida na tayari zabuni za kuwapata makandarasi zimeshatangazwa.
Hii imethibitishwa na mmoja wa waathirika, Tomson Moshi, ambaye amesema mwanzoni mwa mwezi huu aliitwa ofisi za Tarura na kufanya mazungumzo nao kuhusu malalamiko yake.
Moshi amesema japokuwa si kiwango cha fedha alichokitarajia, anashukuru kwamba angalau wamesikiliza hoja zake, ingawa uamuzi umechelewa.
Awali, Moshi alikuwa akidaiwa kulipwa fidia ya makazi ya Sh276, 000 pekee, lakini sasa anatarajia kulipwa Sh600 milioni. Kwa upande wa fidia ya ardhi, anatarajia malipo yapande kutoka Sh4 milioni hadi Sh60 milioni.